Novemba 5, mwaka huu Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli inatimiza miaka minne madarakani. Katika kipindi hicho kifupi, serikali imefanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa uendeshaji wa bandari za Tanzania na imeleta maendeleo makubwa hadi vijijini chini ya usimamizi imara wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari inayoongozwa na Prof. Ignatus Rubaratuka.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, amefanya Mahojiano Maalumu na JAMHURI. Katika sehemu ya kwanza ya mahojiano hayo wiki iliyopita alieleza majukumu ya bandari na mabadiliko ya kimfumo yaliyofanyika.
Leo anaanza kwa kueleza maendeleo yaliyopatikana katika bandari za maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa katika sehemu hii ya pili ya mahojiano hayo. Endelea…
Kwa hiyo hizo ni bandari, lakini kule kwenye Ziwa Victoria tuna bandari kubwa ambazo ni Mwanza, Bukoba, Kemondo, Nansio – Ukerewe kule na Musoma. Na tuna bandari nyingine ndogo ndogo ambazo nazo tunazitengeneza. Kwa mfano tuna Magarini, tuna Kyamkwikwi, tuna Nyamilembe, tuna Chato, Nkome… Nkome na Kome ziko mbili, moja Geita, moja Sengerema, kule Nkome ya pili inaitwa Rushamba, lakini ipo kwenye kisiwa kile, samahani inaitwa Ntama, kwa hiyo tuna Rushamba, lakini pia tuna Ntama ambayo ipo kwenye Kisiwa cha Nkome.
Kwa hiyo hizo zote ni bandari tunazoshughulikia kule.
Ziwa Tanganyika, tunayo Bandari ya Kagunga, ambayo iko mpakani mwa Burundi na imeboreshwa, imepandishwa chati, lakini tuna Kibirizi pale, Ujiji na Kigoma. Hizi ziko pamoja, zitakuwa zinatengeneza bandari moja kubwa ya Kigoma huko mbele, ingawaje kwa sasa zimeachana, lakini kule mbele zitakuwa ni vituo au terminals ambazo zitatengeneza mfumo wa bandari moja ya Kigoma.
Lakini tuna Bandari ya Kalya au Sigwesa, tuna Lagosa, tuna Kipili, tuna Kabwe, tuna Kasanga. Lakini zipo ndogo ndogo zaidi ambazo sasa tulikuwa hatujazichukua kama Mwampemba, ambayo inatakiwa sasa iingie. Kuna nyingine ndogo ndogo katikati humo. Hizo ni zile ambazo zilikuwa bubu, lakini sasa tumepeleka vifaa pale, ili tuanze kutoza.
Na Lake Nyasa tunazo nyingine takriban 15, nitazitaja chache. Itungi na Kiwira zile zipo, ndizo zilizopo kubwa, lakini tuna kule Manda – Ludewa ndiyo bandari kubwa, ambayo ni kwa Mkoa wa Njombe na tuna Mbamba Bay, ambayo ni kubwa pia kwa upande wa Mkoa wa Ruvuma, lakini zipo nyingie kama Liuli na Matema na nyingine za aina hiyo. Kwa sababu mtaona zote hizo.
Na huko nyuma nilisema kwamba baada ya uchumi kuwa unakwenda vizuri na Watanzania wanaongezeka, basi kila eneo linakuwa na maendeleo. Mlimwona Mheshimiwa Rais, hata wakati ule anazunguka akitafuta ridhaa ya Watanzania, alipita katika maeneo hayo, mengine kulikuwa hata madaraja hakuna ndiyo yamejengwa sasa hivi. Mito kama Luhuji kule, bandari ziko kule sasa, vijiji vingine hata kufikika havifikiki vinaingia kwa meli tu, barabara ndiyo kwanza zimeanza kufunguliwa sasa hivi.
