Mpendwa msomaji natumaini hujambo kiasi. Nakushukuru wewe na wengine kwa ujumbe na mrejesho mkubwa mlionifikishia wiki iliyopita, baada ya makala yangu ya kuomba Watanzania tusifanye majaribio katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Hakika nimejiridhisha, Watanzania tulio wengi tunapenda nchi yetu.
Bila kujali itikadi za vyama, makala ile imekuwa kipimo muhari kwangu kujiridhisha kuwa mwakani tunahitaji Rais mwenye mamlaka, anayeweza kutoa kauli ikaheshimika, maana tukimpata Rais mpiga maneno tu na kuchekesha wageni kwenye majukwaa, hiyo gesi tutaisikia Ulaya, Amerika na China.
Nchi yetu imefikia pabaya. Fedha zimepotea tena Serikalini na kwa sasa zipo mikononi mwa wateule wachache na sasa wameanza kuumiza jamii.
Michango ya harusi wamepandisha viwango, eti kadi ya single (mtu mmoja) ni kuanzia Sh 60,000 na ili mwende na mkeo au mmeo inabidi mchange kuanzia Sh 70,000 (double).
Wanandoa sasa wamesahau majukumu yao. Wamesahau kuwa wanaokuja kwenye harusi yako wamekuja kukuunga mkono na si kukupatia utajiri.
Watu wanatangaza kufanya harusi za Sh milioni 30, wakati mfukoni hawana kianzio hata cha Sh 100,000. Baadhi ya watu wanahonga wawe wenyeviti wa kamati.
Sitanii, mada ya leo inahusu ushoga. Tulishuhudia jinsi Wazungu walivyomsonga Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alipotunga sheria ya kuharamisha ushoga nchini Uganda. Kilichofuata waliamua kuikatia misaada Uganda. Mashoga wakafurahi, wananchi wakakosa maji, huduma za afya, barabara na nyinginezo.
Kwa upande wangu nilifurahi misaada kukatwa. Furaha yangu haikutokana na hatua ya Wazungu kuupigia debe ushoga, la hasha, bali kuipa somo Afrika, hasa nchi zetu za Afrika Mashariki, ukiondoa Kenya, kuwa busara za wahenga bado zinafanya kazi: “Mtegemea cha nduguye, hufa masikini.”
Kenya bajeti yake inategemea fedha za ndani kwa asilimia kwa asilimia 95. Wafadhali wanachangia asilimia 5 tu. Hapa kwetu tunaambiwa wafadhili wanachangia asilimia 30, lakini hiyo asilimia 70 inayosalia ukiuliza unaambiwa kuwa Wizara zimepokea asilimia 30 tu ya bajeti iliyotengwa.
Kwa maana nyingine, taifa letu linatoa asilimia 21 tu ya bajeti kwa wizara zake. Hii ni hatari. Nchi yetu ina maana bajeti tunazosomewa ni hewa.
Serikali mara nyingi huwa inatangaza kwa mbwembe bajeti zake wakati wa kuomba fedha, ila ikifikia hatua ya kuonyesha matumizi huwa ni siri.
Sitanii, wiki iliyopita Balozi Celestine Mushi ametoa kauli iliyonifurahisha juu ya Tanzania kukataa ushoga. Kwa mujibu wa Mtandao wa The Habari, Balozi Mushi katika mkutano wa kujadili maendeleo ya milennia kati ya 2015 hadi 2030 amekataa mapendekezo ya baadhi ya wafadhili.
Balozi Mushi ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, amesema Serikali ya Tanzania haitambui ushoga kama moja ya agenda za maendeleo.
“Tunatambua haki za binadamu, usawa wa kijinsia kati ya wanaume na wanawake na hata katiba yetu pendekezwa imetoa haki za sawa kati ya wanaume na wanawake, lakini katika suala la kutambua ndoa za jinsia moja hilo tumekataa,” amesema Balozi Mushi.
Amesema Tanzania imewambia wafadhili kutoka nchi zilizoendelea na wahisani wa maendeleo katika Umoja wa Mataifa kwamba suala la ndoa za jinsia moja (ushoga) si agenda ya Watanzania na si agenda ya maendeleo.
Balozi Mushi aliongeza kwamba serikali ya Tanzania imeweka msimamo huo hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete aliagiza hivyo kwa maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akimtaka Waziri mwenye dhamana, Bernard Membe kuwa wakatae shinikizo la kukubali suala ushoga kama moja ya ajenda za maendeleo.
Amesema Watanzania wanataka masuala yanayowagusa kama vile maji, elimu, huduma bora za afya, miundombinu ya umeme, ajira na kuondoa umaskini wa kipato.
