Naibu Balozi wa Ujerumani Mhe. Jörg Herrera (kulia) na Naibu Balozi wa Israel Mhe. Michael Baror (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na Mkurugenzi wa Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) ya nchini Israel Simon Fisher mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea Taasisi hiyo ili kuona maendeleo ya kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto inayofanywa kwa pamoja na madaktari bingwa wa Moyo wa JKCI, Israel na Ujerumani.

Naibu Balozi wa Ujerumani Mhe. Jörg Herrera (kushoto) na Naibu Balozi wa Israel Mhe. Michael Baror (kulia ) wakimjulia hali mtoto Cecilia Mashao (7) ambaye amefanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua wa kuziba tundu la moyo katika kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto inayofanywa na madaktari bingwa wa Moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Israel na Ujerumani. Katikati ni Mke wa Naibu Balozi wa Ujerumani Dkt. Marlies Herrera.

Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Fedha kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Agnes Kuhenga akisalimiana na mke wa Naibu Balozi wa Ujerumani nchIni Dkt. Marlies Herrera aliyeambatana na mme wake aliyetembelea Taasisi hiyo ili kuona maendeleo ya kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto inayofanywa kwa pamoja na madaktari bingwa wa Moyo wa JKCI, Israel na Ujerumani. Katikati ni Naibu Balozi wa Ujerumani Mhe. Jörg Herrera.

Daktari Bingwa wa watoto wenye matatizo ya moyo waliolazwa katika chumba cha wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU) Vivian Mlawi akielezea maendeleo ya afya za watoto waliofanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua na kuzibwa matundu ya moyo katika kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanywa kwa pamoja na madaktari bingwa wa Moyo wa JKCI, Israel na Ujerumani.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Robert Mallya akiwaonyesha maeneo mbalimbali ya JKCI wageni kutoka Ubalozi wa Ujerumani na Israel waliotembelea Taasisi hiyo kwa ajili kuangalia maendeleo ya kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto inayofanywa kwa pamoja na madaktari bingwa wa Moyo wa JKCI, Israel na Ujerumani.

Naibu Balozi wa Ujerumani Mhe. Jörg Herrera (kushoto) akisaini kitabu cha wageni wakati alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kuona maendeleo ya kambi maalum ya matibabu ya upasuaji wa moyo wa bila kufungua kifua kwa watoto inayofanywa kwa pamoja na madaktari bingwa wa Moyo kwa watoto wa JKCI, Israel na Ujerumani. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Fedha Agnes Kuhenga.

 

23/1/2018 Balozi za Israel na Ujerumani hapa nchini zimeahidi kuendelea kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ili kuhakikisha watanzania hasa watoto wanapata huduma bora za matibabu ya moyo.

Hayo yamesemwa leo na Manaibu Balozi wa nchi hizo walipotembelea Taasisi hiyo leo ili kuona maendeleo ya kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto inayofanywa kwa pamoja na madaktari bingwa wa Moyo kwa watoto wa JKCI, Israel na Ujerumani.

Matibabu hayo ya magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo yanatolewa kwa watoto wenye umri wa kuanzia mwezi mmoja hadi miaka 18  yanafanywa  kwa njia ya upasuaji wa bila kufungua kifua (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa Cathlab.

Naibu Balozi wa Ujerumani nchini  Mhe. Jörg Herrera alisema kuwa nchi yake imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika mambo mbalimbali ya maendeleo ikiwemo afya hivyo basi watafanya kila wanachoweza  ili kuunga mkono jitihada za kuimarisha afya hapa nchini.

“Nimetembelea leo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ili kuona kambi ya pamoja ya upasuaji wa moyo inayofanywa na  madaktari wa JKCI, Israel na Ujerumani nimefurahi  kuona kazi nzuri ya kiwango cha kimataifa inayofanyika hapa ya kuokoa afya za watoto”.

“Wanafanya upasuaji wa bila kufungua kifua kwa watoto wenye matatizo ya moyo nafikiria kuimarisha  zaidi mahusiano tuliyokuwa nayo  ili tuweze kuokoa maisha ya watoto wengi zaidi kwa faida ya kizazi kijacho”, alisema Mhe. Naibu Balozi Herrera.

Naye Naibu Balozi wa Israel nchini Mhe. Michael Baror alisema nchi yake inajivunia  kuwa sehemu ya watoa huduma wa matibabu hayo wataendelea kubadilishana uzoefu wa kazi kwa kuwaleta madaktari ambao watafanya kazi na wataalamu waliopo hapa nchini hii ikiwa ni moja ya kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizi mbili.

“Tumekuwa tukifadhili  elimu za madaktari na wauguzi wanaotoka JKCI na kuja kusoma nchi kwetu vilevile tunatoa matibabu kwa watoto wenye matatizo ya moyo ambao wengine tunawatibu hapa nchini na wengine wanatibiwa nchini kwetu. Nafurahi kuona mahusiano yetu yanafanikiwa na kuimarika zaidi naamini wataalamu hawa wa afya wanapata ujuzi wa kutosha zaidi”, alisema Naibu Balozi Mhe. Baror.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa  ya Moyo ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo Peter Kisenge alisema kambi hiyo ya siku sita inafanya upasuaji wa bila kufungua kifua kwa  kuziba matundu ya moyo kwa watoto wenye umri wa mwezi mmoja hadi miaka 18.

Dkt. Kisenge alisema kuwa madaktari hao kutoka Ujerumani na Israel wanafanya upasuaji wa kuziba matundu na kutoa mafunzo kwa madaktari wa JKCI ya  jinsi ya kuziba matundu ya moyo kwa watoto na kuwahudumia watoto wenye matatizo hayo.

Tangu kuanza kwa kambi hiyo tarehe 20/1/2018 jumla ya watoto 32 wamefanyiwa uchunguzi na watoto 10 wamefanyiwa upasuaji wa  kuziba matundu ambapo hali zao  zinaendelea vizuri na wataruhusiwa pindi afya zao zitakapoimarika.