*Mkurugenzi Mkuu Kipande aingiza ukabila, udini, majungu
*Wafanyakazi watatu bandarini wafariki kutokana na vitisho
*CCTV hazifanyi kazi tangu 2011, wachonga dola mil. 6.5
*Mnikulu Gurumo, Mtawa wampa kiburi, wachafua jina la JK
*Amdanganya Dk. Mwakyembe, amtukana Balozi wa Japan
Kuna kila dalili kuwa Bandari ya Dar es Salaam inakufa kutokana na uongozi mbovu uliojiingiza katika majungu, udini, ukabila na majivuno yasiyo na tija. Wafanyakazi katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) wamepoteza morali wa kufanya kazi kutokana na vitisho na matusi ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Madeni Juma Kipande.
Hadi habari hii ya kiuchunguzi inachapishwa wafanayakazi watatu; Peter Gwamaka Kitangalala, Dotto Mbega na mwingine aliyefahamika kwa jina la Lyochi wamefariki dunia katika kipindi cha miezi mitatu kutokana na shinikizo la damu lililozaa kiharusi baada ya vitisho vya Kipande.
Katika hali ya kuwavuruga wafanyakazi wa bandari, Katangalala alihamishiwa Mwanza na baada ya miezi miwili akahamishwa tena kwenda Lindi, huku akipewa vitisho kuwa muda wowote ajiandae kufukuzwa kazi. Kutokana na hofu, alipata kiharusi (stroke) akafa. Mbega kwa upande wake yeye alikuwa makao makuu Dar es Salaam, lakini kutokana na vitisho vya kila siku vya Kipande na wasaidizi wake, naye akapata kiharusi mwezi mmoja uliopita akafariki dunia.
Jumapili ya Machi 30, mfanyakazi mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Lyochi huku wengine wakisema ni Oluwochi mwenye asili ya Wajaruo, aliyehamishiwa bandari ya Kasanga, Sumbawanga naye aliaga dunia kwa ugonjwa huo huo wa kiharusi kutokana na mashinikizo ya Kipande.
“Uhalisia hali inatisha. Kipande anajinadi kuwa atamfukuza kila mtu, na kweli anafukuza anaajiri watu wa dini yake. Kuna kabila la Wahaya kutoka Kanda ya Ziwa, hilo utadhani waliwahi kushikana nalo ugoni. Mhaya yeyote aliyemkuta kazini ameapa kumg’oa. Amehamisha [Hassan M.] Kyomile kwa sababu ya kabila lake na kwamba aliomba kazi ya Ukurugenzi Mkuu,” kilisema chanzo chetu.
Kyomile amehamishwa Machi mwaka huu, kutoka makao makuu alikokuwa Mkurugenzi wa Ununuzi na kwenda kuwa Meneja wa Bandari Tanga.
Aondoa wasomi wote Idara ya Mawasiliano
Katika hali inayoelezwa kuwa Kipande anamkingia kifua mmoja wa wafanyakazi wa Idara ya Mawasiliano asiye na sifa, amewahamisha watendaji wote wenye sifa kitaaluma waliokuwa wakifanya kazi wa idara hiyo na kumbakiza huyo mpambe wake anayedaiwa kumpa umbea kutoka kila kona.
Kwa shinikizo la Kipande, amewahamisha Beatrice Jairo kutoka Ofisi ya Mawasiliano Makao Makuu kwenda Nasio, Ukerewe ambako hakuna hata bandari inayofanya kazi. “Beatrice ana shahada ya uzamili ya mawasiliano ya umma. Tulijiuliza amehamishiwa Nansio [Ukerewe] kwenda kuwa msemaji wa Bandari ya Nansio au ilikuwa kumkomoa tu? Kwanza mshahara wa Beatrice ni mkubwa kuliko makusanyo yote ya Nansio kwa mwezi mzima. Tukasema hapa kuna jambo,” kilisema chanzo chetu.
Mwingine aliyehamishwa kutoka ofisini hiyo ni Levina Kato, mwenye Stashahada ya Juu ya Uandishi wa Habari, ambapo alipelekwa Bandari ya Kasanga, Sumbawanga ambako meli ya MV Liemba hufika mara moja kwa mwezi katika Bandari ya Kasanga.
