πŸ“Œ Shilingi Bilioni 109.8 zatumika mwaka 2023/2024

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema kuwa, Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) itaendelea kuongeza bajeti kila mwaka ya matengenezo ya miundombinu ya umeme hadi changamoto ya kukatika umeme kutokana na uchakavu wa miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme itakapoisha kabisa.

Naibu Waziri Kapinga ameeleza hayo tarehe 23 Aprili 2024 Bungeni jijini Dodoma wakati akijbu swali la Mbunge wa Jimbo la Segerea, Mhe. Bonnah Kamoli aliyetaka kujua ni lini changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara itaisha nchini.

”Changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara nchini inatokana na uchakavu wa miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme, miundombinu hiyo inahitaji uwekezaji mkubwa sana hivyo Serikali kupitia TANESCO imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kukarabati miundombinu hii na kwa mwaka wa fedha 2023/24, Serikali kupitia TANESCO imetumia jumla ya shilingi 109,896,003,751 kwa ajili ya kuboresha miundombinu husika.” Amesema Mhe. Kapinga

Ameongeza kuwa, Serikali pia imetumia jumla ya shilingi 105,515,860,225 katika miradi ya kuimarisha nguvu ya umeme Tanzania (Voltage Improvement projects) na kwa sasa, TANESCO imeanza kutumia nguzo za zege ambazo zinadumu kwa muda mrefu zaidi.

Akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Mhe. Charles Kimei aliyetaka kujua lini umeme wa REA utafikishwa katika Kata zote Jimbo la Vunjo, Mhe. Kapinga amesema kuwa vijiji vyote 78 kwenye Kata 16 za Jimbo hilo vimesambaziwa umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na TANESCO.

Ameongeza kuwa, katika vitongoji 301 vya Jimbo hilo tayari vitongoji 260 vimepatiwa umeme na katika mwaka 2023/24, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini utapeleka umeme katika vitongoji 15 vya Jimbo la Vunjo na hivyo kusalia na vitongoji 26 ambavyo kazi ya kuvipelekea umeme itaendelea kuratibiwa na REA kulingana na upatikanaji wa fedha.