Katika kinachoonekana kuwa nia ya kuisuka upya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Serikali chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Injinia Deusdedith Kakoko, imefumua muundo wote wa uongozi kwa kufukuza Wakurugenzi sita, wafanyakazi 42 na kuwashusha vyeo mameneja kadhaa.

Habari za uhakika lilizozipata Gazeti la JAMHURI, zinaonesha kuwa uamuzi huo umechochewa na mambo mengi, kati yake ikiwamo upotevu wa makotena, wizi wa hadi Sh milioni 400 kwa mfanyakazi mmoja, kupalilia kuwapo kwa wafanyakazi hewa na ununuzi usiofuata sheria.

Fumuafumua hiyo imewagusa na kuwaondoa kazini aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala, Peter Gawile; Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA, Phares Magessa; Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA aliyemfuata Magessa, Kiliani Chale; Meneja Rasilimali Watu, Jones Macha; Meneja wa Utafiti na Mawasiliano, Suleiman Hassan; na Meneja Uhasibu, Ibin Masoud.

Hawa wameondolewa kazini kwa sababu mbalimbali ikiwamo tuhuma za ufujaji wa fedha, kuingiza wafanyakazi hewa na makosa mengine ya kiutendaji yaliyofanyika chini ya uongozi wa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Madeni Kipande. 

Kipande aliondolewa kazini baada ya Tume iliyoundwa na Samuel Sitta akiwa Waziri wa Ujenzi, kuthibitisha kuwa hakuwa na uhusiano nzuri na wafanyakazi wenzake.

Takwimu zinaonesha kuwa katika fagio hili, wafanyakazi 42 wamefukuzwa kazi, huku wengine zaidi ya 50 wakishushwa vyeo kwa ngazi moja moja. Kati ya walioshushwa vyeo ni pamoja na aliyekuwa Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Hebel Muhanga, anayetarajiwa kuripoti kazini leo baada ya kusimamishwa kazi kwa muda.

“Menejimenti imeamua kuvunja mtandao uliokuwa unashusha ufanisi hapa Bandari. Tumeamua kuwaondoa watu waliokutwa na hatia baada ya uchunguzi uliofanywa na Bandari. Wahusika wamehojiwa, waliokutwa na hatia tumewaondoa kazini,” amesema mtoa habari.

JAMHURI imewasiliana na Meneja Mawasiliano wa TPA, Janet Ruzangi, kupata orodha ya wafanyakazi walioondolewa kazini, ambapo amethibitisha kuwapo kwa tukio la kufukuza wafanyakazi, ila akasema: “Kwa sasa sipo ofisini ila nikiipata orodha hiyo nitakupatieni.”

Kwa upande wake, Injinia Kakoko ameiambia JAMHURI kuwa “Ni kweli idadi hiyo ya wakurugenzi na wafanyakazi wamefukuzwa kazi kwa nia ya kuongeza ufanisi. Ukituhumiwa tukathibitisha tuhuma, tunakuondoa kazini. Nia yetu ni kuhakikisha tunakuwa na Bandari inayohudumia wananchi kwa ufanisi wa hali ya juu na kukuza biashara,” amesema.

Wakati Injinia Kakoko akifanya uamuzi huo mzito, wafanyakazi wameanza kumlalamikia kuwa amechukua mkondo wa mtangulizi wake, Madeni Kipande, aliyekuwa anaajiri watumishi bila kutangaza nafasi zao. “Mkurugenzi Kakoko hakutenda haki. Nafasi ya Mkurugenzi Mkuu pekee ndiyo isiyopaswa kutotangazwa kwani anateuliwa na Rais.

“Nafasi za kurugenzi nyingine zote katika TPA inabidi zitangazwe na kushindaniwa na Watanzania wote kwa uwazi, ila ajabu ameingiza kazini Wakurugenzi watatu; wa HR Editruda Maseko, aliyemtoa Arusha, Mkurugenzi wa Fedha, Nuru Mhando aliyemtoa Ujenzi na Director of Engineering, Injinia Ogale, aliyemtoa katika mabasi ya Mwendokasi… hii si haki. Imetukatisha tamaa wafanyakazi, tunataka haki itendeke,” mmoja wa wafanyakazi ameiambia JAMHURI.

Pia Kaimu Mkurugenzi wa Sheria, aliyefahamika kwa Jina la Mwamunyange, amehamishiwa Bandari bila kushindanishwa kutoka ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Akijibu tuhuma hizo, Injinia Kakoko amesema: “Yeyote anayesema maneno hayo ni kutofahamu utendaji wa Serikali. Kilichofanyika; hawa wakurugenzi wamepata uhamisho wa ndani ya Serikali si ajira mpya. Mfanyakazi wa Serikali anaruhusiwa kuhama kutoka kituo kimoja kwenda kingine ndani ya Serikali pamoja na taasisi zake kwa Check No ile ile, si ajira mpya hizi. Tena hata Mkurugenzi wa Ununuzi namleta, Philipo, ambaye ni Meneja Ununuzi wa Tanroads Shinyanga… tunatafuta ufanisi si upendeleo au michapo. Hapa kazi tu.”

Mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bandari ameiambia JAMHURI kuwa Bodi ilimruhusu Injinia Kakoko kutafuta wafanyakazi wazuri wa kuiwezesha Bandari “kusonga mbele kwa kazi na kukata mtandao wa wizi,” hivyo kama amewapata hao wakurugenzi basi anaamini ametekeleza kwa usahihi maagizo ya Bodi.

“Nafasi nyingi ziko wazi, Kakoko hawezi kufanya kazi peke yake. Tulimwambia ajaribu kushop around kuazima watu na wakaja. Hizi si ajira mpya. Tulisema watu wahamishwe kutoka idara nyingine za Serikali kuja pale bandarini kusaidia. Sisi tunamwamini DG, na hao tunajua aliwaombea uhamisho. Tuliliona hilo [kuwa kuajiri wakurugenzi bila kutangaza kungeleta mgogoro] kama Bodi na tukamshauri, afuate taratibu za uhamisho badala ya kuajiri watumishi wapya,” anasema mjumbe huyo.

Mjumbe huyo wa Bodi ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inaangalia ufanisi wa kazi bila kujali unatokea chama tawala au vinginevyo, na waliamini kuwa utaratibu wa kuhamisha wafanyakazi wazoefu walioajiriwa tayari serikalini ungesaidia kuwahisha ufanisi katika Bandari na kukata mtandao wa wizi.

JAMHURI ilipowasiliana na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Bandari, Dk. Francis Michael, hakukanusha wala kuthibitisha yote yaliyozungumzwa, badala yake akamtaka mwandishi awasiliane na Mwenyekiti wa Bodi, Prof. Ignas Rubaratuka.

JAMHURI ilipowasiliana na Prof. Rubaratuka, alisema: “Bandari ni yetu sote. Mafanikio ya Bandari ni ya Watanzania wote. Ikiwa kuna jambo lolote linalohusu Bandari, sisi tuko wazi. Tukiwa na taarifa za kutoa, tutazitoa bila kusita. Hata hizo za mizigo, ajira za wakurugenzi na kufukuzwa kwa wafanyakazi, nitafuatilia na kuhakikisha tunakupa majibu kwa kuwa umeuliza.” Hadi tunakwenda mitamboni ilikuwa hajatoa majibu.

JAMHURI imefanya juhudi za kuwapata wakurugenzi ‘waliotumbuliwa’ bila mafanikio baada ya kufika hadi nyumbani kwao ikaambiwa hawapo, bila kutaja njia nyingine zilizotumika kuwatafuta akina Magessa na Gawile. Hata hivyo, wakati tunakwenda mitamboni, Gawile alituma ujumbe ufuatao:

“Namshukuru Mungu kwa yote! Nimelitumikia Taifa langu kwa uaminifu mkubwa na weledi, ila yote ni mipango ya Mungu! Sikusudii kuchukua hatua yoyote. Namwachia Mungu!”

Magessa alikuwa akichukuliwa kama mbuyu pale Bandari, kutokana na kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM), cheo kilichotajwa kuwa alikitumia kutikisha wakurugenzi wengi waliokuwa Bandari, ila sasa inaonekana Kakoko na Bodi mpya ya Wakurugenzi wamemdhibiti.

Imetajwa kuwa baadhi ya wafanyakazi wametimuliwa kutokana na kuhusika kwao katika kashfa ya kupotea kwa makontena kutoka bandarini, na uongozi umedhamiria kuendelea kutumbua kila mfanyakazi unayeona ana malengo kinyume na kuhakikisha Bandari inapata biashara na kuiingizia Serikali mapato.

 

Kupungua kwa mizigo

Wafanyakazi wa Bandari waliozungumza na JAMHURI wamesema mizigo imepungua kwa kiwango cha kutisha bandarini, kutokana na tozo mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa huduma zinazotolewa kwa mizigo ya kimataifa (transit goods), hali wanayohofia itaikosesha Bandari mapato. 

“Mfano ni mizigo ya DRC. Hawa kwa mwaka wanapitisha mzigo wa wastani wa tani milioni 3, lakini wamesema bayana kuwa kwa mabadiliko ya VAT tunayowatoza na himaya ya ushuru wa pamoja tuliyoanzisha na DRC, hawataitumia tena Bandari ya Dar es Salaam,” anasema mmoja wa wafanyakazi.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa mwaka 2014 Serikali ya Tanzania iliingia mkataba wa Himaya Moja ya Ushuru na DRC baada ya nchi za Kenya, Uganda na Rwanda kuanzisha kilichoitwa ‘the Coalition of the Willing’. Mkataba huu unaitaka Tanzania kukusanya ushuru kwa niaba ya DRC mizigo inapofika Bandari ya Dar es Salaam na kuwasilisha ushuru uliokusanywa kwa DRC.

