Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel John Nchimbi, leo Jumapili, Aprili 21, 2024, amezuru kaburi la Hayati Kepteni (mst) John Damiano Komba na kutoa heshima zake kwenye kaburi hilo kwa kuweka shada la maua.
Dkt. Nchimbi ambaye ameambatana na Katibu wa NEC – Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa Amos Makalla pamoja na Katibu wa NEC – Oganaizesheni wa CCM Taifa Issa Haji Gavu, pia alipata wasaa wa kuwasalimia na kuwapatia pole familia, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wa Kijiji cha Lituhi, alipozikwa Kepteni Komba.
Hayati Komba, ambaye alikuwa mhamasishaji mkuu wa CCM, akiwa pia amefanya kazi kubwa ya nchi, kupitia kazi za sanaa, na aliwahi kuwa Mbunge wa Majimbo ya Mbinga Magharibi na Nyasa, kwa nyakati tofauti, kwa tiketi ya CCM, alifariki dunia mwaka 2015 tarehe 28 mwezi Februari.
Akiwa hapo Lituhi, Dkt. Nchimbi, amekutana na familia na wananchi wa maeneo ya karibu waliojitokeza kuungana nae katika kuzuru kaburi la Komba na kumuombea apumzike kwa amani.
*”Kwa niaba ya viongozi wenzangu na wanachama wote wa CCM, tumekuja mahali hapa kuona kaburi la aliyekuwa mkuu wa vikosi vya sanaa vya CCM na ni kwa sababu ya kuthamini na kutambua mchango mkubwa katika kushiriki na kuandaa Taifa, vita ya kuitetea Tanzania dhidi ya Uganda, kutangaza na kutoa elimu juu ya ugonjwa wa Ukimwi, kuimarisha sanaa kwa mziki wa jadi na wa kisasa pamoja na mengine mengi yenye msingi imara kwa Taifa letu. CCM itaendelea kuthamini na kuhakikisha aliyoyaanzisha hayati Kepteni Komba hayapotei bure,” amesema Dkt. Nchimbi.
Naye, Dkt. George John Komba kwa niaba ya familia ya marehemu Komba, amesema;
“Tunatoa shukrani kwa CCM kuanzia kwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wote wa taifa, mkoa, wilaya , kata, matawi, mashina na wajumbe wote kwa kuedelea kukumbuka kazi ya hayati Kepteni Komba ambaye kwetu ni Baba lakini kwenu ni askari jasiri ambaye amepigana na kushiriki katika kampeni za CCM kupata ushindi wa kishindo katika awamu zote.
”Familia tunawahakikishia tutaendelea kuwa wananchama waadilifu wa CCM sababu mafanikio yetu sote ni yanatokana na CCM na alituachia urithi kwa kusema isitokee hata mmoja akahama kwenda upande tofauti na CCM nasi tunaahidi kukienzi na kuwa wanachama wa hai.” amesema