Kwa hiyo bandari ni muhimu hata upande ule na ndiyo maana hata ile meli sasa ambayo imeishaingizwa kwenye maji imekamilika, itakapoanza kazi mwishoni mwa mwezi huu au mwezi ujao, mwezi huu tunatarajia tutapata kibali cha TASAC, basi itakuwa kwa kweli ni wokozi mkubwa ikiwa inatembea katika Ziwa Nyasa kwa vile vijiji ambavyo tuna bandari ndogo ndogo zile, lakini havifikiki kwa magari na sisi tutaendelea kujenga gati ndogo ndogo, ambazo kimsingi zitawahudumia hawa wananchi ambapo wakitoka kwenye vijiji vyao kwenda kupanda meli na mama zetu pale wasiwe na haja ya kupandisha nguo kutembea kwenye maji.
Kwa hiyo, unakuwa na gati ndogo ndogo zinazoingia mita 50. Kwa hiyo ile meli inafunga pale unakuwa na zile nguzo zake za kwenye maji, unaingia kwenye meli moja kwa moja. Sasa hayo ndiyo matunda ya Serikali ya Awamu ya Tano, maana hayo ni maono mapya kwa ajili ya huduma kwa wananchi kwa kila eneo, na nadhani inakuwa ni muhimu kutambua juhudi hizo na kufahamu kwamba serikali yao kwa kweli inafanya kazi. Sisi ni mikono tu, lakini serikali ipo kazini.
Kwa hiyo hilo ni eneo la pili ambalo ningependa nizungumzie baada ya kuzungumzia majukumu yetu, basi mjue maeneo ambayo tumesambaa. Katika muda ambao utakuwa si mrefu tunafanya tathmini ili tuweze kuingia kabisa katika Ziwa Rukwa, kwa sababu Ziwa Rukwa halikuwa sehemu ya mtandao wa bandari zile za Marine Services Company Limited, basi lenyewe halikuingia chini ya huduma za TPA kwa sababu halikurithiwa, halikuwepo.
Lakini kama ninavyosema, tunachanja mbunga tunaendelea kutanuka, basi na lile ziwa tunaangalia uwezekano wa kulichukua kama litakuwa linaweza likahudumia vyombo vya usafiri majini, yaani navigability. Sasa tunahudumia nini? Maana kama tunahudumia lazima kuna kitu tunakihudumia. Biashara ya bandari inahusisha biashara, inahusisha pande mbili kubwa. Nilisema pale mwanzo kwamba tunafanya na sisi tufanya na sisi utekelezaji.
Upande mmoja ni inakotokea sehena, upande wa pili ni inakoelekea shehena. Inakotokea shehena, kule tunaita kwa shippers au suppliers, wale ambao wanaanzisha shehena kuileta, kuipakia kwenye meli kuileta. Kwa hiyo kule tuna shipper, tuna mwenye mzigo aliyekuwa anamiliki mzigo sasa anaukabidhi kwenye chombo cha usafiri, yule ndiye shipper au supplier.
Upande ule sasa tuna mwenye meli, ambaye ni liner, shipping line, si ndiyo. Kwa hiyo shipper na shipping line ndiyo waanzishaji wa shehenani wanayoipeleka bandarini. Shipping line kwa sababu ni kama wenye mabasi, hatutarajii mwenye basi. Hatutarajii mwenye mabasi 50 au 100 yeye atakuwa ndiye huyo huyo atapita kwenye ofisi zote ambako mabasi yake yanapita. Atakuwa na wakala, si ndiyo?
Kwa hiyo shipping lines zina wakala, wakala wa meli wale ambao tunawaita ma-shipping agents. Kwa hiyo shipping agent yeye ameajiriwa na shipping line. Na wale shipping agent na shipping liner au shipping line, wao ni wasafirishaji, wanaochukua shehena kwa mtu fulani ambaye ni shipper au supplier.
Kwa sababu wao hawamiliki ile shehena, basi wataifikisha bandarini. Wakishaifikisha bandarini, huo ni upande wa kwanza tumekamilisha, tunapokea. Tunaipeleka upande wa pili kwa yule mwenye sehena aliyeiagiza au aliyeinunua, ambaye ndiye atakayeichukua kuitumia. Kwa hiyo yule anaitwa consignee au cargo owner.
