BandariImenichukua miaka miwili kufikiri juu ya hiki kinachoitwa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo. Ujenzi huu ulianza kutajwa mwaka 2010, na ilipofika Machi 2013, Rais wa China, Xi Jinping, akatia saini mkataba wa ujenzi wa bandari hiyo.
Mkataba ukasema bayana kuwa ujenzi huu utatengewa dola bilioni 10. Nilisubiri kusikia Watanzania wanasema nini, ila muda wote naona kimya.
Mkoa wa Mtwara kidogo ndiyo walipinga ujenzi huu. Wao walikwenda mbali zaidi wakahusisha hata gesi ya Mtwara kuwa ingepelekwa Bagamoyo. Binafsi nimekuwa nikifikiri ‘kimya kimya’ lakini leo nikaona heri niwaze kwa sauti. Kama binadamu tunaweza kufanya makosa. Tunaweza kuwa na sera isiyotekelezeka au inayopoteza mwelekeo kulingana na wakati.


Si jambo la ajabu kubadili uamuz au sera. Mfano, nchi hii ilikuwa ni nchi ya Ujamaa na Kujitegemea. Nikiangalia matendo yanayoendelea, hata wajukuu wa Ujamaa na Kujitegemea walikwishafariki. Nasema walikwishafariki kutokana na kwamba kwa sasa kila kitu ni malipo tu. Hospitalini, shuleni, maji, umeme na hata kujisaidia haja ndogo na kubwa siku hizi ni malipo tu. Bado Ujamaa upo hapo?


Nikirejea katika kujitegemea huko ndiyo basi. Hivi ninavyozungumza ndiyo Taifa letu liko tegemezi kuliko wakati wowote. Leo tunategemea wafadhili katika bajeti yote ya maendeleo. Nasikitika na kushawishika kujiona kuwa Tanzania sasa ni kizazi cha ajabu. Nimesikia wabunge wakitamka kuwa hakuna wizara iliyopata fedha zaidi ya asilimia 40 ya bajeti zilizotengewa.
Sitanii, baadhi ya mambo yanatia uchungu. Wiki iliyopita nilijaribu kwa mbali kugusia shilingi inavyoporomoka. Tunajua wafadhili walivyoishikia fimbo Serikali mwaka uliopita hadi Rais akaamua kuwatosa watendaji wake. Iwe tatizo la Escrow lilikuwa la kweli (kama ninavyoamini hadi leo) au la, lakini kitendo cha wafadhili kutumia fimbo ya misaada kuipa makataa Serikali, kimenitisha.


Nimejaribu kuwaza na kuwazua. Nimesoma na kusikiliza ajenda mbalimbali zinazotolewa na Serikali yetu kuruhusu ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo. Wanasema kampuni kutoka China itajenga bandari hiyo kwa gharama ya dola bilioni 10, yaan shilingi trilioni 20. Kiasi ambacho ni zaidi ya bajeti ya nchi nzima iliyokuwa ya mwaka jana Sh trilioni 19.5.
Fedha hizi nyingi ambazo zingeweza kuendesha uchumi wa Tanzania kwa mwaka mzima na zaidi, sasa wanalenga ziwekezwe Bagamoyo! Bado nasisitiza kuwa ukisikiliza wazo la kuchagua Bagamoyo, msisitizo ni kwamba itapunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam na kwamba vitajengwa vipande vya reli na barabara ya lami kuunganisha Bagamoyo na Mlandizi.


Wakubwa hawa wanasema bandari hiyo itatumiwa na Wachina kusafirisha mizigo yao, hasa shaba kutoka Zambia ambako kwa sasa wanamiliki migodi mikubwa. Hakuna anayewaza kuwa bandari hii itatumika kusafirisha nondo au saruji inayozalishwa Tanzania, hakuna anayewaza kuwa bandari hii inaweza kugeuka mwiba kwa usalama wa Taifa ikiwa waendeshaji wa bandari hii ni wajenzi wenyewe.
Sitanii, binafsi siwaonei gele watu wa Bagamoyo na pengine dhana kwamba Rais Jakaya Kikwete kwa kujenga bandari Bagamoyo atakuwa amewapatia ajira watu wa Jimbo lake, hainisumbui. Tatizo nililopata hapa ni faida ya bandari hiyo.   Niseme wazi tu kuwa ujenzi wa bandari mpya pale Bagamoyo ni maandalizi ya kuua Bandari ya Dar es Salaam.


