Kuna kila dalili kuwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada, Alphayo Kidata, atafikisha mahakamani Kisutu muda wowote kuanzia sasa kujibu tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka wakati akiwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), uchunguzi wa JAMHURI umebaini.
Kidata aliapishwa Mei 10, mwaka huu kwenda kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada, alikokwenda kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Balozi mstaafu, Jack Zoka, aliyehudumu katika nchi hiyo tangu Septemba 30, 2014 hadi muda wake ulipokwisha Machi, mwaka huu.
JAMHURI limepata taarifa zisizotiliwa shaka kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imekuwa ikifanya uchunguzi dhidi ya Kidata kuhusu matendo yake wakati akiwa Kamishna Mkuu wa TRA na Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
“Wasichojua baadhi ya viongozi wetu hawa ni kwamba tunawachunguza muda wote wanapokuwa madarakani na hata baada ya kutoka madarakani kuhakikisha hatumii vibaya madaraka yake. Wapo wengi tunaowachunguza, ila siku za nyuma mfumo ulikuwa umepigwa ganzi, lakini sasa unafanya kazi.
“Serikali ya Awamu ya Tano inahimiza utawala wa sheria. Kwamba kila kitendo unachofanya kama kiongozi, lazima ukipime iwapo kina masilahi ya taifa au ni masilahi yako binafsi. Wanapaswa kufahamu kuwa ni lazima kila kiongozi awajibike kwa matendo yake,” amesema mtoa taarifa wetu aliyepo ndani ya TAKUKURU.
Chanzo cha kuaminika kimeliambia JAMHURI kuwa Kidata ambaye Novemba 8, 2018 mamlaka ya uteuzi imetengua uteuzi wake na wadhifa wa ubalozi, kuwa uchunguzi huo umechukua muda mrefu na sasa umefikia hatua ambayo “hakuna namna” zaidi ya mtuhumiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma.
“Unajua wakati akiwa Kamishna Mkuu wa TRA alifanya mambo ya hovyo mpaka Rais Dk. John Magufuli akaamua kumwondoa pale na kumpeleka Ikulu kuwa Katibu Mkuu, akidhani atajirekebisha. Baadaye akaona ampe nafasi nyingine akampeleka ubalozini Canada.
“Ninafahamu kwamba Kidata amekuwa anachunguzwa na TAKUKURU kwa tuhuma kadhaa, ikiwemo ile ya matumizi mabaya ya madaraka. Kitendo cha Rais Magufuli kumvua nyadhifa zote ikiwemo ya Ubalozi, kuna jambo linakuja,” kimesema chanzo chetu.
Sambamba na suala la matumizi mabaya ya madaraka, chanzo chetu kimesema jambo jingine lililochangia kurejeshwa nyumbani kwa Kidata na kuvuliwa hadhi ya Ubalozi ni pamoja na kushindwa kuendana na kasi na matarajio ya nchi kutoka kwake.
“Unajua pale Canada ndipo zinatengenezwa ndege zetu na Kampuni ya Bombardier. Tangu alipoondoka yule balozi mwingine mambo yamekuwa yanasuasua… hilo nadhani pia halikuwafurahisha wakubwa. Maana zile ndege nyingine zilitakiwa ziwe zimekuja na kiungo hapo ni balozi.
“Ninafahamu kwamba Kidata sasa anafunga mizigo yake ili kurejea nyumbani. Akisharejea kila kitu kitakuwa bayana… kama kutakuwa na kupelekwa mahakamani,” kimesema chanzo kingine.
Jitihada za Gazeti la JAMHURI kuwapata viongozi wa TAKUKURU kuzungumzia kuhusu kuchunguzwa kwa Kidata hazikufanikiwa. Wakati huo huo, jitihada za kumpata Kidata kutoa ufafanuzi juu ya shutuma dhidi yake zinaendelea, maana alipotafutwa nyumbani kwake Canada juzi na jana hakupatikana.
Kidata aliyeteuliwa Januari, 10 kuwa Balozi, awali Machi, 2016, Rais Magufuli alimteua kuwa Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na baadaye kumthibitisha katika wadhifa huo.
Kabla ya uteuzi huo, Kidata alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, nafasi aliyoishikilia tangu Agosti, 2013.
Kidata hapa napo anakabiliwa na tuhuma nyingine. Inaelezwa kuwa wakati akiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alijiuzia shangingi lililopata ajali ndogo kwa bei ya kutupa. Shangingi hilo lilikuwa linatumiwa na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka.
“Mimi nilijua tu kuwa huu msala utabumburuka siku moja. Serikali ya Awamu ya Tano si mchezo. Unajiuzia gari lenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 150 kwa Sh milioni 17? Alipaswa kujiuliza, hivi siku Mthamini wa Serikali akiangalia kiwango lilichoharibika gari na muda lililotumika vikawa haviendani na bei uliyolipa si unaingia matatani?
