Na Magrethy Katengu, JamhuriMedia
Dar es Salaam
Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), Balozi Meja Jenerali Wilbert Ibuge amefunga kozi ya Kuwaendeleza Makamanda Wanawake wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ) kozi ya Uongozi kwa viongozi waandamizi wa Ulinzi wa Amani kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Taasisi za Serikali za kiraia kutoka Tanzania.
Akizungumza Machi 28, 2025 Dar es Salaam katika hafla ya kufunga kozi hizo amesema lengo la kozi hizo ni kuwaandaa makamanda katika misheni hizo za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa (UN) na za Kikanda Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC
” Niwasisitize mliopata nafasi ya kupata kozi ya uongozi kwa viongozi waandamizi wa ulinzi wa amani kutoka SADC, majeshi mbalimbali na raia mhakikishe wanatumia fursa hiyo kujijengea uwezo ili kufika kwenye uongozi wa juu hatimaye mlete amani katika nchi za kikanda na kuwa na ustawi wa wananchi” amesema Balozi Meja Jenerali Ibuge.

Sanjari na hayo amewataka makamanda wanawake kujijengea uwezo binafsi utakaowawezesha kushiriki misheni mbalimbali za ulinzi wa amani duniani na hatimaye washike nafasi za juu za uongozi katika misheni hizo hasa katika maeneo yanayokabiliwa na machafuko na kuleta matokeo chanya
Meja Jenerali Ibuge amesisitiza pia ni muhimu kuendelea kuwajengea uwezo makamanda hao wanawake ili waweze kuongoza misheni hizo za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa (UN) na za Kikanda ikiwemo EAC SADC
Sambamba na hayo amebainisha kuwa bado kuna idadi ndogo ya wanawake makamanda wanaoongoza misheni hivyo kozi hiyo iliyotolewa na Umoja wa Mataifa ndio ya kwanza hapa Tanzania tangu umoja huo uanze hivyo itatoa nafasi kwa wanawake kujijengea uwezo kuweza kufaham fursa za kikanda na kidunia .

Ni kweli kwamba majeshi karibu yote duniani ukiweka ulinganifu kati ya wanawake na wanaume, wanaume ni wengi, na ni wengi kwa sababu ya asili ya majukumu na siyo kwamba wanawake hawawezi hapana, wanaweza kinachohitajika ni kujiamini kuwa nao wanaweza.
“Kupitia kozi hizi watakuza uwezo wao na itakapofikia wamefikia vyeo vinavyowaruhusu kuingia kwenye uongozi wa juu wa misheni hizi waweze kuingia bila kuwa na tashwishwi,” Amesema Balozi Meja Jenerali Ibuge
Naye Mkuu wa Chuo cha Ulinzi wa Amani Tanzania, Brigedia Jenerali George Itang’are amesema lengo la kozi hizo ni kuwapa fursa ili waweze kutumika katika majukumu mbalimbali kijeshi ndani na nje ya nchi katika masuala ya ulinzi wa amani.

“Ni matarajio yetu kwa maelekezo ya Mkuu wa Majeshi maofisa hawa wamepata ujuzi wa kutosha na watatekeleza majukumu yao ipasavyo, kwa upande wa kozi ya viongozi wa ngapi za juu wa misheni, Tanzania tuna upungufu mkubwa katika hizo nafasi hivyo kozi hizo zitaweza kutengeneza maofisa wa kike na kiume wenye utaalamu wa kutosha watakaotumika katika ulinzi wa amani,” amesema
Kwa upande wake mshiriki wa kozi ya wanawake makamanda, Luteni Kanali Glory Mkwizu amesema kozi hiyo inatoa fursa ya kuwaanda wanawake katika masuala ya ulinzi wa amani na imewapa mbinu za kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuongozi ndani ya Jeshi katika ulinzi wa amani na kwenye jamii iliyowazunguka.
Naye Hamida Matimba kutoka Jeshi la Magereza Tanzania, amesema kozi hiyo inawajenga kiakili na kuwaweka tayari kwa lolote na kwenda popote ambapo mtu atatakiwa kwenda kwa ajili ya kulinda amani.