Bandari ya Dar es Salaam

Bandari ya Dar es Salaam

Uongozi mpya wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) unahitaji kufanya kazi ya ziada kudhibiti mapato kwani maafisa wengi walioajiriwa katika Bandari mbalimbali nchini wana mbinu chafu za kutisha zinazoikosesha nchi mapato.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa kwa makusudi baadhi ya maafisa wasio waadilifu wanapoteza kumbukumbu za hesabu za meli kwenye vitabu vya mamlaka na hii imethibitishwa na ukaguzi wa ndani na wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).

“Ilibainika kati ya meli 1,253 zilizotia nanga katika Bandari, meli 145 hazikuonekana kwenye mfumo wa mapato. Kati ya meli hizi ambazo hazikuonekana kwenye mfumo, uongozi umeweza kutoa maelezo na viambatisho vya meli 60 tu, na meli 85 hazikuwemo kwenye mfumo wa mapato,” inasema sehemu ya ripoti ya CAG ya mwaka 2014/2015.

Pia imebainika kuwa kuna tofauti ya kumbukumbu kati ya bidhaa zinazoingizwa kwenye mfumo wa Mamlaka ya Bandari na zile za kwenye Mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mmoja wa maafisa waandamizi wa Bandari ameliambia JAMHURI kuwa Mkurugenzi Mkuu anapaswa kuanza na taarifa muhimu za uchunguzi zilizopo ofisini kwake ambazo zinaonyesha mianya ya wizi na ikimpendeza awasiliane na CAG atakayemweleza matundu yalipo.

“Kimsingi namhurumia sana Injinia Kakoko. Najua ni mgeni, ni mwadilifu na anapenda kusimamia sheria, hasa nikirejea pale Arusha alivyosimamia ubomoaji wa hoteli ambayo Rais [Jakaya] Kikwete aliizindua yeye akasema imejengwa barabarani na muda mfupi baadaye akaibomoa, ila inampasa kusoma ripoti na kusikiliza ushauri wa watu wanaojua matatizo ya Bandari.

“Ombi langu kwake, aje na mguu wa kujenga umoja, ushirikiano na uhusiano mzuri. Viongozi waliomtangulia wameacha nyufa Bandari. [Madeni] Kipande aligeuka Mungu mtu, akawa anatukana wateja, wafanyakazi akawageuza kama vinyang’arika kwa kiwango kikubwa hadi kufikia ubaguzi kuwa ungepanda naye kwenye lift (elevator) anakuandikia barua ya onyo au kukufukuza kazi kwa maelezo kuwa DG anapaswa kupanda peke yake kwenye lift. Hii ilikuwa ni shida,” anasema mmoja wa wafanyakazi.

Afisa Mwingine Mwandamizi ameliambia JAMHURI kuwa Injinia Kakoko anapaswa kuwa makini na masalia ya Kipande, ambayo yalikuwa yanajiandaa kuchukua mikoba, huku akisema wengine wapo kwenye idara kama ya sheria ambao muda wote wamekuwa wapika majungu wakubwa na wamechangia kwa kiasi kikubwa kung’oa viongozi akina Awadh Masawe walioanza kurejesha umoja bandarini.

 “Kama akiingia na mguu wa kutafuta watu badala ya kufanya kazi, basi tutabaki pale pale. Wapo baadhi ya viongozi walioletwa kwa sasa wanaripoti moja kwa moja kwa Waziri na wanampelekea majungu haijapata kutokea. Hawa sasa wanapaswa kutambua kuwa wanaripoti kwa Kakoko na waache kutishia wafanyakazi. Bandari si kambi ya mateso ni sehemu ya kuzalisha fedha.

“Kinachopaswa kufanywa ni kutafuta masoko, kuhudumia wateja vizuri, kudhibiti wizi, kutoa huduma nzuri na kwa wakati na ikiwezekana tufanye kazi saa 24 kama ilivyoanzishwa awali tuweza kuvuna mizigo ya Wanyarwanda ambao sasa ni marafiki wa dhati wa Tanzania, Waganda, Warundi, Wazambia, Malawi, DRC na hata Zimbabwe kama ilivyokuwa zamani,” anasema Afisa mwingine aliyemkaribisha Kakoko kwa mkoyo mkunjufu.

Masawe naye baada ya kuondolewa, aliteuliwa Injinia Aloyce Matei kukaimu nafasi hiyo ambaye sasa amekabidhi mikoba kwa Injinia Kakoko.

Juni 25, 2016 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa alimteua Mhandisi Deusdedit Conatus Vitalis Kakoko kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania. Kabla ya uteuzi huo, Kakoko alikuwa Meneja Miradi wa Wakala wa Barabara Tanzania.

Kakoko alitajwa kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Ephraim Mgawe, ambaye kwa sasa yuko mahakamani Kisutu akishitakiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka. Kabla ya Kakoko, Mhandisi Madeni Kipande anayetajwa kuwa naye huenda akafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa, aliteuliwa na Dk. Harrison Mwakyembe kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, lakini kwa bahati mbaya alizalisha vurugu kubwa katika uongozi wake hadi Waziri Samuel Sitta akamuondoa baada ya kumuundia Kamati ya uchunguzi.