Sasa na kwa sababu wao ni wengi, wengine wako Zambia, ambako hakuna bandari, wengine wako Congo DRC, wengine wako Burundi, wengine Rwanda, wengine wako Mwanza, wengine Singida, hata wengine Dar es Salaam hapa hapa, lakini wana kazi zao.
Kwa hiyo kwa utaratibu ambao upo kimataifa na uliokuwepo, wale watamtafuta pia wakala. Wakala wa shehena au wakala wa mwenye shehena, siku hizi tumezoea kuwaita wakala wa forodha, lakini kimsingi wale, wale wanafanya uwakala kwa mwenye sehena.
Wanasimamiwa na forodha kwa sababu kazi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni kufukuzana na ile shehena kuhakikisha mapato yanapatikana. Ndiyo kazi yao kuu. Wakati bandarini sisi tukipokea na kutunza kwa muda shehena ile, anayeangalia na kuhakikisha kwamba haiendi hovyo hovyo ikapotelea mtaani bila mapato ni Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Kwa hiyo ndiyo maana hawa wakawa mawakala kwa sababu walikuwa wanasimamiwa na Mamlaka ya Mapato kuhakikisha hawapotezi shehena ile mtaani, labda wakisingizia kwamba inakwenda Congo au Zambia kumbe imeishia Iringa au Mbeya. Kwa hivi ndivyo tulivyogawana.
Na ndani ya Bandari, eneo la tatu ninalolizungumzia ni wadau wa Bandari. Ziko taasisi za umma kwa sasa 34, kwa hiyo wakati mwingine hata nyie waandishi wa habari, lakini hata viongozi wetu, wakiona kila kinachotokea bandarini basi watajua ni cha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, kwa hiyo mmoja wetu kati ya hawa 34 anaweza akamkosea mteja, huyo mteja kama tulivyosema ni yule wa upande wa shipping agent, ambaye ndiye amempokea kwa shipping agent, ambaye ndiye ameupokea kwa shipper au supplier, lakini pia anaweza akawa amemkosea mteja mwenye shehena mwenye mzigo ambaye anawakilishwa, anakuwa represented na wakala wa shehena au wakala wa forodha kama nilivyosema.
Sasa anakuwa amemkoseaje? Jambo la kwanza na la msingi sana ambalo linatakiwa lifanyike bandarini, kwa kweli ni ufanisi. Ufanisi katika kuhakikisha kila kitu kinakwenda ndani ya muda. Kwa sababu hizi ni biashara ya watu. Na tumeona katika biashara zote zinazofanyika duniani, biashara zozote, asilimia 80 ya biashara zote duniani, ni maritine based. Zinatokana na usafiri wa majini na nchi kavu kwa pamoja. Kwa hiyo zinapita bandarini, na hata katika biashara za Tanzania imeonekana hivyo.
Kwa hiyo tunakuwa na umuhimu kwa sababu, ukichelewesha shena ya mtu, tayari ana oder Krismasi au ni wakati wa Mwezi Mtukufu, Mfungo wa Ramadhani na ameleta tende wewe unakaa nazo, unazotoa baada ya mfungo umekwisha, kwa vyovyote vile, unakuwa umecheza na ufanisi na umeharibu biashara. Sasa kati yetu sisi na kama tunavyojua kwa nini tulipoteza biashara kwa njia moja au nyingine huko nyuma, inawezekana hatukuwa na ufanisi wa kutosha.
Sasa ufanisi unapimwa kwa sababu unaona wadau ni wengi, mikono ni mingi. Ni lazima tuhakikishe kwamba tunakuwa na muda, ambao tumejipangia, wote kila mtu anapewa muda, ambao amejipangia na anatekeleza jambo lile la upande wake katika muda. Tunalo eneo la nyaraka, documentation ni problem linatuchelewesha sana. Kati ya mawakala, sisi na mashirika ya umma, vyombo vya umma. Taasisi zinazohusika, tumekuwa na ucheleweshaji unatuletea matatizo.
