DAR ES SALAAM
NA FRANK CHRISTOPHER
Ikiwa ni bajeti ya tatu kwa Serikali ya Awamu ya Tano, bajeti ya mwaka 2018/2019 iliwasilishwa bungeni Juni 14, mwaka huu ikilenga vipaumbele mbalimbali na hasa katika ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda pamoja na sera za fedha na bajeti zinazokusudia kuimarisha ukusanyaji mapato na usimamizi wa matumizi ya Serikali. Ufuatao ni uchambuzi mfupi kuhusu bajeti hiyo:
Sura ya bajeti
Kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 Serikali inapanga kukusanya na kutumia Sh trilioni 32.48. Bajeti hii ni ongezeko la Sh bilioni 700 kutoka Sh trilioni 31.7 za mwaka jana. Ongezeko hili dogo linaendana na uhalisia kutokana na mazingira na kasi ya ukuaji uchumi na biashara iliyopo nchini kwa sasa na hali halisi ya utekelezaji wa bajeti zilizopita ambazo zimekuwa na ongezeko kubwa hasiloendana na uhalisia wa utekelezaji wake.
Shabaha na misingi ya uchumi jumla
Kutokana na kuwa na shabaha ya ukuaji uchumi kwa asilimia 7 kwa mwaka ujao wa fedha ni dhahiri kwamba uchumi wa taifa utaendelea kukua kwa kasi hii, hivyo kutofikia kiwango stahiki cha ukuaji wa angalau asilimia 8 ambacho ni kizuri zaidi kutupeleka katika uchumi wa kipato cha kati. Juhudi zaidi zinahitajika katika kuhimiza uwekezaji mkubwa zaidi katika uchumi wetu kama tuna dhamira ya dhati ya kufikia nchi ya kipato cha kati.
MAPATO YA KODI
Mapato ya ndani
Kwa mwaka 2018/2019, lengo la makusanyo ya mapato ya kodi ni Sh trilioni 18 ambalo ni sawa na ongezeko la Sh bilioni 900 kutoka Sh trilioni 17.1 ya mwaka 2017/2018. Lengo la mapato haya ya kodi linawakilisha asilimia 13.6 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na nchi nyingine kama Kenya ambayo mapato ya kodi yamefikia asilimia 20 ya Pato la Taifa. Licha ya kuwa na ufanisi mzuri wa makusanyo ya kodi kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, bado nchi yetu ina wigo mdogo wa utozaji kodi. Takwimu zinaonesha Tanzania ina walipakodi milioni 2.615 ambayo ni sawa na asilimia 4.7 ya idadi ya Watanzania wanaokadiriwa kufikia milioni 55.57 (Benki ya Dunia, 2018).
Na kutokana na takwimu hizi, juhudi zaidi zinatakiwa zifanyike kuongeza idadi ya walipakodi kwa sababu wengi wao bado hawajafikiwa. Na kwa lengo la mapato ya kodi linalofikia Sh trilioni 18, kufikiwa kwake inabidi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikusanye Sh trilioni 1.5 kila mwezi.
Hii siyo kazi ndogo. Na kutokana na bajeti hii, licha ya kutoa vivutio vya kikodi hasa katika uwekezaji kwenye sekta ya viwanda, bado tuna kazi kubwa ya kubuni vyanzo vipya vya mapato kwani katika bajeti hii, chanzo ambacho kimeonekana kuwa kipya ni kupata mitaji kwa kutumia vyeti vya dhamana za uwekezaji (Negotiable certificate of deposit), na mifuko ya uwekezaji ya pamoja (investment funds) katika masoko ya mitaji na dhamana huku vingine vikiwa ni vilevile kama misaada na mikopo nafuu, mauzo ya hati fungani na dhamana za Serikali, mikopo ya kibiashara, na tozo na ushuru katika bidhaa.