  Nchi hii ina mipango mingi ajabu. Wakati unaingizwa mradi mpya wa Bagamoyo, kuna ujenzi wa Bandari ya Mwambani Tanga unaendelea. Kuna ujenzi wa Bandari ya Mtwara unaendelea kwa kasi yakiwa maandalizi ya kusafirisha gesi nje ya nchi. Najiuliza, ilikuwapo sababu gani kujenga bandari nyingine Bagamoyo badala ya kupanua Bandari ya Dar es Salaam na kuboresha miundombinu?
Kiasi kilichotengwa kujenga Bandari ya Bagamoyo iwapo kingetumika nusu yake, tungeweza kuboresha Bandari ya Dar es Salaam na miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam. Mwaka 1906, Mjerumani alijenga reli ya kwanza kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Tabora. Hadi mwaka 1914, reli iliweza kufika Kigoma na Mwanza.  


Leo miaka miaka 109 baadaye, yaani mwaka 2015 sisi tunaona usafiri wa reli haufai tunatumia malori yanayomilikiwa na wakubwa. Tunatumia malori kutoa mizigo bandarini, tunatumia malori kusafirisha mizigo nje ya nchi.
Mwalimu Julius Nyerere alijenga Bandari Kavu pale Isaka, Shinyanga, lakini leo ile bandari haijulikani iko wapi na inafanya nini.
Sehemu ya fedha hizo zinazopelekwa  Bagamoyo kama zingewekezwa katika kufufua Reli ya Kati, zikajengwa barabara na za juu (fly-overs) Dar es Salaam, zingekuwa na mshindo mkuu katika uchumi. Maisha ya wakazi wa Dar es Salaam yangefunguka, usafirishaji wa mizigo ya nchi jirani ungerahisishwa badala ya kujenga bandari kwa ajili ya nchi moja pekee, China.


Sitanii, najua wataibuka mabingwa wa propaganda hapa watasema bado mizigo ya nchi jirani itapitishwa pale Bagamoyo, ila tujue ikipita pale waliotoa fedha za kujenga Bandari ndiyo wenye kukusanya mapato. Itakuwapo miundombinu ya kisasa na mizuri lakini kiuchumi itakuwa ni sawa na tembo mweupe, ambaye kila mlimwengu atamshangaa.
Katika kupita kwangu nimekutana na wananchi wa kawaida wengi wenye kujadili kwa nini thamani ya shilingi ya Tanzania imeshuka. Majibu ya wananchi hawa yameniacha hoi. Mmoja ameniuliza maswali yafuatayo na huenda hata wewe yanakuhusu. Naomba nikuulize maswali hayo hayo, kama ifuatavyo:-
Unashangaa shilingi ya Tanzania inashuka? Hivi jiangalie hapo ulipo. Simu uliyoshika imetoka China. Kalamu unayotumia imetoka China, gari unalotumia iwe daladala au gari binafsi yanatoka nje ya nchi. Shati, suruali, sketi, nguo za ndani, mashuka nyumbani, vijiko, sufuria, sukari na hata unga vyote kutoka nje ya nchi.


Mwalimu Nyerere alijenga viwanda kwa ajili ya kuzalisha bidhaa za matumizi yetu kama Watanzania na kisha kuuza nje ya nchi tukapata dola. Hivi leo kiwanda cha majembe UFI kiko wapi? Kiko wapi kiwanda cha nyama cha Tanganyika Packers? Kiko wapi kiwanda cha kutengeneza tairi cha General Tyre? Viwanda vya nguo kama Urafiki, Sunguratex, Mwatex, Mutex, viko wapi?
Kiwanda cha pamba cha SHIRECU kiko wapi? Jiulize tu maduka ya mikoa kama RTC, mashirika kama SUKITA, MMMT, Benki ya Nyumba (THB), Benki ya Ushirika Vijijini (si CRDB ya sasa inayokopesha matajiri), Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), KAMATA, Reli ya Tanga, Moshi hadi Arusha, Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC).


