Na Stella Aron, JamhuriMedia,Dar

Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Dkt.Wiebe de Boer akizungumza wakati akifungua kikao kazi cha Jukwaa la Wahariri na waandishi wa habari kinachojadili sheria ya habari leo Alhamisi Oktoba 20, 2022 kwenye hoteli ya Slipway jijini Dar es Salaam.

BALOZI wa Uholanzi nchini Tanzania, Wiebe de Boer amelipongeza Jukwaa la Wahariri (TEF),kwa juhudi kubwa za kutoa elimu juu ya umuhimu wa maboresho ya sheria za habari nchini.

Akifungua mafunzo kwa wahariri na wanahabari yanayoangazia uchechemuzi wa sheria za vyombo vya habari nchini ambayo yanaratibiwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), balozi amesema kuwa uhuru wa habari ni miongoni mwa nguzo muhimu katika kuchochea ustawi bora wa demokrasia.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF Bw. Deodatus Balile kushoto na Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF Bw. Bakari Machumu wakiteta jambo katika kikao hicho.

“Ninawapongeza TEF kwa juhudi za kutoa elimu juu ya maboresho ya habari kwani uhuru wa habari ni nguzo muhimu katika ustawi wa demokrasia pia demokrasia inategemea upatikanaji wa taarifa kwa uwazi na za kuaminika.

“Hivyo hivyo, ustawi wa maendeleo unategemea taarifa sahihi na za kuaminika, hivyo nichukue nafasi hii kuipongeza TEF kwa kushiriki kikamilifu katika kutoa hamasa na elimu juu ya umuhimu wa maboresho ya sheria za habari nchini.

Hata hivyo alifurahishwa na ujumuishwaji mkubwa wa wanawake katika mafunzo hayo,na kuwataka wanahabari kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhamasisha mazingira wezeshi ya upatikanaji wa habari nchini.

“Tumeona juhudi kubwa ambazo zinafanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kwani ameonesha dhamira njema katika kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari, nasi tutaendelea kuunga mkono juhudi hizo,” amesema.

Akimkarisbiaha mgeni rasmi Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile ameipongeza Serikali kwa kuonesha utayari wa kufanya maboresho ya mabadiliko ya sheria ya habari ambayo imekuwa na vikwazo kwa wanahabari na kushindwa kutimiza majukumu yao.

Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Dkt.Wiebe de Boer akiwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF Bw. Deodatus Balile kushoto na Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF Bw. Bakari Machumu pamoja na baadhi ya wajumbe mara baada ya kufungua kikao kazi cha Jukwaa la Wahariri na waandishi wa habari kinachojadili sheria ya habari leo Alhamisi Oktoba 20, 2022 kwenye hoteli ya Slipway jijini Dar es Salaam.

Balile amesema kuwa hata hivyo kumekuwa na mwamko wa uhamasishaji wa mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari na umetoa matokeo mazuri hivyo ni jambo la kuishukuru Serikali kwa kuonesha utayari wa kufanya maboresho.

“Lazima tuwe na moyo wa shukurani kwa Serikali, tumeona magazeti ya Mawio, Tanzania Daima na Mseto yakifunguliwa na kuna juhudi mbalimbali zinaendelea ili kuhakikisha sheria ambazo zinaonekana kubinya uhuru wa vyombo vya habari zinafanyiwa maboresho,”amebainisha

Balile amesema kuwa Mei 3, mwaka huu wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti’ katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha, Rais Samia alitoa maagizo; “Nimeelekeza sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,”aliagiza Rais Samia.

“Kuna maagizo yanatolewa na sisi tunavyosubiri ni utekelezaji wake hivyo tunasubiri katika Bunge lijalo kuwepo kwa jambo bungeni kuhisina na mchakato huu wa mabadiliko ya baadhi ya vingufu vya sheria ambavyo vinaonekana kuwa mwiba kwa wadau wa habari,” amesema.

Akifunga mafunzo hayo,Makamu Mwenyekiti wa TEF, Bakari Machumu, amesema ili kupata mafanikio ni vyema waandishi wakashirikiana katika kutoa elimu kwani kuna vifungu vinavyomkandamiza mwandishi na kutakiw akufanyiwa maboresho.

“Tusisubiri wengine watutetee, tuanze sisi wenyewe na haya mafanikio yatapatikana kwa ushirikiano,” amesema.

Anita Mendonza Afisa Mtendaji Mkuu Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) akifuatilia kikao hicho kinachofanyika kwenye hoteli ya Slipway jijini Dar es Salaam pamoja na Elizaberth Chanzi mmoja wa maofisa wa TEF.
Baadhi ya wahariri wakifuatilia mada mbalimbali