Na Mwandishi Wetu
Balozi mpya wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi, ameahidi kuitangaza Tanzania na vivutio vyake kimataifa kwa kutumia uzoefu wake katika fani ya uandishi wa habari, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha diplomasia ya uchumi na utalii.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha ZBC cha Zanzibar katika mahojiano maalum, Balozi Matinyi amesema atatumia mbinu mbalimbali za kihabari kung’amua na kujifunza mikakati inayotumika na mataifa ya Ulaya Kaskazini katika kuvutia watalii.
“Nitakapofika katika nchi hizo tisa katika eneo langu la uwakilishi, nitahakikisha natafuta na kuelewa mbinu wanazotumia kuvutia watalii. Watalii wengi duniani huenda kwenye nchi hizo, hivyo tunapaswa kujifunza kutoka kwao,” amesema.

Matinyi amesema uzoefu wake katika uandishi wa habari umemjengea uwezo wa kuwa mdadisi na mtafiti wa taarifa, jambo ambalo litamwezesha kutafuta fursa za uwekezaji na kukuza taswira ya Tanzania nje ya nchi.
Akitaja historia ya diplomasia ya uchumi nchini, amesema kuwa ilianza katika awamu ya tatu ya uongozi wa Tanzania, ikiwa ni jitihada za kujenga uchumi wa taifa baada ya kipindi cha kusaidia mataifa ya Afrika kupata uhuru.
Akizungumzia namna atakavyoitambulisha Zanzibar, Balozi Matinyi amesema tayari amepokea taarifa muhimu kutoka taasisi za uwekezaji, hususan zinazohusika na uchumi wa buluu na sekta ya utalii.
“Tuna nchi tisa katika eneo ninalokwenda ambazo raia wake hupenda kufahamu vyakula vya watu wengine. Nitawasimulia kuhusu viungo vya kipekee vya Zanzibar vyenye ladha ya kipekee,” Amesema.
Nchi ambazo ataziwakilisha mbali na Sweden ni Denmark, Finland, Norway, Iceland, Estonia, Latvia, Lithuania na Ukraine.
Kuhusu mvutano kati ya Ukraine na Russia, Balozi Matinyi alisisitiza kuwa msimamo wa Tanzania ni kuhimiza amani na mazungumzo kama njia ya kutatua migogoro.
“Tanzania inasimama upande wa amani. Tunapenda kuona migogoro ikitatuliwa kwa mazungumzo, si kwa vita,” amesema