Lakini eneo la pili tunaloliangalia, ni usalama. Ulinzi na uslama. Ziko meli za watu ziko pale, nyingine zinakuwa kule nje mnaziona. Zile zinatakiwa zije zikae salama, zifunge salama, zishushe na kupakia mzigo salama, ziondoke salama.
Ikiguswa meli na zile zinatembea kimataifa, nimetoa mfano wa mabasi, yanatoa Moshi, yatapita yatashuka Makanya, sijui Same, sijui Korogwe na meli hivyo hivyo, itatoka Japan, itapitia itatia nanga Singapore, itakuja India, itakuja Arabuni, itapita South Afrika au Kenya, itakuja Tanzania, itakwenda wapi. Kwa hiyo, ni chombo cha kimataifa, na wafanyakazi wa kimataifa, shehena ya kimataifa, nyaraka za kimataifa.
Sasa ikirudi ikiwa imepata matatizo, basi ujue umeharibu biashara. Kwa sababu meli zote zitakukimbia. Kwa hiyo tunahakikisha suala la usalama. Lakini usalama pia wa mali za watu.
Ikatokea, bahati mbaya, Mungu apishe mbali, shehena ya watu ikadondokea majini, au balaa kama la moto. Lakini kuna usalama wa wizi wa udokozi udokozi, yote haya ni masuala ya biashara, unakuwa umeharibu biashara na huwezi kupata wateja tena.
Kwa hiyo tunayo kazi kubwa ya kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, kuhakikisha kwamba vifaa vya watu, ikiwa ni pamoja na meli, lakini na shehena zinalindwa. Huko nchi kavu, kuna rasilimali za umma, majengo haya. Lakini tuna mali za watu nyingi sana.
Ukihesabu mali za watu ambazo zinakuwa pale bandarini, wakati mwingine huwezi kwenda kulala nyumbani. Unakaa unaangalia kitu gani kitatokea. Hivi hizi juhudi zote zilizowekwa, za kuhakikisha kuna ulinzi na usalama, tuna kikosi kikubwa kabisa kabisa karibu katika nchi nzima isipokuwa cha zima moto, inatosha?
Kwa hiyo, hiyo ni kazi yetu kubwa ya pili, ambayo lazima tuhakikishe, vinginevyo likitokea tukio moja, umepoteza biashara na umepoteza mapato ya serikali. Umepoteza maisha mbalimbali kwa sababu biashara ndiyo shughuli ya watu, shughuli ya wananchi. Kwa hiyo tunakuwa makini kwenye eneo hilo.
Lakini la tatu ni masuala ya afya. Kwa sababu kwenye bandari zote kunakuwa kuna mkusanyiko wa watu. Na tunazo sheria, chini ya mamlaka zinazosimamia afya, lazima tutekeleze hizo. Na sheria nyingine mbalimbali za aina hiyo.
Tuna masuala ya mionzi. Kuhakikisha tuna usalama, hatuleti vifaa vinavyotoa mionzi, ambavyo vinaweza vikahatarisha usalama kwa upande wa mionzi. Kwa hiyo na mambo mengine mengi ya aina hiyo, unaweza ukasema ukafika mpaka keshokutwa.
Kwa Mamlaka ya Bandari, Usimamizi wa Bandari Tanzania tunalo jukumu ambalo ni pana na sisi tunakuwa ni wenyeji wa mamlaka zote hizo, na ndiyo maana, tuna jukumu ambalo ni la ziada la kuhakikisha tunaratibu, tunaunganisha, wadau wote hao wa umma.