Baada ya Kipande kuondoka, Awadh Masawe aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, lakini naye hivi karibuni uteuzi wake umetenguliwa kutokana na kashfa ya upotevu wa makontena, ambayo wakati yanapotea Masawe alikuwa Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, ambayo ilinyang’anywa mamlaka yote na Kipande kazi zake zikahamishiwa Makao Makuu ya TPA, hadi makontena kupotea.

Kwa upande wake, Kakoko ni kiongozi kwenye msimamo wa hali ya juu na anakumbukwa kwa tukio kubwa la aina yake, ambapo Desemba 20, mwaka 2009 alivuja hoteli ya Snow Crest jijini Arusha iliyojengwa kwa gharama ya Sh. bilioni 10, zikiwa ni siku mbili tu baada ya hoteli hiyo kuwa imefunguliwa na Rais Jakaya Kikwete Ijumaa ya Desemba 18, 2009.

Wakati huo, Kakoko alikuwa Meneja wa Wakala wa Barabara mkoani Arusha na alisema kuwa mwekezaji mzawa Wilfred Tarimo, alikuwa amejenga hoteli kwenye hifadhi ya Barabara Kuu ya Arusha-Moshi, akidai kuwa ameingilia eneo la barabara kinyume na sheria. Wengi wanaamini msimamo aliouonyesha Kakoko kwenye tukio hilo, akiutumia kusimamia sheria ataweza kudhibiti wizi katika TPA na kuongeza ufanisi wa Bandari nchini.

 

Mbinu za wizi wanazotumia

Uchunguzi umebainisha kuwa shehena za mizigo inayopokelewa inakuwa na tofauti ya kumbukumbu zikilinganishwa za mfumo wa TANCIS na mfumo wa CMS. Kwa mfano katika mwaka wa fedha 2014/2015 shehena yenye bidhaa 143, nyingine yenye bidhaa 311; na yenye bidhaa 17, ziliripotiwa kutolipiwa hata senti tano, kwa mujibu wa CAG. Inaongeza kuwa meli 15 zilitia nanga katika Bandari, lakini hazionyeshi kumbukumbu yoyote ya malipo.

Uchunguzi umebaini kuwa hata usalama wa taifa kuna nyakati unakuwa hatarini kutokana na maafisa wa Bandari kutofanya kazi zoa inavyostahili. Kwa mfano kwa miezi Septemba na Oktoba, 2014, meli mbili ziliruhusiwa kuondoka na mfanyakazi ambaye si wa Idara ya Mapato.

Kisheria meli zote zinapaswa kuondoka pale tu wafanyakazi wa Idara ya Mapato wanapojiridhisha kuwa kila kitu kiko sahihi, lakini kwa mshangao mkubwa wafanyakazi wawili; Saidi Milanzi wa Idara ya Marine na Karani Michael Msanga waliruhusu meli.

Milanzi aliruhusu meli ya Morning Cornet, iliyotia nanga Septemba 14, 2014 (saa 08:41 mchana) na kuondoka Oktoba 10, 2014 (saa 12:00 jioni), huku Msanga akiruhusu meli mbili; JOP Scorpius iliyofika Sepemba 22, 2014 (saa 10:35) ikaondoka Septemba 25, 2014 (saa 11:28) na Commodore iliyofika Oktoba 12, 2014 (saa 12:45) na kukondoka Oktoba 13, 2014 (saa 08:12).

Ukiukaji huu wa utaratibu unaikosesha Serikali mapato na umekuwa ukitajwa kuwa umekuwa chimbuko la kusafirisha bidhaa haramu ikiwamo nyara za serikali ambapo pembe za ndovu zimekuwa zikipatikana nchini China baada ya kuwa zimepakiwa Bandari ya Dar es Salaam. Hili na mengine mengi, wafanayazi waadilifu wanaamini Injinia Kakoko atapaswa kuyadhibiti.

Suala jingine lililobainika ni kuwa kitengo cha tozo kinatoa ankara za madai, lakini ankara hizo hazilingani na fedha zinazolipwa benki, hivyo wachunguzi wa mambo wamemtaka Kakoko kuangalia mwanya huo pia.

“Sisi tunaliamini Gazeti la JAMHURI, ndiyo maana tumeamua kupita kwenu, tumjulisha Mkurugenzi Mkuu Injinia Kakoko mianya ya uvujaji wa mapato ilipo. Tunaamini akiyafanyia kazi, ataongoza raha mustarehe, akiacha kazi hii na kuanza kutafuta watu badala ya kutafuta kazi iliyomleta, basi ajue kuwa kazi hii itakuwa ngumu kwake, na anaweza kuishia Kisutu mahakamani kama walivyo watangulizi wake wengi,” anasema mtoa habari mwingine.

