Leo tarehe 20 Juni 2024, Phaustine Kasike, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji amekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mhandisi Ladislaus Matindi kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Shirika hilo (ATC House) zilizopo Mtaa wa Ohio, jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kuendelezwa ushirikiano uliopo baina ya Shirika hilo na Shirika la Ndege la Msumbiji (LAM).
Mhandisi Matindi ameeleza kwamba kwa sasa ATCL na LAM zinashirikiana kwa utaratibu wa kuwasafirisha abiria wanaotumia ndege za mashirika hayo (interlining).
Aidha, ameeleza kuwa kulingana na uwezo wa Shirika, hapo baadae ATCL itaangalia uwezekano wa kufikia makubaliano na LAM ili kuanza safari ya kwenda Msumbiji kwa lengo la kuimarisha zaidi ushirikiano huo.
Kwa upande wake, Mhe. Balozi Kasike alimuhakikishia Mhandisi Matindi kwamba Ubalozi wa Tanzania, Maputo utatoa kila aina ya ushirikiano kwa ATCL ili kuhakikisha shirika hilo linakamilisha mipango yake ya kuanza safari zake nchini Msumbiji hapo baadae.
Nchi za Tanzania na Msumbiji zina ushirikiano wa kidugu na kihistoria tangu wakati wa harakati za kupigania uhuru wa Msumbiji.
Ushirikiano huo unaendelezwa katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya uchumi.