Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema amefurahishwa na wahariri wenzake kumwamini baada ya kutokuwepo kwa mwanachama mwingine aliyejitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.

Akizungumza na Jamhuri Digital baada ya kurejesha fomu ya kugombea tena uenyekiti wa jukwaa hilo kwenye ofisi za jukwaa hilo.

Balile amesema kitendo hicho, kinaonyesha wazi kwamba wameridhika na utendajikazi wake katika kipindi chote alichohudumu.

‘’Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kufikia hatua hii, ni uwezo wake nawashukuru Wahariri na wenzangu, kwa heshima waliyompatia wameonyesha imani kwangu kwa kazi niliyofanya kwenye jukwaa wakati wote nikiwa kama Mwenyekiti wao hapa Tanzania.

Tutaendelea kushirikiana sote, Mungu atatupatia neema, na mwishowe mawazo yetu yatatimia kwa faida yetu na vizazi vijavyo vitakavyokuja katika sekta ya habari.

Kwa sasa, tunahitaji kutafakari jinsi tunavyo hudumia taaluma ya habari, kwa kuipa uhai, na kubadilisha mwelekeo wake.

Ni muhimu kutambua kwamba, vyombo vya habari havipaswi kila wakati kuonekana kama vinalia njaa kwa kukosa uwezo tunatakiwa kusimama imara kwa kuanzisha vyanzo vya mapato vitakavyotupatia fedha zetu wenyewe.

Wakati umefika sasa, kuimarisha ajenda ya uchumi wa vyombo vya habari na kuhakikisha uadilifu wa waandishi wa habari una imarika.

Pia hatupaswi kusahau, umuhimu wa maendeleo ya taaluma ya habari ikiwa tutakosa kuimarisha taaluma hii, vizazi vijavyo vitatukumbusha kwa kuchapa fimbo makaburi yetu.

Ili kufikia lengo hili, ni muhimu kujenga misingi ambayo itawapa watu uwezo wa kiuchumi, kitaaluma, na maarifa yatakayosaidia jamii.

Eckland Mwafisi mhariri Mtendaji Mkuu Tanzania leo, amesema kitendo cha baadhi ya wajumbe kutokuchukua fomu za kugombea nafasi ya mwenyekiti wa TEF kinaonyesha wazi kazi nzuri iliyofanywa na Deodatus Balile inakubalika.

Mwafisi amesema katika kipindi chake, amefanya kazi ya kipekee ambayo imeifanya taasisi hiyo kuwa na hadhi ya kitaifa na kimataifa, kutokana na juhudi zake katika kutekeleza kazi mbalimbali zilizofanywa na jukwaa hilo.

Amesema wajumbe wote kwa sasa, wana imani na ufanisi wa mwenyekiti, Balile, ambaye anakaribia kumaliza muda wake.

“Balile amekuwa kiongozi katika kipindi ambacho TEF haikuwa katika hali nzuri kiuchumi lakini aliweza kuinua na kufikia sehemu ilipo sasa.

Katika kipindi chote Balile, aliweza kufanya maendeleo makubwa ambayo yameifanya TEF kuwa maarufu kitaifa na kimataifa kama taasisi yenye nguvu nchini Tanzania. Hivi sasa, chini ya uongozi wake, TEF imeanza kuwekeza katika mali zake, ikiwa ni pamoja na kumiliki jengo lake la kisasa na la kibiashara.

Kwa msingi huu, TEF inatarajia kuendesha shughuli zake kwa kutumia mapato ya ndani, bila kutegemea wafadhili.

Haya ni mafanikio makubwa ambayo mwenyekiti ameyapata, na ndiyo sababu wajumbe watamchagua tena ili aendelee na uongozi wake na kuwafaidisha zaidi.