Leo tunamsifia Said Salim Bakhresa kwa kuwa tajiri, lakini anatumia majengo na vihenge vilivyojengwa kwa kodi za wananchi. Nenda ukaangalie Mbeya kama Shirika la Zana za Kilimo bado lipo. Angalia mashirika ya usafirishaji ya mikoa maarufu kama RETCO yako wapi? Mwadui Shinyanga na almasi yake mbona haivumi tena?
Kiwanda cha Tumbaku Morogoro na Sigara Dar es Salaam bado ni vyetu au tunamiliki kwa hadithi za vitabuni?  Katani Tanga iko mikononi mwa Serikali tena? Kiwanda cha Chai (TATEPA) leo tunasikia kiko mikononi mwa mwanasiasa Joseph Mungai kinaitwa Chai Bora. Zabibu Dodoma, mvinyo wenye sifa ya pekee unaotumika hadi makanisani, bado Serikali inajua uzalishaji ukoje?


Kahawa imetelekezwa. TANICA na Bucop vinajiendesha kwa kuchechemea. Ukiangalia pamba kwa Wasukuma ndiyo sasa wanang’oa miche na kupanda mahindi. Nenda Mtwara uangalie magofu ya viwanda vya korosho. Rejea hapa Dar es Salaam ukaangalie mashirika karibu 400 yaliyouzwa kama si maghala, na wakubwa hawajajenga nyumba za kupanga kwenye viwanda badala ya uzalishaji!
Sitanii, baada ya kukumbusha tone katika bahari unadhani Tanzania sasa inacho cha kusafirisha nje ya nchi? Si inawezekana Rais Kikwete yuko sahihi kuwapa Wachina nafasi ya kujenga bandari pale Bagamoyo weweze kusafirisha shaba nje ya nchi kutoka Zambia, na sisi Tanzania tuko ‘busy’ kuandika miradi ya kuomba ufadhili kwa MCC na mingine?


Ndugu yangu msomaji, inawezekana wewe hili halikusumbui. Najaribu kupata tafsiri pana. Serikali kisera kuamua kujenga bandari kwa ajili ya taifa moja, ni wazi kuwa haina mpango wa yenyewe kuzalisha na kuuza nje ya nchi. Matokeo ya sera kama hii ni nchi kuendelea kuwa ombaomba. Matokeo yake ni wafadhili kuchagua kama wawalipie dawa hospitalini au elimu.
Hapa tulipofika kama hatutafunga breki, China itakuwa na nguvu kubwa katika uendeshaji wa uchumi wetu. Sera yetu ya mambo ya nje pamoja na mwaka 2004 kubadilika kutoka Sera ya Siasa ya Ukombozi kwenda Diplomasia ya Uchumi, haikufuta Sera ya Kutofungamana na Upande Wowote. Wachina tunawakaribisha mno. Kosa hili la Bandari ya Bagamoyo litaigharimu nchi kabla ya mwaka 2050.


Usalama wa Taifa hili utakuwa hatarini. China itakuwa inashikilia mlango wa kuingilia nchini. Wakipata kiongozi asiye na maadili wataingiza hadi silaha kupitia bandari hii. Naomba kuweka kumbukumbu sawa. Kuwa, mosi, sina hamu ya kuona kifo cha Bandari ya Dar es Salaam. Pili, uwekezaji utakaofanywa Bagamoyo hautakuwa na tija kubwa katika uchumi wa Taifa letu.


Sitanii, Watanzania wenzangu fungueni masikio. Tuweke kando siasa za umajimbo na umimi. Madereva kama wameungana na kuifanya Serikali itende watakavyo, tutakuwa wa ajabu mno iwapo tutaacha uchumi wa Taifa letu ukalengeshwa na hatimaye vizazi vyetu kukuta magofu.   
Narudia, fedha za kujenga Bandari ya Bagamoyo ziwekezwe katika Bandari ya Dar es Salaam na tuanze kufufua viwanda vya ndani tuuze bidhaa nje ya nchi, vinginevyo tumekwisha.