Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na minong’ono kuhusu kupungua kwa shehena ya mizigo katika bandari ya Dar es Salaam, hali hiyo imeendelea hata baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuitembelea bandari mwishoni mwa wiki iliyopita.
Tunaamini kwamba njia pekee ya kuondoa minong’ono hiyo ni kuwa na kikao cha pamoja kitakachohusisha wadau wote, kuanzia kwa mawakala wa kupokea na kusafirisha mizigo, wafanyabiashara wanaotumia bandari yetu, pamoja na wale wateja wetu tuliowapoteza kutokana na sababu mbalimbali.
Tunaelewa kwamba Mheshimiwa Rais John Magufuli, alipiga marufuku mikutano, semina, warsha na makongamano, lakini mkutano huu uwe muhsusi katika kuhakikisha wadau wanasikilizwa na kupatiwa majibu ya wazi kuhusu hali inayoendelea na hatimaye kurekebisha.
Kitendo cha shehena ya mizigo kushuka kwa wastani wa asilimia 9-30 sio jambo zuri kwa mustakabali wa uchumi wa nchi yetu, japokuwa ni kweli kwamba takwimu zinaonesha kwamba mizigo imepungua na mapatao yameongezeka, ni wakati sasa wa kuhakikisha kwamba mizigo inaongezeka na hivyo kuongeza mapato ya nchi.
Bandari ya Dar es Salaam, imekaa kimkakati kabisa katika kuzihudumia nchi zaidi ya sita ambazo hazina bandari, nchi hizo ni Zambia, Malawi, Burundi, Rwanda, Uganda pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Tunafahamu kwamba Serikali imewapatia bandari lengo la kukusanya Shilingi trilioni 1 katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2016/2017 kutoka kwenye makusanyo ya shilingi bilioni 660 ambayo yamekuwa yanakusanywa na bandari, lengo hilo linahitaji kuwepo kwa jitihada za pamoja kwa kuwahusisha wadau.
Ni wazi kwamba Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Mhandisi Deusdedit Kakoko, amekuwa akijitahidi kuondoa makandokando yaliyowafanya baadhi ya wafanyabiashara wakubwa kuacha kuitumia bandari hiyo, tuna imani kwamba jitihada hizo sasa zinatakiwa kuhamishiwa katika kuhakikisha kwamba wanarudi na kuendelea kuitumia bandari yetu.
Ni ukweli uliowazi kwamba kutokana na changamoto zilizokuwa katika bandari ya Dar es Salaam, baadhi ya wafanyabiashara kutoka Kongo DRC, waliamua kutumia bandari ya Durban, Afrika Kusini, ambako ni mbali zaidi kwa kilomita 4000, ikilinganishwa na Dar es Salaam, tunaamini fursa ya kufanya biashara na Kongo DRC, Zambia, Uganda, Rwanda na Burundi iko ndani ya uwezo wa mamlaka zinazohusika.