Na Andrew Chale, JamhuriMedia, Zanzibar

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Naibu wake katika Wizara hiyo, Cosato Chumi wamejitambulisha rasmi na kufanya mazungumzo Ofisini kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, jana Migombani, Mkoa wa Mjini-Magharibi, Unguja.

Tukio hilo la kujitambulisha, baada ya mabadiliko ya hivi karibuni, aliyoyafanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya Baraza lake la Mawaziri.

Akitoa Salamu zake mbele ya Ujumbe huo, Mhe.Othman amesema ni vyema kwa Taifa kutumia fursa zilizopo katika Muunganiko wa Afrika Mashariki, ili kujiimarisha kiuchumi.

Amesema, Afrika Mashariki siyo Jumuiya tu, bali ni shirikisho la kufungua fursa nyingi za kiuchumi ambazo zikitumika vyema, zitaleta tija kwa Taifa.

Aidha amewaelekeza Viongozi wanaosimamia Wizara hiyo, pia kuzitumia fursa zilizopo katika Taasisi za Kimataifa ili kuendana na kasi za kimaendeleo Ulimwenguni.

“Zipo Taasisi kama WIPO, zinazobeba fursa nyingi ndani yake, ambazo Mataifa ya Asia na Ulaya wanazitumia vilivyo kujinufaisha, ila kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla bado tupo nyuma sana; tukizingatia hili ni jambo adhimu kwa mustakbali wa maendeleo ya Nchi yetu”. Amesema Mhe. Othman.

Aidha Mhe.Othman amewahimiza wahusika na Watendaji wa Wizara hiyo kutoa elimu, kwa Jamii za Wazawa na hata Wageni, juu ya Mambo ya Msingi yanayoihusu Serikali ya Muungano, na yepi ya Zanzibar, ili kuondoa mkanganyiko, sambamba na kuwajengea uelewa mpana wananchi, katika, kuelewa haki zao, na pia maeneo sahihi ya kupata huduma kwa wakati.

Akieleza suala la Tija kupitia Sekta za Utalii, kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, Mheshimiwa Othman amehamasisha kuwepo kwa Kumbi za Mikutano zenye Hadhi ya Kimataifa, ili kuvutia Harakati za Mataifa ya Kigeni, kwa lengo pia la Kulinufaisha Taifa.

Hivyo, Mheshimiwa Othman ameridhishwa na Hatua ya Ujumbe huo, kufika na kubadilishana mawazo, huku akiahidi mashirikiano mema, kwa Maslahi ya Taifa.

Kwa upande wake, Waziri Mhe Balozi Kombo ameahidi kwamba Wizara yake hiyo mpya, itafanya kazi kwa karibu na Viongozi Wakuu, pamoja na Watendaji wote waliopo Zanzibar ili kuleta ufanisi, na kuhakikisha wanayafikia Malengo, kwaajili pia kuitangaza zaidi, Nchi katika Jamii ya Kimataifa.

Aidha, Mhe. Kombo ambaye ameshika Wadhifa huo hivi karibuni akitokea kuwa Balozi wa Tanzania Nchi Italia, ameahidi kuitendea kazi miongozo na mashauri yote aliyopewa, kwa Maslahi ya Taifa.

Aidha, Viongozi wengine waliohudhuria Mhe. Denis Lazaro; Mkurugenzi wa Mambo ya Nje Zanzibar, Balozi Silima Kombo Haji; pamoja na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Ilyasa Juma Pakacha.