Nasikitika kusema bajeti imenikatisha tamaa. Najua watu wengi wamekwishaizungumzia, najua wengi wameisifia. Wamesifia fedha zilizotengwa kwa ajili ya maji, umeme na reli. Ila mimi nimesikitika. Nimesikitika si kwa sababu nyingine, bali kuona imekuwa bajeti ya mazoea.
Serikali yetu imesheheni watu wenye uvivu wa kufikiri. Wanashangilia bajeti ya maji na barabara, ambazo ni bajeti za matumizi kwa gharama ya kudumaza uchumi wa taifa letu. Fedha za matumizi ya maendeleo ni Sh milioni 5,674,034. Kati ya hizo Sh milioni 2,981,965 ni fedha za ndani na Sh milioni 2,692,069 zinategemea wafadhili. Bajeti Kuu ni Sh milioni 18,248,983.
Sitaki kukufanyia hesabu mpendwa msomaji, ila piga hesabu mwenye uone kiasi kilichosalia ukitoa fedha za maendeleo. Kiasi hiki ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Ukisikia matumizi ya kawaida ni kulipana posho, mishahara, matengenezo ya magari, ununuzi wa mafuta, takrima na mengine.
Sitanii, niliposikia bajeti ni siri kubwa nikawa na mawazo kuwa bajeti hii itakuwa ya kufufua uchumi. Waziri anatoa malengo kuwa uchumi utakua kwa asilimia 7 mwakani. Hii imenisikitisha. Uchumi hauwezi kukua kwa nchi kutofanya uwekezaji. Leo fedha tunazopeleka kwenye ujenzi wa barabara ni sawa na kuzitekeleza.
Barabara ya Kati kuanzia Morogoro hadi Dodoma imefikia ukomo. Kila baada ya miaka mitatu tunajenga barabara hii, tena kwa fedha za mikopo. Niliwahi kuliandika hili na sasa naomba kulirudia. Dili zinaua nchi hii. Wapo watu wamejipanga na wamekodoa macho kama kunguru kusubiri kutoa taifa letu. Huwezi kusema tunajiandaa kuondoka kwenye umasikini wakati huna mpango wa kuwekeza kwenye reli.
Mwaka 1906 Mjerumani alikamilisha ujenzi wa Reli ya Kati kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza. Mwaka 1914 Julai, Mjerumani huyo huyo alikamilisha ujenzi wa reli kutoka Tabora hadi Kigoma. Mjerumani alijenga Bandari ya Dar es Salaam na kuweka miundombinu ya reli. Kwamba treni ndiyo itoe makontena bandarini na kuyapeleka mikoani.
Sitanii, Mjerumani hakuwa mjinga. Nimepata fursa ya kuishi Ulaya. Ni sera ya mataifa ya Ulaya kuwa mizigo yote mikubwa lazima isafirishwe kwa treni. Malori yanayoharibu barabara yasingekuwapo kama bajeti hii ingetumika kujenga miundombinu ya reli. Kwa kuanzia nilitarajia kama kweli tumejipanga kujiondoa kwenye umasikini zingetengwa trilioni 3 kwa ajili ya kujenga reli ya kisasa.
Kwa wanaokumbuka Reli ya Kati ilikuwa inatumia umeme wa jua kwa ajili ya mawasiliano tangu miaka hiyo hadi sasa ilipotekelezwa. Tunalo jua la kutosha na teknolojia imeimarika sasa kuliko wakati wowote. Kama mwaka 1996 mkoloni aliweza kufikiri kutumia umeme wa jua kuendesha miundombinu ya reli, leo naamini tulipaswa kuwa tunatumia treni za umeme wa jua.
Sitanii, treni ya umeme ina uwezo wa kutoa kontena la mizigo Dar es Salaam hadi Kigoma kwa muda wa saa 6. Kwa kawaida treni za umeme zinatembea kasi ya kilomita 350 kwa saa na umbali kati ya Dar es Salaam na Kigoma ni kilomita 1,800. Hii maana yake ni nini? Maana yake hii ni kwamba treni ingekuwa inatoa mzigo Dar es Salaam asubuhi, inaufikisha Kigoma mchana, inapakia na kugeuza jioni inalala Dar es Salaam.
Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Julius Nyerere ilikuwa inafikiri. Ndiyo maana unakuta ilianzisha Bandari Kavu pale Isaka. Mizigo ilikuwa inatolewa Dar es Salaam kwa treni na kushushwa Isaka, kisha wenye mizigo wanakwenda kufanya taratibu za kulipia kodi na ushuru mbalimbali kisha kuondoa mizigo yao.
