Moja ya mambo yanayotafuna weledi wa wabunge wengi ni ‘imani kivuli za kisiasa’ walizonazo kuhusu uungwaji mkono wao. Kupitia imani za namna hii utaona mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anaamini kuwa wananchi wote wa jimbo lake ni wana-CCM, au mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) anadhani kuwa wanajimbo wote ni wana-Chadema.
Imani hizi zinawafanya wabunge watoe michango bungeni inayowakilisha ajenda za vyama vyao kwa kivuli cha kutumwa na wananchi. Mbunge wa jimbo langu la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, mara baada ya kusomwa kwa bajeti aliitisha mkutano wa hadhara na kutueleza kuwa anataka tumwambie cha kusema bungeni kuhusu bajeti hiyo.
Ninamsifu kwa hekima na ukaribu wake kwetu sisi wananchi. Pamoja na hayo, kuna makosa kadhaa nilibaini. Kwanza, mkutano alioutumia kukusanya maoni ulikuwa ni wa kichama (Chadema); kitu kilicholeta maoni na sura ya Uchadema badala ya ujimbo. Pili, hakukuwa na mjadala wa kuichambua bajeti kwa maana ya kuonyesha mazuri na upungufu wake.
Tatu, msimamo wa mbunge wangu pamoja na viongozi wengine wa Chadema ulikuwa ni kukataa bajeti hiyo tangu siku iliposomwa. Kwa maana hiyo, mkutano aliouitisha ulikuwa ni kubariki msimamo wake na wa chama chake. Hulka za Uchadema na u-CCM ndizo ninazoendelea kuzishuhudia katika Bunge la bajeti linaloendelea.
Katika masuala ya nchi kuna mambo ambayo unapotaka kuyachambua au kuyaelewa, unahitaji ufahamu wa kiujumla (general knowledge), na yapo mambo yanayohitaji uelewa wa kitaalamu (professional knowledge). Bajeti ya nchi kwa asilimia kubwa inatawaliwa na masuala ya utaalamu wa kiuchumi, hivyo utaona kuwa ili mbunge amudu vizuri kuijadili anatakiwa angalau awe na ‘a, b, c’ za kiuchumi na aweke kando (ama apunguze) hisia, ushabiki/ unazi wa kisiasa.
Ukiisikiliza michango ya wabunge wengi utabaini kuwa wanatumia ‘general knowledge’, jambo linalosababisha wajikute ‘wanazungumzazungumza tu’ pasipo kuichimbua bajeti kwa kina. Kama alivyosema mbunge mmoja kuwa wabunge wengi wanaisoma bajeti nusu nusu; ndiyo maana wanajikuta hawafanyi uamuzi wa busara katika kuipinga au kuiunga mkono.
Inaonekana utamaduni wa uvivu wa kujisomea unaotuandama Watanzania wengi, pia unawatafuna hata wabunge wetu. Kwa mtazamo wangu, wabunge wanapaswa kuwa wasomaji wakubwa wa ripoti, taarifa na vitabu kwa maana kazi zao zinahitaji uelewa wa kitaalamu kinagaubaga katika maeneo mengi ya kiuchumi, kisheria, kibiashara, sayansi ya uongozi na mengine mengi.
Kuna nyimbo zimeendelea kusikika midomoni mwa wabunge wengi kuhusu kupunguza matumizi (wao wanasema yasiyo ya lazima) ya serikali, kudhibiti nidhamu ya matumizi ya bajeti na kuongeza mapato. Mambo haya yamekuwa yakijadiliwa kwa hisia za kipropaganda, kisiasa na kiushabiki pasipo kuainisha njia za kitaalamu za kuboresha bajeti husika au kuangalia vigezo vilivyoikwamisha iliyopita.
Kwenye uchumi mdogo ambao ni wa mtu mmoja mmoja (micro-economics), njia ya kumudu bajeti ni kupunguza matumizi, lakini kwenye uchumi mkubwa ambao ni wa mataifa (macro-economic) kupunguza matumizi si suluhu ya kumudu bajeti.
Kwenye uchumi wa kitaifa (national economy); matumizi ni njia mojawapo ya kuingiza fedha katika mzunguko na kumimina ajira mitaani. Matumizi haya kwa ujumla wake ni pamoja na mishahara, posho, marupurupu na miradi ya maendeleo.
Kuna jambo wanasiasa wanapotosha wananchi kutuaminisha kuwa matumizi ya kawaida (karibu trilioni 10) ni ‘dhambi’ katika uchumi. Jambo hili si sahihi kwa sababu katika kanuni na sayansi za kiuchumi, matumizi ya kawaida ni nyenzo ya kukuza uchumi hasa wa mtu mmoja mmoja (households economy).
Mathalani; katika bajeti ya nchi ukipunguza matumizi (yawe ya kawaida au ya maendeleo); mosi, unafanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei, lakini kwa wakati huo huo unazalisha tatizo la upungufu wa ajira. Nchi isiyo na viwanda kama Tanzania hali inakuwa mbaya zaidi kwa sababu fedha nyingi zinaondoka kwenda nje kwa bidhaa au huduma ambazo si za uzalishaji (non-productive products).