“Sisi wafanyabiashara wa kutoka Congo hatuwezi kulipa kodi tunayojua kuwa viongozi wetu wanaihamishia Ubelgiji. Kwa nini tulipe fedha tunazojua ni kwa ajili ya watu na si kwa maendeleo ya nchi yetu? Kama Tanzania mtaendelea na kodi hii, sisi kamwe hatutatumia Bandari yenu na tutatumia za Beira na nyingine tusikotozwa ushuru huu usio na manufaa. Tunazo bandari nane za kupitisha mizigo yetu, si lazima Dar es Salaam kama mnataka kumpa hela [Rais Joseph] Kabila,” anasema mmoja wa wafanyabiashara kutoka DRC.

DRC inatajwa kuwa taifa lililokuwa na mzigo mwingi unaopita kwenye Bandari ya Dar es Salaam, ambapo kwa mwaka inapitisha nchini wastani wa tani milioni 3 za mizigo. Wafanyabiashara walimlalamikia Afisa wa Mapato kutoka DRC aliyewekwa Bandari ya Dar es Salaam, Peter Morisho, aliyefikia hatua ya kukadirisa kontena moja hadi dola 3,000 huku akidaiwa kulazimisha rushwa. Morisho ameondolewa baada ya ziara ya Rais Joseph Kabila.

Mmoja wa wakurugenzi alipoelezwa kuwa mizigo imepungua kwa sababu ya VAT iliyoongezwa kwenye huduma za mizigo ya transit na Tanzania kukusanya ushuru kwa niaba ya DRC, ambapo wafanyabiashara wa DRC hawana utamaduni wa kulipa kodi, amesema:

“Decision (uamuzi) zikishafanywa huko juu, huku chini unafanyaje? Kuna vitu vipo juu yetu. Haya, ni kweli lakini [Rais] Kabila alivyokuja amebadilisha. Tatizo kubwa watu walikuwa wanaondoa mizigo hapa inaishia njiani. Inaweza kupungua si kwamba ilikuwa inakwenda Congo, bali ilikuwa inaishia hapa nchini. Ni wazi mizigo lazima ipungue kwani kuna udhibiti mkali. Kuna watu walikuwa wanatoa mizigo wanadai ni ya transit halafu haipelekwi Congo inaishia hapa nchini. Kwa mfumo tulioweka hawawezi kuileta tena… lazima itapungua tu,” anasema Mkurugenzi huyo.

Hata hivyo, amesema wakati mizigo inapungua mapato yanapanda na akamnukuu Rais John Mafuguli aliyesema: “Afadhali ije meli moja, ilipe mapato kwa usahihi na nchi ipate mapato halisi kuliko kuleta meli zisizo na idadi wakati mapato hayaonekani.”

 

Kipande kunyang’anywa gari

Aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande, uamuzi umepitishwa kuwa anyang’anywe gari aina ya Range Rover alilojikopesha wakati akiwa anakaimu wadhifa huo. 

“Ameshindwa kulipa deni lake analodaiwa… Bandari sisi bado tunayo kadi ya gari hilo, sasa tumeona bora tumtake arejeshe gari maana amevunja masharti ya mkataba kwa kutolipa deni lake. 

“Kila tukimpelekea barua nyumbani kwake anagoma kuzipokea. Barua karibu zote zinaachwa kwa Afisa Mtendaji. Sasa huyu tumeona hakuna njia nyingine, ila kumtaka aturejeshee gari alilojikopesha na hatua za kumnyang’anya gari hilo zimekamilika,” alisema mtoa habari wetu.

Habari kutoka Bandari zinaonesha viwango viwili tofauti anavyodaiwa Kipade. Wakati mtoa habari wa kwanza akisema anadaiwa Sh milioni 120, mtoa habari wa pili amesema anadaiwa Sh milioni 50. Viongozi wote waliozungumza na JAMHURI hawakuwa tayari kuzungumzia deni hili.

JAMHURI ilipozungumza na Kipande, amesema: “Sina taarifa kama gari langu limeagizwa kukamatwa, lakini kuhusiana na hilo deni aulizwe Meneja.” Alipoulizwa iwapo ni kweli hilo deni lipo au la, akasema: “Andika mnavyotaka kuandika.”

Bandari ya Dar es Salaam imekuwa katika misukosuko kutokana na tuhuma za baadhi ya watumishi kupoteza makontena zaidi ya 12,000, mita za mafuta kuharibiwa kwa makusudi, baadhi ya mameneja kuingiza kazini watumishi hewa na tuhuma nyingi zilizopunguza ufanisi wa Bandari. Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ilipoingia madarakani, imeamua kusafisha uozo bandarini kwa kufumua unaoitwa ‘mtandao wa wizi’, hali iliyoleta kihoro kikubwa.

Hadi sasa Bandari Kavu (ICDs) nyingi zimefungwa nchini na wafanyabiashara wengi waliokuwa wanafanya biashara ya ujanjaujanja wamefunga maduka yao kwani taratibu za kuingiza na kutoa mzigo bandarini kwa sasa zinafuatwa kwa usahihi.