Kwa muda wa miaka minne sasa gazeti hili la JAMHURI limekuwa likiandika habari za uozo katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA). Katika maandishi hayo tumebainisha suala la upotevu wa makontena, vibarua hewa, usitishaji wa matumizi ya flow meter za mafuta, wizi wa mafuta, malipo hewa, wizi wa mali za wateja, ukosefu wa CCTV cameras, uongozi wa kiimla, ubadhilifu na mengine mengi.

Tumeifanya kazi hii kwa uzalendo wa hali ya juu. Baadhi ya watu waliibeza kazi ya mikono yetu wakati tunaanza kuifanya na wengine wakatumika kutufungulia kesi zisizo na kichwa wala miguu mahakamani kama akina Madeni Kipande na wapembe wake, lakini bado mkono wa Mungu uliosheheni haki ukashinda hila zao.

Ni kwa bahati mbaya kuwa baadhi ya watu walizitafsiri habari tulizoandika kama zililenga watu binafsi badala ya kuangalia masilahi mapana ya taifa. Tunajua habari tulizoziandika zimewanyang’anya tonge mdomoni mabazazi wengi na baadhi wamepoteza kazi, na sasa tunashuhudia juhudi kubwa wanazofanya kujisafisha kwa mfano katika suala la kusitisha matumizi ya flow meters kwa miaka mitano tuliyoibua.

Mtu kama Kipande, Kamati iliyoundwa na Samuel Sitta ilitoa ripoti iliyodhihirisha kuwa pale Bandari hakukuwapo uongozi chini yake, bali kuligeuzwa kambi ya mateso. Si nia yetu kurejea historia, ila kwa ufupi tu, wiki iliyopita tumeibua tena suala la mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya viongozi wa Bandari ya Dar es Salaam kujipatia fedha binafsi kwa gharama ya kushusha uchumi wa nchi.

Katika habari hiyo, tumeibua uozo unaoonyesha kuwa baadhi ya viogozi wa Bandari wanashirikiana na wafanyabiashara binafsi kuhamisha mizigo kutoka Bandari kwenda kwenye Bandari Kavu (ICDs). Si hilo tu, hata mashirika ya meli wameyahamisha kutoka Bandari kwenda kwa washindani wa Bandari. Kwa kufanya hivyo mapato ya Bandari yanashuka, ila wao na familia zao wananeemeka.

Tumeandika kuwa Bandari ya Dar es Salaam ina uwezo wa kuhuhifadhi kontena 8,500 kwa sasa, ila kwa faida biafsi, pamoja na mzigo kupungua hadi kontena 600 wakubwa hao wamekuwa wakihamisha asilimia 75 ya kontena hizo chache kwenda ICDs. Baada ya habari hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Deusdedit Kakoko, amesitisha utaratibu huo.

Katika habari tuliyoichapisha leo, baadhi ya wamiliki wa ICD wanalalamika kuwa Bandari inawanyima mizigo hivyo biashara yao inakufa. Meneja Mawasiliano wa Bandari, Janet Ruzangi, amebainisha kuwa kwa sasa Bandari inayo nafasi ya kutosha na hao wa ICD watapata mizigo baada ya Bandari kujaa. Amewataka warejee mikataba kati yao na Bandari.

Sisi tunampongeza Kakoko na Serikali kwa ujumla kwa kufanyia kazi habari tunazozichapisha. Tunapendekeza wote waliohusika na mchezo huu wa kupeleka kontena na magari ICD wakati Bandari kuna nafasi, si tu wasimamishwe kazi, bali wachunguzwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa kosa la kuhujumu uchumi uhusika wao ukithibitika. Mungu ibariki Tanzania.