Balozi Mushi alifafanua zaidi kwamba mambo ya ushoga na ndoa za jinsi moja yanakwenda kinyume na maadili ya Watanzania, maisha, historia, utamaduni, mila na desturi za Mtanzania zinakataza masuala ya ushoga.
Amesema Serikali inatambua kwamba Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, ikiwamo kujamiiana yaliwekwa na mkoloni Mwingereza kabla ya uhuru na Serikali ya Tanganyika imerithi kutoka kwa Serikali ya Mwingereza.
Naamini Waingereza waliona busara kuzuia ushoga, na ndio maana ikawamo katika sheria tulizorithi.
“Watanzania na Afrika kwa ujumla inataka malengo ya milennia na haki za binadamu zisifike mahali kuwadharirisha watu kutoka bara hili kwa kuruhusu mambo yanayokwenda kinyume na historia yao, mila na desturi za Mwafrika,” aliongeza.
Sehemu kubwa ya maandishi ya hapo juu, nimenukuhu habari iliyoandikwa na mtandao wa the Habari. Binafsi nakiri kuwa Balozi Mushi amenifurahisha. Kizazi chetu cha sasa kinapaswa kufikiri. Tunapaswa kujiuliza wazee wetu waliwezaje kupigania uhuru.
Mkoloni wakati wote alikuwa akiwaahidi pipi na biskuti Waafrika. Hawa watu tuliwafukuza. Walipokaa pale Berlin Ujerumaini, nchi zetu waligawana na kupeana hati kama mashamba. Tukawafulu kuwaondosha kwa mtutu wa bunduki. Hivi nani kakwambia wanatupenda hadi watupe misaada?
Sitanii, wakubwa hawa bado wana hasira ya dhati. Hawafurahishwi si tu na ngozi yetu (Mungu anisamehe maana sipalilii ubaguzi), lakini uamuzi wao wa kutoheshimu mila na desturi zetu ni wazi ni aina mpya ya ubaguzi.
Marehemu Profesa Ali Mazrui, wakati namhoji mwaka 2002 pale Hoteli ya Sea Cliff, alinishitua.
Ikumbukwe Profesa Mazrui alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Afrika ya Kudai Fidia (Reparation Committee) kutokana na udhalilisha tuliofanyiwa na kupotezewa nguvu kazi wakati wa utumwa.
Kamati hii ambayo sijui majaliwa yake baada ya kifo cha Profesa Mazrui, Mkenya huyu, ilikwama.
Ilikwama si kwa sababu nyingine, bali Profesa Mazrui aliniambia: “Tatizo kubwa ni kwamba hao tunaokwenda kuwadai fidia, ndio tunaowapelekea maombi ya nauli na posho za kuhudhuria vikao vya kuwadai fidia. Serikali zetu za Afrika, ambazo zitanufaika na fidia hii ikitolewa hazina habari.”
Maneno haya ya Pofesa Mazrui, yalikuwa na uzito wa aina yake. Yalistahili kuyawaza na kuyawazua. Si jambo jepesi unayemdai, kumwomba akulipie nauli na posho ya kuhudhuria kikao cha kumdai. Ni kwa msingi huo vikao vingi havikufanyika na nguvu ya kudai fidia kwa unyama tuliofanyiwa ikapotea.
Sitanii, msimamo wa Balozi Mushi unahitaji ujasiri kuutoa mbele ya Umoja wa Mataifa. Na pengine katika hili nimpongeze Rais Jakaya Kikwete. Kwamba kwa mtiti alioupata Rais wa Uganda, Museveni kwa kukataa ushoga, Kikwete angekubali kirahidi kuepusha shari, hakufanya hivyo.
Tanzania bila misaada inawezekana. Hofu hewa iliyojengwa kuwa bila misaada ya wafadhili nchi haiwezi kwenda ni ufinyu wa mawazo. Wafadhili hawa wanataka almasi yetu, dhahabu yetu, Tanzanite yetu, mbao zetu, gesi yetu, mafuta yetu na mengine mengi tu ambayo hayapatikani Ulaya na Amerika ya leo.
Afrika tukiwa na msimamo, tukataa kushikwa sharubu na wenye nia mbaya, wakajua kuwa wakithubutu wataondoka na kibao, akiri itawarejea.
Hawatathubutu kuleta mawazo ya kipumbavu ya kutaka ushoga uje hapa nchini. Katika hili Watanzania tunapaswa kuungana tukashikamana kupinga ushoga.
Ninachojiuliza ni iwapo tupo tayari kusimamia ajenda hii kwa umoja hadi mwisho. Naamini Watanzania tumegawanyika kwa kiasi kikubwa kwa sasa. Wapo wenye kuamini kuwa chochote kinachowezesha mkono kwenda kinywani kwao ni halali. Mimi nasema Watanzania tuungane kusema ushoga hapana.