Miaka michache iliyopita, Bandari ya Dar es Salaam ilikuwa na changamoto ya usalama wa mizigo ya wateja. Mhandisi Deusdedit Kakoko alipoteuliwa Juni 25, 2016 kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), aliahidi kuimarisha ulinzi na kuondoa udokozi bandarini.

Mhandisi Kakoko alisema usalama wa mizigo ya wateja unapaswa kuwa namba moja na huo ndio msingi wa Bandari ya Dar es Salaam na nyingine zote nchini kuaminiwa na kuzidi kupata wateja. “Tulisema usiibiwe mzigo hata mmoja. Atakayethubutu, afahamike na kukamatwa. CCTV Camera zimetusaidia mno. Kwa sasa mizigo ya wateja ni salama 100%,” amesema Mhandisi Kakoko.

TPA katika kuboresha ulinzi bandarini imeweka mfumo maalumu wa ulinzi unaoitwa Integrated Security System (ISS). Mfumo huu unahusisha; kamera maalumu ambazo zipo 486 (CCTV Camera) na zimewekwa kila sehemu bandarini, vifaa maalumu vya kusoma vibao vya namba za magari ambavyo vimewekwa kwenye mageti bandarini na mashine za ukaguzi wa mizigo midogo midogo (X-rays).

Pia kuna mashine za ukaguzi wa watu wanaoingia na kutoka bandarini (walk through metal detectors), turn styles kwa ajili ya kudhibiti upitaji wa watu getini, bollards na barriers kwa ajili ya kudhibiti upitaji wa magari getini, vifaa maalumu vya kubaini urukaji ukuta au uzio bandarini (perimeter intruder detection system) na taa maalumu kuongeza mwanga usiku.

Bandari ya Dar es Salaam ni lango kuu la biashara kwa nchi yetu na nchi zote zinazotumia bandari hii. Bandari inahitaji ulinzi madhubuti na wa kiwango cha hali ya juu. Kutokana na umuhimu katika nyanja za uchumi na biashara, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeimarisha na inaendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa bandari, ikiwemo watu, mizigo, vifaa na meli bandarini kwa kuzingatia International Ship and Port Facility Security Code (ISPS) na Merchant Shipping Act ya mwaka 2004.

Bandari za TPA zinatekeleza kikamilifu masuala mbalimbali ya ulinzi kama yalivyoainishwa katika sheria mpya ya kimataifa ya Ulinzi wa Bandari na Meli ya Mwaka 2004 kutokana na Tanzania kuridhia utekelezaji wa Sheria ya International Maritime Organization (IMO) iliyoundwa kudhibiti vitendo vya kigaidi kupitia njia ya meli na bandari.

Ulinzi wa bandari umejikita katika maeneo ya meli, mizigo na watu. Katika uingiaji wa meli katika Bandari ya Dar es Salaam, hupata taarifa kupitia mnara wa kuongozea meli (control tower) pamoja na ratiba za uingiaji wa meli zinazopatikana katika vikao vya upangaji uingiaji meli kupitia wakala wa meli husika.

Meli ikiingia bandarini huwekeana makubaliano yanayohusiana na hali na usalama wa meli na bandari yanayokuwa katika hati inayoitwa Declaration of Security (DOS). Pia nyaraka zilizotuma mizigo na zenye maelezo ya mizigo zinazotumika katika kupokea na kuhifadhi au kutoa mizigo Bill of Lading na Manifest.

Kwa upande wa baharini, TPA kupitia kikosi chake cha ulinzi cha Auxialiary Police, kuna boti maalumu zinazolinda mlango wa bandari na sehemu ambayo meli husubiri kuingia bandarini (entrance channel) pamoja na eneo lote la boya la mafuta la Single Point Mooring. Pia kikosi cha ulinzi cha TPA katika ulinzi wa eneo la baharini hushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kama Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Polisi kuhakikisha usalama wa meli.

Ulinzi wa mizigo huanza tangu inaposhuka kutoka melini mpaka inapotoka eneo la bandari kwa kuchukuliwa na wahusika au mizigo inapoingia bandarini mpaka inapopakiwa melini. Ni jukumu la TPA kuhakikisha mizigo ya wateja inakuwa salama wakati wote inapokuwa bandarini.

Uingizaji au uchukuaji wa mizigo bandarini ni lazima ufuate au uzingatie sheria na utaratibu wa kiforodha, ukaguzi na kupata vibali au nyaraka zinazohusika katika kuchukua au kusafirisha mzigo. Iwapo mhusika hatakuwa na nyaraka husika katika kusafirisha au kuchukua mzigo bandarini hataweza kuruhusiwa kuchukua au kuingiza mzigo bandarini.

Uingiaji wa watu bandarini ni lazima uzingatie sheria na taratibu zilizopitishwa na mamlaka husika. Kila mtumiaji wa bandari kwa maana ya wadau wa bandari ni lazima wawe na vibali maalumu vya kuingilia bandarini. Vibali hivyo vinaweza kuwa ni kitambulisho kilichotolewa na TPA, kitambulisho cha mfanyakazi wa TRA, LATRA, taasisi za Ulinzi na Usalama kwa taarifa bandarini na ruhusa ya maandishi kutoka kwa viongozi wa TPA. Hata wafanyakazi wa TPA ni lazima wavae vitambulisho wanapoingia bandarini na wakati wote wakiwa kazini bandarini. Hakuna mtu anayeruhusiwa kuingia bandarini bila kibali au kitambulisho.

Mfumo wa ulinzi umeimarishwa na umeendelea kuimarishwa bandarini. TPA imewajengea uwezo askari wetu kwa kuwapatia mafunzo maalumu kuhakikisha usalama wa meli, mizigo ya wateja, miundombinu ya Mamlaka na watu wote wanaoingia bandarini.

Ili kuimarisha ulinzi upande wa majini au baharini, TPA imenunua boti maalumu mpya za kutosha. Boti hizo ni kwa ajili ya bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga, ambapo kila bandari imepata boti za kutosha.

Katika kuimarisha ukaguzi wa makasha yote yanayopita bandarini, TPA ina mashine maalumu (scanners) za kukagulia makasha yote yanayoingia au kutoka bandarini. Pia TPA imo katika hatua za mwisho za uwekaji wa mashine nyingine 3 mpya,  ikiwemo moja itakayokagua makasha yanayoingia au kutoka kwa treni. Lengo ni kuhakikisha mizigo yote inayopita bandarini ni salama na halali.

“Kutokana na kuimarishwa ulinzi katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita hakuna wizi wowote wa mizigo ya wateja uliotokea. Jitihada hizi pia zimechangiwa na ulinzi shirikishi wa wafanyakazi wote, ambapo licha ya kuwepo kwa askari wenye jukumu la ulinzi, lakini kila mfanyakazi ni mlinzi,” amesema Kakoko.

Amewapongeza wafanyakazi wa bandari kwa kuwa wazalendo na kushiriki kuimarisha usalama, hali inayoipa bandari fursa ya kufanya biashara kwa utulivu na kupata wateja wapya siku hadi siku.

Wadau na wateja wote wa bandari ni wajibu wetu kusaidiana na Mamlaka husika kuhakikisha bandari zetu ni lango salama la biashara na uchumi. Iwapo kutakuwa na tatizo wakati wa kuchukua mzigo wako bandarini usisite kuwasiliana nasi kwa kupiga simu au kutuma meseji za bure 0800110032 au 0800110047.