Ufanisi wa chanzo cha masoko ya mitaji na dhamana utategemea sera na mikakati ya Serikali na sekta binafsi kuvutia uwekezaji. Vilivyobaki vitategemea mipango ya kitaifa, kisekta na kimkakati iliyowekwa na Serikali katika utekelezaji wa bajeti yenyewe.
Misaada na mikopo nafuu
Kwa miaka miwili iliyopita chanzo hiki kimeonekana kuwa muhimu zaidi kuliko mikopo ya kibiashara ambayo licha ya kuipata imechelewa, ina riba kubwa na hata wakati mwingine Serikali ikisitisha ukopaji kutokana na hali ya soko la fedha kimataifa kuwa na riba kubwa isiyo himilivu kwa nchi kama Tanzania.
Mwaka wa fedha uliopita Serikali ilipata asilimia 47 ya lengo na kwa mwaka huu Serikali inapanga kupata kiasi cha Sh trilioni 2.68 ambazo ni sawa na asilimia 8.2 ya bajeti yote; jambo linaloashiria punguzo la Sh trilioni 1.29. Upungufu huu unatokana na uhalisia kwamba upatikanaji wa misaada na mikopo nafuu ya kibajeti umekuwa mgumu kwa nchi nyingi zinazoendelea pamoja na kubadilika kwa masharti ya wakopeshaji hasa kutokana na sera za ndani za serikali zao.
Pamoja na hayo, licha ya changamoto zilizopo, kama chanzo hiki kitaendelea kutumika kwa uangalifu, tutaweza kupata fedha za kutekeleza bajeti na kudhibiti kwa kiwango kikubwa kasi ya ukuaji wa deni la taifa.
Mikopo ya kibiashara
Kutokana na kupungua kwa misaada kwa kiasi kikubwa, nchi iliamua kutafuta mikopo ya kibiashara kutekeleza bajeti yake. Licha ya chanzo hiki kuigharimu Serikali hasa kwenye ulipaji wa mikopo, pia kimekuwa na ufanisi mdogo kwani mikopo mingi imekuwa ikichelewa sana kiasi cha kuzorotesha utekelezaji wa bajeti. Kwa mwaka 2017/2018 nchi ilipanga kupata Sh trilioni 1.59 kutoka katika chanzo hiki, lakini ni Sh trilioni 1.374 ndizo zilizotarajiwa kupokewa hadi mwisho wa mwaka wa fedha 2017/2018; sawa na asilimia 86.4 ya lengo.
Na, kwa mwaka 2018/2019 Serikali imepanga kupata Sh trilioni 3.11 kutoka katika chanzo hiki ambazo ni sawa na asilimia 9.5 ya bajeti ya mwaka huu; huku mikopo mingi ikitarajiwa kukopwa katika soko la ndani. Pamoja na matarajio tuliyonayo juu ya chanzo hiki, ni muhimu kwa sasa Serikali ifikirie vyanzo vingine vya mapato katika masoko ya mitaji na dhamana hasa kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kwani licha mikopo ya kibiashara kuigharimu Serikali, ufanisi wake umeendelea kupungua mwaka hadi mwaka na kuzorotesha maendeleo ya taifa.
