Na Mwandishi Maalum,JamhuriMedia,Dar
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amekutana na kuzungumza na Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IOM) Bw. Maurizio Busatti ambaye amejitambulisha rasmi kwa Mhe. Waziri katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho Waziri Mulamula ameipongeza IOM kwa kazi inazofanya nchini na amemuhakikishia Bw. Busatti kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kufanya kazi na Shirika hilo.
Amesema Shirika hilo (IOM limekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika masuala ya wakimbizi, majanga ya asili na kuongeza kuwa ni matumaini yake kwamba Bw. Busatti ataendeleza uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na IOM kwa kuzingatia uzoefu wa muda mrefu alionao kwa kufanya kazi kwa muda mrefu ndani ya shirika hilo.
Balozi Mulamula ameipongeza IOM kwa kuendelea na shughuli za kuwarejesha nyumbani rai awa Ethiopia waliokuwa katika magereza nchini na kuongeza kuwa kitendo hicho kimesaidia Tanzania kukabiliana na msongamano wa watu katika magereza yake.
Ameipongeza IOM na jitihada zake za kukijengea uwezo kituo cha mafunzo cha maafisa Uhamiaji Kanda ya Afrika kilichoko ndani ya Kituo cha mafunzo cha Maafisa Uhamiaji cha mjini Moshi ambapo pia maafisa uhamiaji wa Tanzania wananufaika nacho.
Naye Bw. Busatti ameishukuru Serikali kwa jinsi inavyoshirikiana na Shirika hilo katika kutekeleza majukumu yake hapa nchini.
Bw. Busattia ameahidi kuendeleza ushirikiano mzuri ambao shirika hilo umekuwa na Serikali ya Tanzania kwani imekuwa mdau wake mkubwa katika kufanikisha majukumu yake.