Uchunguzi wa kina umebaini kuwa Usalama wa Taifa ulishitushwa na uhamisho usio na tija, hivyo ukampa maelekezo Kipande awarejeshe Dar es Salaam kazini Kato na Jairo, kinyume chake Kipande ameagiza mabinti hao wasimamishwe kazi mara moja na kuanzia Februari, mwaka huu amesitisha mishahara yao.
Ugomvi na binti wa Jairo
Uchunguzi wa gazeti JAMHURI umebaini kuwa binti wa Jairo, Beatrice anaumizwa kutokana na uamuzi wa kiutumishi wa umma alioufanya baba yake, David Jairo wakati akiwa Katibu wa Rais Jakaya Kikwete. “Ninavyofahamu, Madeni Kipande alipata kumpigia simu Jairo wakati akiwa Katibu wa Rais, akimuomba amsaidie kupata ukurugenzi. Jairo akamwambia yeye hana uwezo wa kumpatia ukurugenzi bali mapendekezo yanapaswa kuanzia wizarani.
“Baada ya jibu hilo, Kipande alikaa na kijiba moyoni. Siku moja Jairo akiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, transfoma ya Kipawa [Dar es Salaam] ililipuka. Ikabidi wizara ikodishe boti isafirishe transfoma ya akiba kutoka Tanga kuja kufungwa pale Kipawa. Kwa mujibu wa sheria ilibidi Wizara ya Nishati na Madini ipate kibali kutoka Wizara ya Ujenzi kwa ajili ya kusafirisha mzigo mzito kupita barabarani.
“Jairo alimpigia simu Kipande kwa nia ya kuomba kibali hicho, lakini Kipande alipopokea simu tu alianza kumporomoshea matusi Jairo. Akamwambia alipokuwa Ikulu alikuwa analinga sana. Hakupata kujua kuwa angetoka pale Ikulu. Akamwambia sasa ameangukia kwenye mikono yake. Jairo alisisitiza kuwa hakupiga simu kukumbushana ya Ikulu bali kuomba kibali au roller ya kubebea tansfoma hiyo, Kipande akaendeleza matusi.
“Jairo alimweleza yote hayo Katibu Mkuu wa Ujenzi Balozi [Herbert] Mrango, aliyemwambia kuwa Kipande ndivyo alivyo asimshangae. Balozi Mrango alimsaidia Jairo kupata kibali au roller transfoma ikatolewa bandarini na kwenda kufungwa Kipawa. Baada ya hapo Kipande alipita kwa watu akitamba kuwa amemtukana vilivyo Katibu Mkuu Jairo. Yanayoendelea dhidi ya binti ya Jairo, sasa tunaona ni visasi,” kilisema chanzo chetu.
Kauli ya Jairo dhidi ya Kipande
Gazeti JAMHURI lilipowasiliana na Jairo kupata ukweli wa tuhuma hizi, alikiri kuwa yalitokea isipokuwa akasema hataki kuyarejea kwani anaamini kuwa uongozi una miiko, taratibu, kanuni na sheria za kazi, ambazo ikiwa Kipande alikereka alipaswa apambane na yeye Jairo, na si binti yake.
“Ninachoweza kusema, katika uongozi hakuna suala la utashi, bali tunafuata kanuni na taratibu. Suala la uteuzi taratibu zake zinafahamika, sidhani kwa kumweleza utaratibu aliopaswa kuufuata iwapo nilimkosea adabu hadi afanye hayo aliyonifanyia na hayo anayoendelea kumfanyia binti yangu,” alisema Jairo.
Alipoulizwa anamuonaje Kipande kama kiongozi wa TPA, alisema: “Hafai uongozi. Hawezi kuleta tija huyu. Bandari ni sehemu ya mahusiano na ni chanzo kikuu cha mapato. Inaweza kukuza uchumi wa nchi yetu. Bandari ya Dar es Salaam inahudumia nchi nane, ambazo ni landlocked, kwa utendaji aliouonyesha hafai anachochea magendo na kuua bandari.