Matumizi
Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imepanga kutumia Sh trilioni 32.45 huku Sh trilioni 17 ambazo ni sawa na asilimia 53 zitatumika katika kulipa mishahara na deni la Serikali. Asilimia 37 ya bajeti ambayo ni Sh trilioni 12.01 imeelekezwa katika matumizi ya maendeleo huku fedha za ndani zikiwa Sh trilioni 9.88; sawa na asilimia 82.2 ya bajeti ya maendeleo. Ukuaji wa deni la taifa huchangiwa zaidi na mikopo ya nje ambayo imekuwa na riba zisizo rafiki hasa kwa nchi zinazoendelea kama inavyoelezwa hapa chini:
Deni la Taifa
Licha ya vipimo vya kimataifa kutuonesha kwamba deni letu kwa sasa ni himilivu, wasiwasi umetawala zaidi kwa namna deni linavyoongezeka kwa kasi na hasa likichangiwa na deni la nje lililofikia Sh trilioni 35.72 (Machi 2018) ambalo huchangia asilimia 71.8 ya deni lote la taifa ikilinganishwa na Sh trilioni 30.8 (Machi 2017). Licha ya ukweli kwamba ongezeko hili ni kutokana na kupokewa kwa mikopo mipya ya kugharimia miradi ya maendeleo na malimbikizo ya riba, ongezeko la Sh trilioni 5 kwa mwaka mmoja ni tishio kwa uhimilivu wa deni la taifa hasa kutokana na ukweli kwamba haliendani na kasi ya ukuaji wa mapato ya ndani pamoja na ukuaji wa uchumi wa taifa. Na kama kasi hii isipodhibitiwa, ni dhahiri kwamba nchi yetu inaweza kutumbukia kwenye mgogoro wa madeni (debt crisis).
MAMBO MENGINE MUHIMU
Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo
Kutokana na kupungua kwa misaada na ushirikiano wa kibajeti, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wameamua kupitisha Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo (Development Cooperation Framework) ambao utakuwa chachu ya kuboresha uhusiano na ushirikiano wa maendeleo huku Serikali ikipewa jukumu la kuongoza michakato ya ushirikiano na kimkakati ya kitaifa. Hili ni jambo zuri kwa maslahi ya pande zote mbili na endapo ushirikiano huu utakuwa wa vitendo, ni dhahiri kwamba hata bajeti ya nchi itapata msukumo wa kipekee katika kutekeleza vipaumbele, shabaha na misingi ya uchumi jumla ya kitaifa na kuchochea maendeleo.
Akaunti Jumuifu ya Hazina (Treasury Single Account)
Kutokana na makubaliano ya nchi za Afrika Mashariki, Serikali inapendekeza kuanzisha akaunti hii kwa ajili ya kupokea fedha zote za Serikali pamoja na kufanya malipo yote ya Serikali. Suala hili lina faida na hasara. Faida itakayopatikana kutokana na azimio hili ni kuimarika kwa usimamizi wa fedha za Serikali. Lakini kwa upande mwingine, suala hili liangaliwe kwa mapana zaidi kwani bila umakini katika utekelezaji wake, mifuko mingi ya kisekta itachechemea kimapato hivyo kuhatarisha utekelezaji wa mikakati ya kisekta na hatimaye kupunguza kasi ya maendeleo ya nchi.
Matarajio na mwelekeo wa ukuaji uchumi
Kutokana na hatua mbalimbali za kikodi, na sera za fedha kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 hapana shaka kwamba uchumi wa nchi utaendelea kuimarika na kuchangiwa zaidi na sekta ya ujenzi, uchimbaji madini na mawe, usafirishaji na uhifadhi mizigo; huku sekta ya fedha ambayo imeendelea kuwa imara kutokana na kuimarika kwa amana na ukwasi katika mabenki pamoja na juhudi zinazoendelezwa na mabenki katika kuongeza kasi ya ukopaji kwa ajili ya shughuli za maendeleo hasa kwa sekta binafsi.
Changamoto
Utekelezaji wa bajeti hii utakumbwa na changamoto kadhaa ikiwamo wigo mdogo wa utozaji kodi, ukwepaji kodi, mazingira yasiyo rafiki na urasimu katika ukusanyaji na utozaji kodi, uchache wa mapato ya kodi, matumizi madogo ya mifumo ya kielektroniki katika kukusanya kodi (mfano EFD) sambamba na mchango mdogo wa mashirika ya umma katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali. Hatuna budi kuongeza juhudi ili kuyafikia malengo yetu makuu ya kimaendeleo kama taifa.
Mwandishi wa makala hii ya uchambuzi wa bajeti anapatikana kwa simu namba 0763-64 31 99