Siku za karibuni yamekuwapo malalamiko yasiyo rasmi juu ya wateja kucheleweshewa mizigo inayosafirishwa nje ya nchi. Kutokana na hali hiyo, Bandari imebaini kwamba, kwa kuwa Tanzania inaingia kwenye uchumi wa viwanda kwa kasi, kuna uwezekano kuwa baadhi ya watu wanazalisha mazao au bidhaa za kuuza nje ya nchi hawafahamu vema taratibu za kusafirisha mzigo nje ya nchi.

Kutokana na hilo, Bandari imeona ni vema ieleze utaratibu unaopaswa kufuatwa kwa nia ya kuepusha mzigo wa mteja kuchelewa kusafirishwa. Kimsingi Bandari imebaini katika malalamiko hayo kuwa wasafirishaji wa mizigo nje ya nchi huenda kuna taratibu hawazifahamu au hawazikamilishi kabla ya kupeleka mzigo bandarini.

Bandari kama Bandari haiwezi ikachelewesha mzigo wa mtu. Chanzo cha kuchelewesha mzigo wa mtu ni mambo mawili tu; kwamba huyo mteja akute bandarini vyombo vya kupakia au kupakua vimeharibika vyote, tatizo ambalo halijawahi kutokea katika bandari zetu ikiwemo ya Dar es Salaam, lakini ya pili ama mteja mwenyewe hajailipa bandari au hajakamilisha taratibu za vibali vya TRA au taasisi nyingine za serikali.

Kwa mizigo inayoharibika kama maparachichi unapaswa kuwekwa kwenye ‘refer containers‘, ambazo ni makontena yenye jokofu. Mteja anatakiwa kufahamu bidhaa yake inahitaji ubaridi kiasi gani, ili yakae miezi miwili bila kuharibika kwani kuna joto ambalo ukiweka matunda hayawezi kuharibika. Pia muda wa matunda yenyewe, yaani wakati matunda yanapovunwa na kuwekwa kwenye vifungashio yalikuwa na muda gani.

Hata hivyo, kutokana na malalamiko hayo, Bandari imeona ni vema ikaeleza utaratibu sahihi wa jinsi ya kusafirisha mzigo nje ya nchi. Bandari imekuwa ikisafirisha samaki, njegele, matunda na vitu vinavyoweza kuharibika haraka, ila hatujawahi kusikia malalamiko kwa kuwa wanafuata taratibu zote.

Maelezo haya ni muhimu katika sekta ya usafirishaji hasa tunapoelekea kwenye uchumi wa viwanda ni Usafirishaji wa mizigo ng’ambo. Lengo la makala hii ni kuelezea hatua muhimu ambazo msafirishaji anatakiwa kuzifuata ili aweze kusafirisha mzigo wake kwenda ng’ambo kupitia bandari zetu, kuanzia kupata vibali, ukaguzi, kulipia na hatimaye kusafirisha.

Hatua ya kwanza ambayo msafirishaji anatakiwa kuichukua ni kumpata wakala wa forodha ambaye atamsaidia kuhakikisha mzigo wake unapitia hatua zinazotakiwa mpaka kuusafirisha. Kama msafirishaji huyo ni mara yake ya kwanza kusafirisha mzigo kwenda ng’ambo, wakala anatakiwa amsaidie msafirishaji huyo kupata vibali (export permits) vinavyotakiwa kutoka katika mamlaka husika kulingana na aina ya mzigo.

Baada ya kupata kibali cha kusafirisha, wakala wa forodha anatakiwa kupata nyaraka ya kuchukulia  kontena kutoka kwa wakala wa meli (shipping agent), ambapo atapata gharama za kusafirisha mzigo (freight charges). Pia katika hatua hii, wakala atapatiwa nyaraka ya kusafirishia mzigo ambayo inaitwa shipping order.

Shipping order ni nyaraka inayotengenezwa na mteja akishirikiana na wakala wake ili kumsaidia kuitumia wakati wa kutoa taarifa za mzigo kwenye mfumo wa TRA uitwao Tancis.

Hatua inayofuata ni wakala kuchagua eneo maalumu kwa ajili ya kupakia mzigo kwenye kontena chini ya uangalizi wa ofisa wa TRA ambaye pia atafanya ukaguzi kwa kushirikiana na mamlaka zingine za serikali. Baada ya kufanyika kwa ukaguzi, ofisa huyo atafunga kontena kwa kutumia lakiri (seal) ambayo ina namba maalumu, pia wakala wa meli naye atafunga seal ya kampuni yake ya meli.

Wakala wa forodha akishakamilisha hatua hiyo, atatakiwa kuingia kwenye mfumo wa Tancis ili kuingiza taarifa za mzigo wa mteja wake ambapo atapata nyaraka inayoitwa Tansad na nyaraka inayomruhusu kusafirishia mzigo (release order). Tansad ni nyaraka yenye taarifa za shipping order, orodha ya upakiaji vitu kwenye kontena (packing list), na stakabadhi ya malipo.

Baada ya kupata vibali vya TRA, wakala wa forodha atatakiwa kuviwasilisha TPA kwa ofisa anayehusika ambaye ataingiza taarifa za mzigo kwenye mfumo wa TPA unaohusika na mizigo (cargo system). Hatua hiyo itamwezesha wakala kuingia kwenye mfumo wa malipo wa TPA wa kielektroniki (e-payment system) ambapo atapata namba ya kumbukumbu ya kulipia tozo za TPA (payment reference number – PRN) kupitia benki mojawapo kati ya TIB, NMB, CRDB na Standard Chartered au kwa njia ya simu.

Wakala akishakamilisha malipo ya TPA, ataingia kwenye mfumo wa TPA kutoa taarifa za mzigo ili aweze kuingiza taarifa za gari na dereva, kisha aingize mzigo husika bandarini. Taarifa atakazoingiza kwenye mfumo wa TPA ni pamoja na namba za lori litakaloleta mzigo bandarini, namba za kontena, jina la dereva na namba ya leseni ya dereva.

Baada ya kuingiza taarifa hizo kwenye mtandao wa TPA, wakala atapatiwa kibali kwa ajili ya kuingiza kontena bandarini. Baada ya kontena kufikishwa bandarini litapakiwa kwenye meli ili kusafirishwa kwenda ng’ambo.  Mara baada tu ya kupakia kontena kwenye meli na meli kuondoka kutoka bandarini, wakala wa forodha kwa kushirikiana na wakala wa meli wataandaa bill of lading na kuituma kwa mteja aliyenunua mzigo unaosafirishwa.

Bill of lading ni nyaraka yenye jina na anuani ya muuzaji mzigo, jina la nchi ulikonunuliwa mzigo, aina ya mzigo, namba za kontena lililopakiwa mzigo, jina la bandari lilikopakiwa kontena, jina la meli iliyochukua kontena, jina la aliyenunua mzigo na anuani yake na jina la bandari ambako kontena litakakoteremshwa.

Ni muhimu sana kuzielewa hatua hizi za usafirishaji wa mizigo kwenda ng’ambo hasa kwa wakati huu ambao Tanzania imo kwenye mapinduzi makubwa ya kuingia kwenye uchumi wa viwanda. Kwa kuwa uzalishaji bidhaa katika viwanda utalenga soko la nje, ni vizuri kwa wazalishaji wa bidhaa za viwandani wakazielewa hatua hizi ili kuwawezesha kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi. 

Iwapo una tatizo au swali kuhusiana na huduma za bandari, usisite kuwasiliana nasi kwa kupiga simu au kutuma meseji za bure kupitia namba 0800110032 au 0800110047.