Na Mwandishi Wetu,Jamhurimedia
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Deidatus Balile, amesema, licha ya kuwepo kwa uhuru wa habari nchini, ameomba uhuru huo ulindwe kisheria.
Akizungumza katika Kongamano la Kwanza la Maendeleo ya Sekta ya Habari leo tarehe 17 Desemba 2022, amesema, wadau wa habari nchini wanafurahia uhuru uliopo lakini haujalindwa kisheria.
“Wadau wa habari nchini wanafurahia uhuru wa habari uliopo nchini, tunaamini serikali italinda uhuru huu kisheria katika Mabadiliko ya Sheria ya Habari yajayo.
Kwenye mkutano huo Balile amesema, mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari yatafikishwa bungeni Januari 2022.
“Nimezungumza na Waziri Nape (Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) kuhusu mjadala wa Sheria ya Huduma za Habari, amesema Januari (2022) mapendekezo yatafikishwa bungeni,” amesema.
Akizungumzia madeni ya vyombo vya habari katika serikali na taasisi zake, Balile amesema licha ya juhudi kufanywa, bado taasisi za serikali ikiwemo halmashauri hasijalipa madeni yao kwa vyombo vya habari.
“Mpaka mwishoni mwa mwaka jana, madeni ambayo vyombo vya habari vinadai kwa serikali na taasisi zake ni Tsh. 7 bilioni.
“Ukijumuisha na deni la Gazeti la Daily News la serikali (Tsh. 11 Bilioni), jumla ya deni ni Tsh. 18 Bilioni na zaidi,” amesema.
“Halmashauri wana roho ngumu, hawajalipa mpaka leo licha ya kuandikiwa barua na TAMISEMI. Tunaomba mheshimiwa waziri (Nape) liwekee mguu chini, utusaidie,” amesema Balile.
Katika mapendekezo ya mabadiliko ya sheria, miongoni mwa mapendekezo ya wadau wa habari, ni kuweka sheria itakayowalazimisha watangazaji kwenye vyombo vya habari kulipa fedha ndani ya miezi sita baada ya matangazo yao kuchapishwa.
Miongoni mwa adhabu iliyopendekezwa iwapo mtangazaji atashindwa kulipa, walau kifungo cha miezi Sita.