Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),linaamini kuwa njia bora ya kupigania upatikanaji sheria rafiki kwa vyombo vya habari ni ya kidiplomasia.

Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa jukwaa hilo Deodatus Balile,
wakati wa mkutano wa mtandaoni (online meeting) uliofanyika leo Aprili 27,2023.

Akijibu swali la mhariri kutoka Sahara Media, Michael Noel aliyetaka kujua, iwapo mapendekezo yaliyotolewa na wadau wa habari na kuachwa, ni hatua gani wanahabari watachukua ambapo amesema kuwa TEF inaamini katika njia za kidiplomasia.

Balile amesema, Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI) walikutana na baadhi ya wabunge kwa ajili ya kuwaeleza umuhimu wa kujumuisha vipengele vilivyoachwa kwenye muswada wa habari, uliosomwa bungeni kwa mara ya kwanza tarehe 10 Februari 2023, na kwamba yapo mafanikio.

Baadhi ya wahariri wakijadili kuhusiana na mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari


“Tunaona kabisa kwamba kuna mabadiliko, lakini sisi kama TEF hoja ya kutumia nguvu hatujaifikiria na siyo sehemu ya mipango yetu, tunaamini katika diplomasia,” amesema Balile.

Kwenye mkutano huo, James Marenga ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa MISA TAN amesema, bado kuna changamoto inayohitaji kufanyiwa kazi.
Na kwamba, baadhi ya wabunge wanaelewa changamoto za vyombo vya habari hasa kupitia sheria iliyopo na wengine hawazifahamu kwa undani.

“Bado tunachangamoto sana ya kupata upimaji halisi, kwani kuna baadhi ya wabunge ambao wanaunga mkono hiki tunachokilalamikia juu ya kuwasilishwa bungeni kwa muswada wa habari ambao una mapungufu akiwamo.

“Miongoni mwa wanaounga mkono moja kwa moja ni Mbunge wa Viti Maalum, Salome Makamba ambaye alitaka kushikilia shilingi ya Waziri kwa serikali kupeleka sehemu ndogo ya muswada wa marekebisho ya sheria ya habari,” amesema.

Rashidi Kejo, mhariri kutoka Gazeti la Mwananchi ameshauri kutengenezwa vipande vipande vya sheria ilivyopendekezwa na vilivyopitishwa na kuvisambaza kwenye mitandao ya kijamii kwa ajili ya ufahamu zaidi.

James Marenga ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa MISA TAN

Jessy Kwayu kutoka Jarida la FAMA amesema, mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari hauishi kwa mara moja, ametaka kujua ni kwa asilimia ngapi harakati hizi zimefanikiwa mpaka sasa?

Hata hivyo mto mada, James Marenga ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa MISA TAN amesema, bado kuna changamoto ya kupata uhalisia kwa kuwa, baadhi waliokutana nao walionesha kuelewa na baadhi bado, na kwamba mwenedo mpaka sasa ni mzuri.

Peter Nyanje amewapongeza wajumbe wa CoRI kwa kiwango walichofikia kwenye mchakato wa Mabdiliko ya Sheria ya Habari na kuwataka wanahabari kuandika kwa ukubwa zaidi.

“Suala hili ni la kwetu lakini namna tunavyolichukuliwa si kwa umuhimu unaostahili, vyombo vya habari viandike kwa kiwango kikubwa kuhusu suala hili,” amesema.