“Serikali ingemuondoa, na kutafuta mtu mwingine. Watu wameondolewa pale bandarini kwa ajili ya majungu tu, mapato yanashuka anatoa taarifa za uongo kuwa yanapanda… bandari inahitaji iwe na utulivu mkubwa. Wafanyakazi wafanye kwa ari, sasa wanafanya kwa woga, ni hatari,” alisema Jairo.
Mtawa amkingia kifua Kipande
Habari za uhakika ambazo JAMHURI imezipata katika uchunguzi, zinaonesha kuwa Madeni Kipande Idara ya Usalama wa Taifa imeshitushwa na utendaji wake na imeelekeza asithibitishwe kazini kuwa Mkurugenzi Mkuu wa bandari kwa vigezo viwili. Kigezo cha kwanza ana umri wa miaka 58, kwani alizaliwa Oktoba, mwaka 1956, na sababu ya pili Kanuni za Utumishi zinazotokana na Sheria ya Utumishi wa Umma Na 8, zinataka kiongozi anayeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu awe amesalia na muda usiopungua miaka mitatu au zaidi ya utumishi kazini kabla ya kustaafu.
Kanuni hii inalenga kumpa fursa kiongozi anayethibitishwa kushika wadhifa husika aweze kuwa na mpango wa muda mfupi, mpango wa kati na mpango wa muda mrefu utakaosaidia taasisi aliyoteuliwa kuiongoza. Mchakato wa kumpata Mkurugenzi Mkuu unachukua kati ya miezi tisa na 15, hivyo kanuni inalenga kuepusha upotezaji muda kwa kumteua mtu ambaye amebakiza miezi 24 au 30 kustaafu.
Taarifa za ndani zinasema kuwa Kipande amekuwa akitisha watu kuwa yeye ni mwajiriwa wa Usalama wa Taifa na kwamba ni ndugu wa karibu wa Rais Jakaya Kikwete, hivyo anaweza kufanya lolote bila kujali sheria, kanuni au taratibu za nchi zinasemaje.
Uchunguzi umebaini kuwa Rais Kikwete hahusiki na ubabe anaofanya Kipande, bali anapata kinga kutoka kwa Kassim Mtawa, ambaye ni Msaidizi Binafsi wa Rais Kikwete, akishirikiana na Mnikulu Gurumo, ambao wamekuwa wakimhakikishia usalama wake kwa kuwa wanatoka pamoja Bagamoyo. Kipande anatumia udugu wa Mtawa, ambaye ni mjomba wa damu wa Rais Kikwete kujihalalishia matendo ya kibabe anayoyafanya kila sehemu ya kazi aendako. Gurumo na Mtawa wanampa kiburi Kipande bila baraka za Rais Kikwete, uchunguzi umethibitisha.
Kipande agoma kujibu maswali
Februari 18, mwaka huu baada ya kuwa Kipande amemzungusha mwandishi wa habari hizi, aliagiza kupitia Katibu wake Muhtasi kuwa mwandishi aandike maswali. Mwandishi aliandika maswali haya na kuyawasilisha ofisini kwa Kipande Machi 7, 2014, kama ifuatavyo:-
  ;
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Bandari Tanzania
S. L. P. 9184
Dar es Salaam
Ndugu/Eng.,
YAH: MAHOJIANO YA KIHABARI KWA NJIA YA MAANDISHI KUHUSU MAMLAKA YA BANDARI TANZANIA
Pamoja na salaam za gazeti JAMHURI, naomba kuchukua fursa hii kukushukuru kwa jibu lako zuri ulilolitoa kupitia kwa Katibu Muhtasi wako juu ya ombi langu la kufanya mahojiano na wewe kuhusu masuala mbalimbali hapo bandarini. Nikufahamishe tu, kuwa tayari nilikwishahojiana na Ndugu Phares Magesa kuhusiana na Idara yake, na sasa nawasilisha maswali yangu kwako. Nitasafiri nje ya Dar es Salaam kwa muda wa wiki moja kuanzia kesho, hivyo nataraji wakati narejea majibu yatakuwa tayari. Yafuatayo ni maswali tunayoomba majibu yako, na tunatanguliza shukrani kwa ushirikiano wako:-
1. Mamlaka ya Bandari Tanzania tangu mwaka 2011 imekuwa haina mita za kupimia mafuta (flow meters) yanayoingia nchini. Ofisi yako inasema ilizuiwa na Idara ya Vipimo kutumia mita zilizonunuliwa kwa maelezo kuwa zinapunja wateja. Je, huoni kwa kukaa muda wote bila mita hizi nchi inapoteza mapato makubwa? Ni juhudi gani mnafanya kudhibiti hali hii?