“Pale TRA wanasema yale makontena yaliyokuwa na mashangingi na Range Rover nayo yanamhusu. Jamani, tukipewa nafasi tujiangalie. Tujue kuna leo na kesho. Nafahamu kuna aliowakwaza watashangilia na kuona malipo ni hapa hapa duniani, lakini yanayokwenda kumkuta yanasikitisha,” kilisema chanzo kingine.
Machi 23, 2017 aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu (Ikulu) akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Peter Ilomo, ambaye alistaafu. Alidumu katika nafasi hiyo hadi Januari 10, alipoteuliwa kuwa Balozi.
Ibara ya 31 ya Mkataba wa Vienna unaohusu uhusiano ya kidiplomasia (VCDR-1961) inaeleza hivi; Balozi atakuwa na kinga dhidi ya mashtaka yote ya jinai katika nchi iliyompokea (Receiving State).
Pia, Balozi atakuwa na kinga dhidi ya mashtaka ya madai ama ya kiutawala katika nchi hiyo anayofanyia kazi isipokuwa kwa:
(a) Suala linalohusu mali binafsi ya Balozi isiyohamishika ambayo ipo ndani ya mipaka ya nchi iliyompokea (Receiving State). Isipokuwa kama Balozi ataishikilia mali hiyo kwa niaba ya nchi iliyomtuma (Sending State) kwa malengo ya ubalozi.
(b) Jambo linalohusiana na Balozi kumiliki kutoka kwa mtu mwingine/Balozi ambalo ni la binafsi na halihusiani na nchi iliyomtuma. (c) Jambo linalohusiana na weledi au masuala ya biashara ambalo Balozi amelifanya nje ya majukumu yake ya kibalozi.
Kwa mujibu wa Ibara ya 36 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inasema Rais atakuwa na madaraka ya kuteua watu kushika nafasi za madaraka ya viongozi wanaowajibika kuweka sera za idara na taasisi za Serikali, na watendaji wakuu wanaowajibika kusimamia utekelezaji wa sera za idara na taasisi hizo katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, nafasi ambazo zimetajwa katika sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge kwamba zitajazwa na uteuzi unaofanywa na Rais.
Katika historia ya nchi hii, Kidata anakuwa Balozi wa pili kutenguliwa nafasi yake na kufikishwa mahakamani, baada ya Balozi Prof. Costa Ricky Mahalu kutenguliwa ubalozi na kufikishwa mahakamani Kisutu.
Prof. Mahalu aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, alitenguliwa ubalozi wake na kushtakiwa kwa tuhuma za kununua nyumba kwa bei isiyo na uhalisia, ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka.
Kesi ya Balozi Mahalu iliweka historia katika nchi ya Tanzania, kwani Rais (mstaafu) Benjamin Mkapa, alilazimika kupanda kizimbani kutoa ushahidi kuwa masuala yote aliyoyafanya Balozi Mahalu yalitokana na maelekezo yake.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 46 (2), Rais haruhusiwi kushtakiwa kwa jambo lolote alilolitenda akiwa madarakani, iwe ni jinai au madai. Kwa ibara hii, na baada ya Rais (mstaafu) Mkapa kutamka kuwa alimwagiza yeye kutenda yote aliyoyatenda, kesi ya Prof. Mahalu ilikufa kifo cha asili kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuwasilisha nia ya kutoendelea na kesi mahakamani (nolle presequi).
Ibara ya 46(2), inasema: “Wakati wote Rais atakapokuwa bado ameshika madaraka yake kwa mujibu wa Katiba hii, haitaruhusiwa kufungua mahakamani shauri kuhusu jambo lolote alilolitenda au alilokosa kulitenda yeye binafsi kama raia wa kawaida ama kabla au baada ya kushika madaraka ya Rais, ila tu kama angalau siku thelathini kabla ya shauri kufunguliwa mahakamani, Rais atapewa au ametumiwa taarifa ya madai kwa maandishi kwa kufuata utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge, na taarifa hiyo ikiwa inatoa maelezo kuhusu chanzo cha shauri hilo, kiini cha madai yenyewe, jina lake na anwani ya mahali anapoishi huyo mdai na jambo hasa analodai.”
Baadaye Rais Magufuli alimrejeshea hadhi ya Ubalozi Prof. Mahalu mwezi Machi mwaka huu. “Kwa Kidata, yajayo yanafurahisha. Hapa namuona akipambana na hali yake. Inasikitisha, ila kama alivyopata kusema Waziri Mkuu (mstaafu) Cleopa David Msuya; ‘kila mtu atabeba msalaba wake’,” kimesema chanzo chetu kingine.