Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar imesema uchunguzi wao umeonesha dawa nyingi za kulevya zinazoingizwa visiwani humo zinatoka Tanzania Bara kupitia bandari bubu.
Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Burhani Zuberi Nassor amesema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuteketeza dawa za kulevya Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja.
“Tumefanya uchunguzi na kubaini kwamba dawa za kulevya zinazoingizwa nchini nyingi zinatoka katika mikoa jirani ya Tanzania Bara ikiwemo Bagamoyo na Tanga ambazo huingizwa kwa kutumia bandari bubu,” amesema Nassor.
Amesema utafiti umebaini dawa za kulevya zinaingizwa nchini kwa wingi kwa kutumia njia za bandari ambazo sio rasmi katika kisiwa cha Unguja na Pemba.
Nassor amesema kumekuwa na ongezeko la uingizaji wa dawa za kulevya aina ya bangi kutoka maeneo ya Tanzania Bara jirani na Zanzibar ikiwemo Bagamoyo na Tanga.
Amesema mikakati imewekwa kudhibiti bandari ambazo si rasmi lakini ni vigumu kwa sababu bandari zinatumiwa na wananchi wakiwemo wavuvi kwa shughuli za kila siku.
Nassor amesema wameteketeza dawa za kulevya za aina mbalimbali zikiwemo heroin kilogramu 21, bangi kilogramu 16.65 na mirungi.
Amesema Mamlaka imeteketeza dawa hizo baada ya kumalizika kwa kesi za watuhumiwa mbalimbali ambao walikuwa wamekamatwa na dawa hizo katika maeneo mbalimbali.
“Licha ya kuteketeza dawa za kulevya pia tumetaifisha mali zinazotokana na chumo haramu ikiwemo gari na pikipiki na vitu vingine,” amesema Nassor.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Harusi Said Suleiman amesema wamejipanga kuhakikisha mamlaka inakuwa na uwezo kamili katika kupambana na kudhibiti uingizaji wa dawa za kulevya.