2. Kwa muda wa miaka minne sasa, bandari haina Closed Circuit Televisions (CCTV) ambazo ni nguzo ya usalama wa mizigo bandarini. Kuna maelezo kuwa mmeandaa zabuni (procurement) ambayo inaweza kuchukua hadi miezi tisa kuanzia mwezi huu kupata CCTV cameras. Je, huoni kuwa usalama wa bandari uko hatarini kwa kutokuwa na CCTV cameras, hasa wizi wa mizigo ya wateja?
3. Mamlaka ya Bandari (hasa wewe) inatuhumiwa kumpa taarifa za uongo Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe aliyetoa taarifa kwa vyombo vya habari baada ya ninyi kumpa taarifa kuwa bandari sasa inakusanya hadi Sh bilioni 50 kwa mwezi, wakati uhalisia makusanyo makubwa kwa mujibu wa vielelezo vilivyopo yalikusanywa Januari 2014, ambapo yalifikia Sh bilioni 43. Inadaiwa hizi ni njama za kuonesha kuwa uongozi uliopita ni mbaya. Je, unazungumziaje upungufu huu?
4. Zipo taarifa kuwa unaendesha Mamlaka ya Bandari kwa Ubabe na Vitisho (rejea barua yako kwa Rukia Shamte) yenye Kumb. No. DG/3/3/01 ya Juni 21, 2013, iliyodhihirisha ubabe wa aina yake kwa kudai kuwa amekuagiza na ukamshauri asubiri awe Katibu Mkuu au Waziri. Pia rejea ushauri wa Bodi kupitia kwa Prof. Msambichaka akikutaka usiendeshe uongozi wa watu sawa na kuendesha mitambo (mashine). Je, kwa nini unatumia ubabe badala ya kufuata taratibu na sheria za kazi kwa mtumishi anayekwenda kinyume cha sheria ya utumishi wa umma?
5. Inadaiwa kuwa umewavuruga na kuwagawa wafanyakazi katika makundi bandarini, ikiwamo wafanyakazi uliowahamisha na kuwapeleka katika vituo visivyoendana na kazi walizoajiriwa kufanya. Baadhi ya mameneja umewaondolea mamlaka ya kufanya kazi na inatajwa kuwa unawapa vitisho. Hii yote inaelezwa kuwa unajenga himaya yako na inaelezwa kuwa wengi wanahamishwa kwa hisia kwamba hawamuungi mkono mgombea wako wa urais ifikapo mwaka 2015. Naomba ufafanuzi.
6. Bodi ya wakurugenzi iliyovunjwa, ilitoa maelekezo mengi ikiwamo utekelezaji wa maazimio ya Kamati ya Mbakileki, ambayo mengi hayajatekelezwa kwa asilimia 90 hadi sasa. Inaelezwa kuwa ulikuwa ukiwapuuza (rejea kauli yako kwa waziri Mwakyembe mkiwa Dodoma Agosti, 2013 kuwa hawakubabaishi). Je, unapokataa kutekeleza maagizo ya Bodi unataka kutekeleza ya nani?
7. Mwisho, naomba ikiwa unalo lolote unalodhani unataka kulizungumza kwa maslahi ya taifa kuhusiana na utendaji wa bandari ulizungumze kupitia mahojiano haya.
