Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limepewa changamoto ya kufuatilia taarifa zitolewazo na vyombo vya habari kujua kama maudhui halisi ya Uislamu, kudumisha amani na upendo yanaifikia jamii.
Changamoto hiyo imetolewa na mlezi wa Wanafunzi wa Jamii ya Kiislamu wanaosoma katika Chuo Kikuu cha Tanzania cha Mtakatifu Augustino-SAUT (SAMUCO), Altaf Hiran Mansoor maarufu kwa jina la ‘Dogo’ (pichani).
Mansoor alikuwa akizungumza katika harambee ya kuchangia Redio Iqraa, iliyofanyika wiki iliyopita kwenye ukumbi wa New Mwanza Hotel, jijini Mwanza.
Alisema baraza hilo linapaswa kujiwekea utaratibu wa kufuatilia matangazo na taarifa mbalimbali, kubaini kama maadili na miongozo ya dini hiyo inafuatwa kwani kufanya hivyo kutasaidia kuimarisha ushirikiano, upendo, utulivu na amani nchini.
“Kwa kuzingatia umuhimu na maadili ya dini ya Kiislamu katika jamii, upo umuhimu kwa Bakwata kuanza kufuatilia taarifa zote zinazotolewa kwenye vyombo vya habari ili kujua iwapo ujumbe halisi wa Kiislamu unaifikia jamii inavyotakiwa.
“Naamini kabisa iwapo Bakwata itafanya hivyo, itasaidia sana kuimarisha ushirikiano, maadili ya Uislamu pamoja na kujenga upendo, amani na utulivu katika nchi yetu,” alisema Mansoor ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya MOIL inayojishughulisha na biashara ya mafuta.
Alisema dini ya Kiislamu ni dira inayohusisha mambo ya kijamii, ikiwa ni pamoja na kumwezesha kila mtu kulinda heshima yake kama mwakilishi wa Mungu duniani.
Aidha, Mansoor aliwahimiza Waislamu na Watanzania kwa jumla, kuepuka jazba kwani nchi yetu inahitaji maendeleo na ushirikiano wa dhati bila kujali kabila, dini, rangi na sura.
Alitumia nafasi hiyo pia kuwakumbusha viongozi jukumu la kuhakikisha wanasimamia vizuri rasilimali za taifa kwa manufaa ya wote, kwani huo ndiyo wajibu na dhamana yao kwa jamii.
“Mafundisho ya Kiislamu ya sheria ya kidini yanahimiza maadili ya utawala kwa misingi ya uaminifu, uadilifu, haki na uwajibikaji. Pia, maandishi ya kidini yanawaonya watu na viongozi wenye kupenda rushwa na kuwadhulumu wengine,” alisisitiza Mansoor.
Mlezi huyo wa SAMUCO, aliwakumbusha walezi wa watoto yatima na wanyonge kuepuka kasumba ya kujitwalia mali za makundi hayo ya watu na kuzitumia kwa maslahi yao binafsi, badala yake waziendeleze kwa manufaa ya wanaowatunza.
Katika harambee hiyo, shilingi zaidi ya milioni sita zikiwamo fedha taslimu na ahadi, zilichangwa na watu mbalimbali, wakati Mansoor aliyekuwa mgeni rasmi alichangia Sh milioni 1.5 kuiwezesha Redio Iqraa kuimarisha matangazo yake kwa manufaa ya jamii kwa jumla.