SERIKALI ya Tanzania imekuwa ikiboresha bandari nchini kote ikilenga kurahisisha huduma za usafirishaji wa majini kwa ajili ya Watanzania na nchi nyingine zinazotumia bandari za Tanzania.
Moja ya bandari ambayo inaboreshwa kwa kiwango kikubwa ikiwa ni pamoja na kujengwa gati la kisasa na eneo la kuhifadhia mizigo ni Bandari ya Mtwara.
Katika mahojiano na gazeti hili hivi karibuni, Mkurugezi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, anasema kwamba TPA inapanga kujenga gati mpya nne katika Bandari ya Mtwara kuanzia sasa hadi mwaka 2025.
Anasema wanaimarisha Bandari ya Mtwara kutokana na idadi ya shehena kuongezeka kwa kasi na shughuli zinazotokea kusini mwa Tanzania na nchi za jirani.
Mkurugenzi Mkuu anasema bandari hiyo ilikuwa na gati moja pekee ambalo limehudumu kwa muda mrefu na kwamba mwaka juzi lilikaribia kufikia ukomo wake baada ya kusafirisha tani 400,000.
Anasema kwa sasa ujenzi wa gati Na. 2 litakaloiwezesha bandari hiyo kupokea mizigo hadi zaidi ya tani milioni moja kwa mwaka unaendelea. Anasema magati mengine katika bandari hiyo yatajengwa kati ya sasa na mwaka 2025 kwa jinsi walivyojipanga.
Kingine kinachofanyika Mtwara anasema ni ujenzi wa eneo kubwa zaidi la kuhudumia makontena na kwamba wanatarajia kusakafia eneo lote la Bandari ya Mtwara na kuliwekea uzio katika kuboresha usalama wake.
Mwandishi wetu hivi karibuni alizuru Bandari ya Mtwara na kujionea ujenzi wa gati hilo la kisasa ukiendelea na kuzidi kubadilisha mandhari ya bandari hiyo.
Hatua hiyo inazidi kuufungua zaidi kiuchumi Mkoa wa Mtwara na kuunganisha kibiashara na nchi jirani za kusini, zikiwemo Malawi, Msumbiji, Zambia na Namibia. Nchi hizi zote ni wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Kutokana na kuboreka kwa barabara na uwepo wa Ziwa Nyasa, sasa hivi ni rahisi pia kwa wafanyabiashara wa Zambia na Malawi kutumia Bandari ya Mtwara ambako ni karibu kulinganisha na Bandari ya Dar es Salaam.
Mzigo unaweza kusafiri sasa kwa barabara kutoka Mtwara hadi Songea na kama mzigo ni wa Malawi au eneo la Msumbiji linalopakana na Ziwa Nyasa unaweza kusafiri kwa njia ya meli.
TPA pia imejenga meli mbili za mizigo katika Ziwa Nyasa zinazosubiri wafanyabiashara wa Tanzania na nchi za SADC kuzitumia. Lakini pia mzigo unaweza kusafiri kwa njia ya barabara kutokea Mtwara kupitia Songea na Njombe hadi Tunduma.
Gati Na. 2 linalojengwa Mtwara na serikali kwa gharama ya Sh bilioni 137.4 linatazamiwa kukamilika ndani ya mwaka huu.
Meneja wa Bandari ya Mtwara, Juma Kijavara, anasema sifa muhimu ya gati hilo ni kwamba, limejengwa mahali ambapo kuna kina kirefu cha maji cha asili kinachofikia mita 13 wakati maji yanapokupwa, jambo linalowezesha meli zenye uzito mkubwa kutia nanga wakati wowote.
Kijavara anabainisha kuwa moja ya shehena kubwa ya mizigo inayohudumiwa na bandari hii ni zao la korosho. Anaitaja bidhaa nyingine inayofuatia kuwa ni saruji inayozalishwa na Kiwanda cha Dangote pamoja na mafuta yanayoingizwa kupitia bandari hiyo kwa ajili ya Mkoa wa Lindi na Mtwara.
“Gati hili litakuwa na urefu wa mita 300 na likikamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia meli zenye ukubwa wa tani 65,000 ikilinganishwa na gati la sasa lenye uwezo wa kuhudumia meli zenye uwezo wa tani 45,000. Pia litakuwa na eneo la kuhifadhia mizigo lenye ukubwa wa mita za mraba 79,000 na uwezo wa kuhudumia tani zaidi ya milioni moja kwa mwaka,” anasema Kijavara.