Natanguliza shukrani za dhati kwa ushirikiano wako,
Wako,
Deodatus Balile
Managing Editor/Director,
Jamhuri Media Limited
Baada ya barua hii Kipande alikaa kimya. Aprili 1, 2014 mwandishi wa habari hizi alimpigia simu kuulizia iwapo maswali yake yalifika au yalipotelea njiani kwani hayajajibiwa. Kwa dharau ya aina yake, alisema:
“Hivi wawe Balile una uzalendo kweli? Maswali yenyewe ya kitoto, ulitaka nijibu nini?” Baada ya kauli hiyo, mwandishi wa habari hizi aliamua kumpasulia ukweli, hadi Kipande akanyamaza kimya. Alimweleza wizi anaoufanya kwa kutumia mifumo mpya ya mawasiliano bandarini (ICT), alimweleza CCTV cameras zilivyoachwa makusudi kwa nia ya kufanikisha wizi na kwamba Mkurugenzi wake wa IT alikwishakiri kuwa hazifanyi kazi tangu mwaka 2011.
Kisha mwandishi wa habari hizi, alimuonya Kipande kujiepusha na tabia ya kufokea au kudharau watu asiowafahamu, hasa ikitiliwa maanani kuwa tabia hii ilikuwa imeushawishi uongozi wa juu kumuondoa bandarini Desemba 31, mwaka jana, lakini Mtawa na Gurumo wakafukia mashimo. Baada ya majibizano, Kipande alikaa kimya sawa na mtu aliyenyeshewa mvua kwani inawezekana hakuyatarajia majibu aliyopewa kisha akasema:
“Samahani kaka, hayo tuyaache sasa tumeishia wapi?” Mwandishi akamwambia kinachotakiwa ni miadi kwa nia ya kumuonesha vielelezo vilivyopo aweze kuvitolea ufafanuzi likiwamo hili la kumdanganya Dk. Mwakyembe kuwa bandari inakusanya Sh bilioni 50 wakati haijapata kufikia kiwango hiki. Baada ya kibano hicho, Kipande akasema.
“Kaka sasa naomba tukutane Ijumaa (Aprili 4) saa 8 ofisini kwangu na Magesa atakuwapo,” Mwandishi alimshukuru na kukata simu. Ilipofika saa 10:13 jioni, Meneja Mawasiliano wa TPA, Janet Ruzangi, alimpigia simu Mwandishi wa hizi habari na kwa mshangao akasema:
“Hallo, ni kaka Balile?” Mwandishi akaitikia ndio. “Mkurugenzi Mkuu ameniambia nikupigie simu.” Mwandishi akasema sawa nimepokea niambia kakupa ujumbe gani. Janeth akasema: “Hakunipa ujumbe wowote ila ameniambia nikupigie simu tu.” Mwandishi akamuuliza kama hana ujumbe anapiga kwa ajili gani, ndipo akamwambia kilichotokea na jinsi Mwandishi alivyomweleza ukweli bila kificho Mkurugenzi huyo.
Inawezekana katika hali ya kuchanganyikiwa, Kipande alimwambia Janeth apige simu bila kujua ujumbe upi aufikishe kwa mwandishi na hali hiyo ilijitokeza tena siku ya Ijumaa. Mwandishi alipofika lango kuu, alijitambulisha na mlinzi akapiga simu kwa Katibu Muhtasi wa Kipande alisema aende ofisini kwa Kipande kuna maelekezo yake.
Mwandishi alipofika kwenye lango la pili, walinzi walipopiga simu mara Katibu Muhtasi akasema mwandishi akazungumze na Janeth, mara akasema Mwandishi aondoke kwani Kipande aliitwa Wizarani na Naibu Katibu Mkuu, na baada ya mkanganyiko huo mwandishi aliondoka.
Mwandishi alimtumia ujumbe mfupi Kipande akimweleza jinsi alivyotekeleza wajibu wake kisheria wa kumpa fursa ya kufafanua tuhuma dhidi yake, kwa miadi na maswali yaliyowasilishwa kwake ofisini, kisha Kipande akajibu ujumbe huo kwa sms hivi:-
“Nimeitwa Wizarani tangu saa tatu, niliacha maelekezo kumuona meneja wa communications, hawakukwambia?” Mwandishi alipomjibu kuwa hawakufanya hivyo, akajibu ujumbe wa mwisho, hivi: “Pole brother.”
