Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile, leo Machi 21, 2025 amechukua fomu ya kuwania uenyekiti wa jukwaa hilo na kuahidi kuleta mabadiliko katika sekta ya habari nchini.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Anita Mendoza akimkabidhi fomu ya kugombea uenyekiti, Deodatus Balile.

“Nilichaguliwa kipindi cha kwanza cha miaka minne na sasa nina waomba wahariri wenzangu kuwaongoza kwa kipindi kingine cha mwisho.

Uzoefu wangu wa miaka mingi kwenye sekta ya habari umenifanya nifahamu mbinu nyingi za kuikwamua sekta hii, hasa kwenye uchumi wa vyombo vya habari katika kipindi chenye changamoto nyingi ikiwamo za uwepo wa dijitali,”amesema.

Mkutano Mkuu Maalum wenye agenda moja ya uchaguzi mkuu utafanyika mjini Songea, mkoani Ruvuma na kuwaleta pamoja wahariri zaidi ya 150 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi.

Tayari wagombea 12 wamechukua fomu katika nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TEF na nafasi ya Makamu Mwenyekiti na Mwenyekiti zina mgombea mmoja mmoja ambapo mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu ni Machi 24, 2025.