Meneja huyo anasema wakati ujenzi ukiendelea, bado uwezo wa Bandari ya Mtwara kwa sasa katika kuwahudumia wateja wa Tanzania na nje ya nchi unakidhi viwango vinavyotakiwa kutokana na kuwa na vifaa vya kisasa na vya kutosha.
Shughuli za msingi za kila siku za Idara ya Utekelezaji bandarini hapo ni kupakua na kupakia meli katika gati, kuhifadhi mizigo kwa muda pamoja na kukabidhi mizigo inayohifadhiwa kwa wateja.
“Tuna vifaa vingi vya kutosha kuweza kuwahudumia wateja wetu saa 24. Tuna ‘winchi’ kubwa inayotembea yenye uwezo wa kunyanyua tani 100 za mzigo na nyingine mbili zenye uwezo wa kunyanyua tani 50 na tani 25 kila moja.
“Pia, tuna trekta (TT) nane za kubeba mizigo na makontena, ‘forklift’ zenye uwezo wa kubeba tani tatu hadi tano zipo nane na zenye uwezo wa kubeba tani 12 hadi 42 zipo tatu pamoja na mzani wa kupimia mizigo,” anasema meneja.
Kutokana na uwezo huu, anasema Bandari ya Mtwara imeweza kusafirisha tani 229,397 za korosho kwenda kwenye masoko ya nje ya nchi ikiwemo India na Vietnam katika msimu wa 2017/2018 pamoja na saruji kwenda Zanzibar, visiwa vya Comoro na nchini Msumbiji.
“Hayo yote ni mafanikio ya uwezo wa Bandari ya Mtwara ambayo ni muhimu kwa uchumi na maendeleo ya watu wa mikoa ya Kusini ya Lindi, Mtwara na Ruvuma; pamoja na nchi jirani za Kusini zinazotumia bandari hii kusafirishia mizigo yao,” anasema.
Anaongeza kuwa kwa utaratibu waliojiwekea, Bandari ya Mtwara inatakiwa kuhudumia makontena 250 kwa saa 24, lakini kutokana na umuhimu wa kuhudumia mizigo kwa haraka, bandari inahudumia makontena 315 kwa saa 24.
Kwa kuwa bandari hiyo siyo kisiwa, wanafanya kazi kwa kushirikiana na wadau wengine wa bandari wakiwemo mawakala wa meli, mawakala wa ushuru na forodha.
Kutokana na kushirikiana vema na vyombo vya ulinzi na usalama, Bandari ya Mtwara inawahakikishia wateja kwamba kupitia bandari hiyo wanahudumiwa kwa wakati, kwa usalama na bila usumbufu.
Anasema matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) inasaidia sana katika kuboresha shughuli zao za kila siku.
Mifumo ya Tehama bandarini imeimarishwa kusaidia shughuli za kila siku za uendeshaji wa bandari. Shughuli hizo ni pamoja na kuingiza meli bandarini, upakuaji na upakiaji wa mizigo, pamoja na malipo mbalimbali yanayofanywa na wateja au mawakala wa meli.
Anasema bandari iko salama, kwa kuwa bandari ni sehemu nyeti inayopaswa kuhakikisha mzigo wa mteja unakuwa salama muda wote.
“Dhana ya kudhibiti ulinzi inabeba mambo mengi, lakini makubwa ni matatu, ambayo ni pamoja na kuhakikisha wafanyakazi wako salama, mali za wateja ziko salama, na hata miundombinu ya bandari ikiwemo njia ya kuingilia meli, majengo na vifaa viko salama,” anasema.
Ili haya yote yaweze kutekelezeka, anasema wamewekeza katika rasilimali watu kwa maana kwamba Idara ya Ulinzi ina askari wa kutosha na vifaa zikiwemo kamera 38 za CCTV.
Kamera hizi zina uwezo wa kuangalia usalama wa bandari yote saa 24 kwa kumulika kila kinachofanyika bandarini hapo, kumwona kila anayeingia na kutoka bandarini na zaidi sana bandari nzima imezungushiwa uzio.