Kumdanganya Dk. Mwakyembe
Kwa nyakati tofauti, Kipande kwa nia ya kujionesha kuwa anafanya kazi kwa ufanisi mkubwa, amekuwa akimpa taarifa za uongo Waziri wake, Dk. Mwakyembe, kuonesha kuwa bandari sasa inakusanya Sh bilioni 50 na kwamba kuna unfanisi mkubwa kuliko wakati wowote.
Tangu mwaka 2011 camera za CCTV zimekuwa hazifanyi kazi bandarini hapo, ambapo walinzi wanazungukia mizigo ya wateja kwa virugungu bila msaada wa teknolojia ingawa camera hizo zipo zilifungwa mwaka 2007 na inaelezwa kuwa zimeharibiwa kwa makusudi kutoa fursa kwa baadhi ya wafanyakazi kudokoa mizigo ya wateja.
Kipande amtukana Balozi wa Japan
Katika hali ya kushangaza, wiki iliyopita Madeni Kipande amemtukana Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada. Balozi Okada alikwenda ofisni kwa Kipande wiki iliyopita kumweleza nia ya Japan kutoa msaada wa kukarabati gati Na 1-7 kama msaada, lakini kinyume na matarajio kuwa Kipande angepokea msaada huo, aliishia kumrushia matusi Balozi wa Japan.
“Kwanza alikuwa amekataa kumuona huyo Balozi, akisema aonane na wasaidizi wake, lakini Balozi aliposisitiza msaidizi wa Kipande akamwambia protokali zinamtaka amuone, akakubali kumuona. Kilichotokea baada ya hapo kilikuwa kituko. Balozi alimweleza kuwa anataka nchi yake isaidie kukarabati gati Na 1-7 la bandari, Kipande akamwambia bandari ilitangaza zabuni, na Japan kama ilikuwa inataka kufanya hivyo ilipaswa kuomba zabuni na kuingia kwenye ushindani.
“Balozi alisisitiza kuwa nia yake ni kutoa msaada si kufanya biashara, Kipande akasema huo ni uongo kwani amezoea kauli za aina hiyo na ni ujanja wa kupenyeza rushwa na kuzipatia kazi kampuni za Kijapan kwa njia za panya, hivyo yeye hatakubali kama Japan inataka kutoa msaada wa ukarabati wa bandari basi isubiri zabuni ijayo.
“Kauli kwamba Japan inataka kutumia mkondo wa ubalozi kwa njia ya rushwa kuzipatia kampuni za nchini kwake kazi wakati nchi hiyo ililenga kutoa msaada ilimuuma mno Balozi na taarifa zilizopo anataka au tayari ameandika barua Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kutaka ufafanuzi kwa nini nchi yake ya Japan ihusishwe na rushwa kwa kutaka kuisaidia Tanzania,” kilisema chanzo chetu. Juhudi za JAMHURI kuwasiliana na Ubalozi zinaendelea.
Je, unajua mbinu wanazotumia kufuja fedha za bandari. Unajua Phares Magesa alijibu nini alipohojiwa na JAMHURI juu ya CCTV kutofanya kazi bandarini tangu mwaka 2011? Unazo taarifa kuwa Kipande amezuia wafanyakazi kupanda rift ya ofisi anapokuwa anaipanda yeye? Unajua kuwa bandari imetelekeza mpango wa Big Results Now? Je, unajua kuwa shahada ya uzamili (Masters) ya Kipande aliyoipata nchini Afrika Kusini inatiliwa shaka? Unafahamu mradi wa electronic single window system walivyoutengea dola milioni 6.5 kiujanjaujanja? Usikose toleo lijalo la JAMHURI upate majibu ya maswali haya na mengine mengi jinsi bandari za Tanzania zinavyotafunwa hadi mizigo ya Tanzania ipatayo tani 160,000 kwa sasa inapitishwa Mombasa Kenya.