Na Is-Haka Omar, Zanzibar

Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Kusini Unguja kwa kauli moja imemfukuza uanachama kada na mwanachama mkongwe wa chama hicho Ali Abeid Karume kutokana na mwenendo wake wa kukiuka maelekezo ya maadili, miongozo na nidhamu iliyoainishwa katika Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2022.

Akizungumza baada ya kutolewa maazimio ya kikao hicho Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa huo Ali Timamu Haji, amesema maamuzi hayo yamefikiwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2022 ibara ya 89 inayoeleza kazi za Halmashauri Kuu ya Mkoa inayoelekeza kuangalia mienendo ya wanachama na viongozi wa CCM wa ngazi ya mkoa kichama na kulazimika kutoa taarifa kwa vikao vinavyohusika ngazi za juu.

Pia Ibara ndogo ya 14 kifungu kidogo cha 14 inaelekeza kumuachisha au kumfukuza uanachama mwanachama yeyoye endapo itaridhika kwamba tabia na mwenendo wake vinamuondolea sifa za uanachama wake na mwanachama anayeachishwa au kufukuzwa uanachama anaweza kukata rufaa kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.

Katika maelezo yake Katibu wa Siasa na Uenezi huyo Ali Timamu, amefafanua kuwa baada ya kupewa nguvu na Katiba ya CCM na kujiridhisha kwa kina juu ya madai ya kukiuka maelekezo ya kikatiba  na kupitia mapendekezo yote yaliyopokelewa kutoka ngazi za Tawi, Wadi, Jimbo na Wilaya ambazo ni ngazi za chini za Mkoa huo Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa huo imeridhia na kuridhika kwamba kutokana na kauli na vitendo vya mwanachama huyo Ali Abeid Amani  Karume wamekubaliana kumuachisha uanachama wa CCM na kumtaka arudishe kadi ya uanachama wa CCM ya kielektroniki namba C000/2809/993/1 ya tarehe 17/03/2022.

“Mwanachama huyu ameitwa na kuonywa kwa maandishi na vikao mbalimbali vya Chama Cha Mapinduzi, lakini hakutii wala kubadilisha tabia na vitendo vyake, badala yake kuendelea kukiuka kwa makusudi maadili na miongozo ya CCM hivyo kwa mamlaka tuliyopewa na katiba yetu ngazi ya Mkoa ya CCM  Kusini Unguja kwa kauli moja tumefikia maamuzi, makubaliano kumuachisha na kumfukuza uanachama mwanachama huyo’’, amefafanua Katibu huyo wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja.

Mwanachama na mwanasiasa mkongwe aliyewahi kushika nafasi mbalimbali za Chama na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  zikiwemo Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya, Mkoa, Mwakilishi wa kuteuliwa, Waziri Mstaafu wa Mawasiliano, ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, Waziri wa Vijana na Michezo Zanzibar  pamoja na kuwa Balozi Mstaafu wa Tanzania mwaka 2006.

Maisha Yake Kisiasa Na Uongozi

Balozi Mstaafu Ali Abeid Karume alizaliwa May 24, 1950 ni mtoto wa kwanza wa Rais wa kwanza wa Zanzibar Mzee Abeid Amani Karume pia ni ndugu wa Rais mstaafu wa awamu ya sita wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

Mwaka 2005 na mwaka 2010 alijitosa kugombea uteuzi wa chama chake ili apeperushe bendera ya CCM kwa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini pia bahati haikuwa yake.

Uzoefu Wake
Akiwa na miaka 28 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri, Wizara ya Biashara na Viwanda katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kazi aliyoishikilia kwa miaka sita (1972 – 1978) alipoomba likizo na kwenda kujiendeleza zaidi kimasomo nchini Marekani.
Ali Karume alianza kufanya kazi za kibalozi mwaka 1989 alipokuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani.


Mwaka 1993 akawa Mkurugenzi wa Idara ya Masuala ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Tanzania hadi mwaka 1996 alipopelekwa Ubelgiji kuwa Balozi wa Tanzania kwa nchi za Ubelgiji, Uholanzi, Luxembourg na Umoja wa Ulaya.

Mwaka 2002 Ali akawa balozi wa Tanzania katika nchi za Ujerumani, Uswizi na Poland sambamba na kuangalia mahusiano na nchi za Australia, Jamhuri ya Chek, Slovakia, Hungary, Romania na Bulgaria.
Kuanzia mwaka 2006 Ali karume aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Balozi wa Tanzania katika nchi za Italia, Ugiriki, Uturuki na Malta. Pia amekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cyprus na Amidi Mkuu (Mkuu wa Mabalozi) wa Tanzania.