Wapo wengi wanaotoa vibali. Wako TBS, ambao wanaangalia viwango, wapo wanahusika na vipimo, wapo kina EWURA, wapo wanaongalia dawa, wanaoangalia vyakula, lakini kama nilivyosema afya, hata hili jengo hili ambalo tumo tumewachukua wale waangalizi wa afya kwa sababu wale ndiyo kwanza, wanaangalia mabaharia wakiingia.
Kabla mtu yeyote hajaingia kwenye meli, wanaingia kupima afya. Isije ikawa anaingia, huko alikotoka amekuja na magonjwa mbalimbali yanayoweza kutuathiri. Lakini pia baada ya hao, tuna mpaka watu wa uhamiaji.
Kwa hiyo wote hao tunafanya nao kazi kwa pamoja. Ndiyo maana nimewaambia tukiwajumulisha watafika 34. Wanakuwa bandarini. Nimesikia juzi, nimeona waandishi mnaandika masuala ya NEMC na mambo ya mifuko, nadhani baadhi yenu mlikuwa hapa, basi huwezi kuingia sana lakini tulikuwa na Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana anayehusika na huduma hizi.
Kwa hiyo wale wote tunao hapa. Tunayo Mamlaka ya Misitu, tunasafirisha sana, tunauza nje mbao. Kwa hiyo wote hawa ukiwataja wako hapa. Tunao wadau wa reli, ambapo Mheshimiwa Rais anatuachia reli yenye nguvu, ambayo ni sawa na semi-treler 500 kwa wakati mmoja, inaondoa mzigo pamoja. Kwa sababu ni mdau mkubwa sana TRC, lakini kwa sasa bado anaongeza uwezo yeye na TAZARA.
Katika tani, takriban milioni 5 na nusu tunazopeleka nje za transit ambazo siyo local, local tuna tani karibu milioni 11.5 kati ya tani milioni 17.1 tulizozifanya, milioni 5 ni za kupita – ni transit, zinakuja au zinakwenda, wao kwa pamoja hawajaweza kufikia kusafirisha asilimia 1. Kwa hiyo asilimia 99 inasafiri kwa barabara na zaidi. Kwa sababu asilimia 1 ya tani milioni 5 ni tani 50,000 kwa hiyo wakifanya biashara za ndani na biashara za nje, sasa hivi ndiyo wanakwenda kwenye hicho kipimo.
Kwa hiyo tunataka reli isafirishe haidhuru, asilimia 15 hadi 30. Kwa hiyo hao ndio wadau, nimeona ni eneo la tatu tunaweza tukalizungumzia kwa pamoja, tukashirikishana. Na faida yake sasa ni kwamba mtakapokuwa mnaandika, sisi kama waratibu tutakuwa pamoja na wahariri, tutakuwa pamoja na waandishi, lakini mtaujua ukweli kwa kina kwamba chanzo cha hili tatizo ni sekta ipi hapa? Ni shirika lipi? Kwa sababu ni suala la kupata ule uelewa. Lakini hatukwepi jukumu letu la kuratibu.
Kwa hiyo kama serikali inatoa maelekezo, siwezi kusema hili ni la Mamlaka ya Misitu, hapana. Nitalitekeleza, nitamtafuta yule wa misitu tufanye kazi na yeye, lakini ni vizuri kufahamu kwamba hao wadau tunafanya nao kazi kwa namna hiyo. Kwa hiyo, hiyo ni awamu ya kwanza, ambayo ningependa tushirikishane, awamu inayotuzungumza sisi ni nani, na tunafanyaje kazi, jukumu letu likoje, nini wajibu wetu kama mamlaka?
Kabla sijaeleza sasa tulikotoka, angalau katika kipindi cha miaka mitatu, mitano, sijaeleza biashara yetu imekuwaje, na awamu ya mwisho nitapenda kuzungumzia, labda miradi kiasi fulani. Sasa labda kwa hapo nilipoishia, niwasikilize ninyi ili baadaye niweze kuendelea.
Je, unafahamu mageuzi makubwa iliyofanya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli? Usikose nakala yako Jumanne ijayo kupata sehemu ya tatu ya mahojiano haya.