“BAKWATA kwa niaba ya Waislamu wote, inalaani mauaji yote yanayotokea mkoani Pwani, na kutoa wito kwa Waislamu kukaa mbali na makundi yanayojihusisha na mauaji haya.
“Tumesikitishwa sana na vitendo hivi vyenye viashiria vya kutaka kuchafua sifa nzuri za nchi yetu kuwa ni kisiwa cha amani na tulivu. Na hasa pale inapohusishwa na dini ya Kiislamu. Uislamu ni dini ya amani, upendo kuvumiliana na kuishi pamoja na watu wa imani tofauti.”
Hiyo ni kauli iliyotolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Sheikh Salim Ahmed Abeid, kwa mgeni rasmi, Mh. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, katika Baraza la Idd el Fitr, lililofanyika katika Masjid Riadha, mjini Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, wiki iliyopita.
Kauli hiyo ina ujumbe mzito ambao hauna budi kutazamwa kwa makini na Watanzania hasa kwa watu tunaopenda amani na utulivu, kwani matendo haya yana dalili ya nchi kukumbwa na wimbi la kuvunja amani na utulivu na kuwaweka Watanzania katika maisha ya kutangatanga.

Mauaji ya mara kwa mara yanayotokea katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani Pwani, yanaleta woga na shaka kubwa kwa wakazi wa wilaya hizo na wasiwasi kwa sisi tunaoishi nje ya wilaya zilizotajwa.
Wenzetu katika maeneo hayo, ukweli wanasongwa na hali ngumu katika kutafuta riziki, kutembeleana na wanapata lepe la usingizi wakihofia kuuawa. Tulio nje ya wilaya hizo tunajenga hoja na maswali mbalimbali yenye msingi, kulikoni?
Nini kiini cha mauaji? Ni nani wanaofanya mauaji? Nini hatima ya mauaji hayo? Maswali hayo na mengine mengi yanatengenezwa hapa na pale ndani ya vichwa vya Watanzania wenye mazoea ya kuishi kwa amani na utulivu katika shughuli zao za kila siku.
Ilani ya Serikali kuhusu mauaji na mapambano ya Jeshi la Polisi dhidi ya wauaji yana hitaji zaidi nguvu na mbinu za wananchi nchini kote kuwa mstari wa mbele pamoja na vyombo hivyo kuzuia mauaji.

Kwa viongozi wa dini nchini, nguvu na ushawishi wenu wa kiroho unahitajika mno kuamsha na kuwaelekeza waumini wenu kuwa askari wazalendo wanaoipenda nchi yetu na kuwa tayari kufa kwa ajili ya nchi hii. Aidha, viongozi wa siasa kuwashtua wananchi kutambua faida ya kuwa askari mzalendo na hasara ya kuwa askari wa fedha (mercenary) na kuelewa siasa ya nchi yetu.
Pili, “Uislamu ni dini ya amani, upendo, kuvumiliana na kuishi pamoja na watu wa imani tofauti.” Kauli hii ya BAKWATA inaelekezwa kwa baadhi ya watu wanaoamini mauaji yanayotokea mkoani Pwani au duniani yana mkono wa Uislamu. Si imani sahihi.
Ni dhana potovu na yenye kudhalilisha dini ya kweli.  Hakuna dini ya Mwenyezi Mungu inayoelekeza waumini wake kuua mtu. Ni busara kwa Watanzania kusoma na kukariri vitabu na maelekezo ya Mwenyezi Mungu yenye kumuamrisha mwanadamu kutenda mema hapa duniani.

Hekima itumike katika kutoa na kupokea mafunzo ya imani ya dini tofauti, kuepuka chuki, fujo na mauaji, badala ya baadhi ya watu kuelekeza kidole kwa dini fulani kwa kuzingatia dhana ya udhanifu ambayo kwayo inaweza kuleta songombingo nchini.
Watu wanaopenda kuvunja amani na utulivu wa watu wengine wana roho za kihayawani. Husukumwa na tamaa ya wivu na dharau ya kutomwogopa (kumcha) Mungu aliyemleta duniani kwenye starehe chache na za muda mfupi.
Ni vyema wananchi wenzangu tukaungana na BAKWATA kuacha kutumia udhanifu katika kuielezea na kuiunganisha dini ya Uislamu na matukio ya mauaji nchini au nje ya nchi. Wanaofanya udhanifu huo watakuwa hawautendei haki Uislamu.
Nakamilisha makala hii kwa kusema matendo mazuri au mabaya hayafanywi na dini yoyote ya kweli na ya Mwenyezi Mungu. Yanafanywa na nafsi ya mtu kutokana na tamaa ya mambo ya dunia. Kwa mantiki hii unaweza ukafukua makaburi kupata yakinifu.

 

DAR ES SALAAM
NA ANGALIENI MPENDU
SIMU: 0717 113542 au 0787 113542