Vyanzo vyetu vimelieleza JAMHURI kuwa maafisa wengi wanapata fedha ‘ndefu’ kwa kuelewana na wenye mizigo kisha wakawatoza kodi ndogo. “Kiwango cha chini cha ada ya Pilotage kinachotumika ni Dola za Marekani 55 badala ya Dola za Marekani 150 ambazo zipo kwa mujibu wa mwongozo wa tozo wa April 2013. Hii inaipotezea Bandari mapato na TPA kwa kiasi kikubwa, aliangalie. Watu wananufaika huko,” anasema mtoa habari mwingine.

Kwa makusudi wanatumia taarifa zisizo sahihi kukokotoa mizigo, ambapo unakuta wanaonyesha makontena yana vyandarua, wakati uhalisia yana magari ndani yake.

 

Jamana atapeliwa

Wakati huo huo, mmoja wa wafanyakazi wa Bandari ameshirikiana na ndugu yake kuifanyia utapeli Kampuni ya Uchapishaji ya Jamana Printers.

Kwa mujibu wa nyaraka za Bandari, Kampuni ya Invex Holding Limited, iliomba zabuni Na AE/016/2015-16/CTB/G/18 kwa ajili ya kuchapisha Diaries na Kalenda za mwaka 2016 kwa gharama ya 96,760,000 na ikapewa ushindi Oktoba 13, 2015, lakini ikawa haina mtaji.

Baada ya kukosa mtaji, aliomba barua ya dhamana ambapo Mfanyakazi wa Bandari, M. H. Kissanta, kupitia barua yenye Kumb. Na. SU/3/3/01 ya Januari 6, 2016 alimwandikia barua Meneja wa Benki ya CBA Tawi la Nyerere Road, akimjulisha kuwa wana mkataba na Invex Holding Limited, hivyo apewe msaada unaotakiwa na akikamilisha kazi atalipwa fedha zote kupitia akaunti hiyo hivyo deni atakalokuwa nalo litakatwa moja kwa moja.

Jamana Printers, ambao awali walikuwa wameomba zabuni hiyo kwa gharama ya Sh milioni 53, pamoja na kunyimwa akapewa huyo Invex Holding kwa gharama ya Sh milioni 96, hata baada ya Rais John Mafuguli kupiga marufuku uchapishaji wa dairy na kalenda serikalini, bado walipelekewa kazi hiyo wakaichapa kwa gharama ya Sh milioni 38,454,000 wakazikabidhi kwa kampuni hiyo.

Kwa ujanja wa hali ya juu, Invex baada ya kukabidhiwa kalenda na diary hizo, ilifungua akaunti nyingie benki ya CRDB ikaingiziwa fedha zote kutoka Bandari na hadi leo Jamana Printers wanaendelea kuidai Bandari kwani iliwapa hakikisho kuwa fedha hizo zingelipwa CBA ndipo wakakubali kuchapa kalenda hizo.

Afisa Masoko wa Jamana Printers, Hellen Mushi ameliambia JAMHURI kuwa tayari wamefungua kesi polisi na Mhusika amekamatwa, ila bado wanaendelea na mazungumzo na Bandari kuona kwa nini wao wamekiuka maelekezo yao waliyotoa kupitia barua waliyomwandikia meneja wa Benki ya CBA.

“Bandari hawawezi kulikwepa hili. Wao walituhakikishia kuwa malipo yangepitia kwenye akaunti ya CBA, sasa imekuwaje yakapitia CRDB? Sisi tunayo barua yao yenye maelekezo halali, na kalenda tumechapa na kuwasambazia kilichosalia sasa ni hatua za kisheria dhidi ya Bandari ikiwa hawataki kutulipa stahiki yetu.

“Tuliomba zabuni hii kwa bei ndogo wakatunyima na kumpa mtu ambaye gharama yake ni karibu mara mbili ya gharama halisi, potelea mbali ameileta kwetu kwa sababu hana mitambo wala nini tukaifanya, na bado wanashirikiana naye kututapeli, hili halikubaliki,” Mushi ameliambia JAMHURI.

JAMHURI ilipowasiliana na Afisa wa Bandari, Juma Mwenda anayetuhumiwa kuchepusha malipo yasiende CBA, Mwenda alisema “tuwasiliane baadaye”.

 

Kakoko aomba muda

JAMHURI limewasiliana na Injinia Kakoko kuomba kufahamu mpango mkakati wake na amelenga kufanya nini kuhakikisha Bandari inarejesha heshima yake kwa kutoa huduma bora na kwa wakati, ila akasema: “Naomba unipe muda angalau mpaka wiki ijayo, tutazungumza. Ndo nimefika ofisini bado najifunza, sitatenda haki kusema kabla sijaelewa kinachoendelea. Nipe muda kidogo kaka,” amesema Ijinia Kakoko.

Taarifa za uhakika ambazo JAMHURI limezipata zinaonyesha kuwa siku za Alhamisi na Ijumaa, Injinia Kakoko alizitumia kutembelea maeneo mabalimbali ya Bandari ya Dar es Salaam ikiwamo eneo la Flow Meter kule Mji Mwema Kigamboni. Wafanyakazi waliozungumza na JAMHURI wameonyesha imani kubwa kwa Kakoko wakisema wanaamini atairudisha Bandari kwenye mstari.