Leo, serikali yetu sikivu imeona busara ni mizigo yote kutengenezewa kitu kinachoitwa Bonded Warehouses. Makontena yanatolewa bandarini na kuhifadhiwa Temeke, Sinza na Buguruni kwenye vijumba vya watu binafsi. Hii ni akili gani? Tunawezaje kujishusha katika kufikiri kwa kiwango hiki? Hivi hatuoni kwa kila mtu kuwa na ICD yake tunatengeneza mwanya wa kodi za Serikali kuibwa?
Nimejaribu kufanya utafiti. Wakubwa hawaitaki reli. Ni ama wakubwa wenyewe au watoto wao wanamiliki malori ya kusafirisha mizigo. Wakati lori linafanya safari mbili kwa mwezi kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma na tena kwa kupeleka kontena moja au mawili, treni ingeweza kupeleka makontena 70 mpaka 100 kwa wakati mmoja na kufanya safari 30 kwa mwezi.
Sitanii, viongozi wetu wamejifungia kwenye boksi. Wanatafuta kinachoitwa comfort zone (mawindo rahisi). Leo badala ya kufikiri kuwa tungewekeza trilioni 3 kwenye treni tukasafirisha mizigo ya Rwanda, Burundi, Uganda, DRC, Zambia, Malawi na Zimbabwe tungeweza kupata fedha nyingi, wanafikiria kutoza asilimia 14.5 kwenye muda wa maongezi ya simu.
Viongozi wetu wanafikiria kuongeza Sh 50 kwenye miundombinu ya kupeleka umeme vijijini, badala ya kuweka digitali, kazi hii ikafanywa na watu binafsi. Nchi kama Uingereza haikuendelezwa na Serikali, kuna matajiri akina Rotterdam, Metcalf na wengine ambao wakati wa enclosure system katika Karne ya 11 Uingereza ilikuwa inaweka sera wezeshi matajiri wanajenga miudombinu.
Kwa mfano, ukiwezesha watu kujenga viwanda vijijini, kwa nia ya kuvutia masoko ni lazima watajenga barabara na kuvuta umeme kwenda kwenye viwanda vyao, ambapo kwa kufanya hivyo wananchi katika maeneo husika watafaidika mara mbili.
Moja, watapata ajira kwenye viwanda, pili viwanda vikivuta umeme ni lazima kote zinakopitia nyaya watahakikisha wananchi wanapata umeme. Kwa bahati mbaya Serikali yetu inataka kufanya kila kitu. Inataka yenyewe ipeleke umeme vijijini, itenge Sh bilioni 38 kwa ajili ya reli sawa na kumwekea mgonjwa dripu, lakini ikamue wananchi kupitia sigara, bia, soda na kuongeza ushuru wa magari.
Sijaona mpango mkakati wenye kuonesha kuwa Serikali itaanza kukusanya kodi kwenye kiwanda fulani ilichowezesha mwekezaji kukijenga au treni ya umeme itaanza kufanya kazi ndani ya miaka miwili au mitatu, tuanze kukusanya ushuru na kodi mbalimbali kutokana na uwekezaji huu.
Mimi najiuliza, sisi ni taifa la namna gani? Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati anazindua kiwanda cha saruji cha Dangote Mtwara, akatangaza kuwa yatakuwa yanaingia malori hadi 300 kwa siku. Nilisikitika na bado naendelea kusikitika.
Nikijaribu kuangalia mipango ya Serikali, uchumi wetu umejikita katika misingi ya matumizi na si uwekezaji wa kuvuna mbele ya safari. Hadithi zote zinazoelezwa tusipozibadili katika vitendo au tukapata viongozi waliojiandaa kuacha historia ya uwekezaji hapa nchini sawa na alivyofanya Mwalimu Nyerere kupitia mashirika ya umma, maendeleo tutayasikia kwenye bomba.
Kazi pekee inayopaswa kufanya Serikali yetu ni kutekeleza mpango wa mwaka 2004 ulioasisiwa na Rais Benjamin Mkapa. Serikali ipimie watu ardhi na kuwapatia hati za viwanja, kisha watu wahangaike wenyewe kupata mikopo na kufanya uwekezaji.
Serikali ikiwawezesha Watanzania, watajiwezesha kujenga viwanda, kufungua kampuni na kufanya biashara kisha watalipa kodi na wigo wa kodi ukipanuliwa tutaanza kutoa misaada hadi nchi kama Marekani kutokana na makusanyo makubwa.
Sitanii, Serikali yetu isipokubali kubadilika yenyewe kimawazo, sisi wananchi tutaibadilisha.