Ukisikiliza asilimia kubwa ya wabunge (iwe kwa kujua au kwa kupapasa), utabaini kuwa wanachangia mambo yanayoathiri uchumi mdogo. Ni kweli kwamba hatimaye tutataka kuona maisha ya mtu mmoja mmoja yakiwa bora, lakini kuwa bora huko ni matokeo ya bajeti ambayo msingi wake ni wa uchumi mkubwa.
Wabunge wanatakiwa waibane serikali, waipe ushauri na mbinu mwanana ili bajeti hii iwe na muunganiko mzuri na uchumi wa mtu mmoja mmoja. Tumesikia wabunge wengi wanalia kuona asilimia iliyotengwa kwa ajili ya maendeleo imekuwa 30 badala ya 35 iliyotazamiwa.
Kimsingi unapotenga fedha za miradi ya maendeleo kuna milinganyo unayotakiwa uiangalie. Je, mapato yaliyokusudiwa kukusanywa yamerandana kiasi gani na yaliyokusanywa? Kuna uwiano gani kati ya bidhaa zilizoingia nchini na zile zilizopelekwa nje ya nchi? (exim-trade balance). Je, bajeti ya mwaka uliopita imechangia vipi kutengeneza ajira na kupambana na mfumuko wa bei?
Kanuni za uchumi zinabaki kuwa kanuni za uchumi hata kama kuna matamko ya kisiasa. Kusema kuwa bajeti ya maendeleo ingekuwa asilimia 35 mwaka huu ni jambo moja, lakini uhalisia wa milinganyo ya kiuchumi ni jambo jingine kabisa. Kitu wabunge wanachotakiwa kutusaidia wananchi ni kutazama kwa nini milinganyo ya kiuchumi haikwenda kama ilivyotazamiwa?
Wasiishie kulalamika, badala yake waieleze serikali ni nini ifanye ili kurekebisha milinganyo ya kiuchumi ambayo hatimaye itazaa matokeo yatakayoathiri kipato cha mtu mmoja mmoja. Na pale Serikali inapokwama kutekeleza ahadi zake waisaidie kutathmini sababu za ndani na za nje (local and global factors) na kutafuta ufumbuzi.
Ninachoshuhudia sasa hata Serikali inapokwama kwa uhalisia, wabunge wanatumia mwanya huo kuigongomea msalabani. Mtindo huu wa kuisulubu Serikali hata kwa mambo yenye uhalisia unaweza kuonekana ukiwanufaisha wapinzani. Lakini utamaduni huu wa mijadala ya bungeni kushindwa kuisaidia Serikali utaendelea kuwatesa hata wapinzani siku wakiingia madarakani.
Ndiyo maana kuna haja wabunge wetu waongeze weledi na uzalendo. Kuna mambo mbunge akizungumza (tena akachanganya na hisia kali), yanaonekana kuwa na maana kubwa. Kwa mfano, wabunge wengi wanazungumzia ukosefu wa ajira hasa kwa vijana, lakini ni wachache wanaoshauri mbinu za kitaalamu (ambazo Serikali imezisahau au haizijui) kuhusu utatuzi wa tatizo hili.
Kama taifa, tumepungukiwa na busara ya ufahamu kwa sababu wabunge wanaozungumza sana ndiyo tunaowahesabu kuwa ‘machachari’. Wabunge wanaolalamika sana tunaona ndiyo wenye uchungu na nchi hii. Na sasa hivi kule bungeni kumezuka makundi matatu mapya ya wabunge.
Kuna wabunge ambao huzusha vijembe, kuna wale ambao huamua kujibu mapigo ya vijembe, na kuna kundi la tatu ambalo ni wasuluhishi.
Dakika 10 zote mbunge anasimama kuelezea namna ya kuvumiliana, kutumia busara baina ya wabunge wa chama tawala na wale wa upinzani. Ni mwendo wa vijembe na usuluhishi wakati mambo ya msingi yakiwekwa kando.
Wabunge wengi katika akili na fahamu zao wanadhani wanachambua bajeti, lakini kiukweli wanachambua ajenda za mikutano ya vyama vyao vya siasa, wanapiga kampeni; na sehemu kubwa wanatafuta umaarufu ‘potential popularity’. Hakuna anayependa ufisadi, lakini bajeti ya nchi ni zaidi ya ufisadi.
Misamaha ya kodi ni kweli inatakiwa kupunguzwa, lakini bajeti ya nchi ni zaidi ya misamaha ya kodi. Wabunge wasiishie kulalamika ukubwa wa misamaha ya kodi iliyotolewa mwaka uliopita, bali watueleze pia namna misamaha hiyo ilivyosaidia kutengeneza ajira, kudhibiti bei na kuimarisha ugavi.
Tunachoaminishwa Watanzania wengi kwa sasa ni kwamba misamaha ya kodi haina umuhimu hata kidogo kwa ustawi wa nchi, kitu ambacho si kweli kiuchumi. Wabunge wawe weledi na wawazi zaidi. Wanachotakiwa kutusaidia ni kuielekeza Serikali iwe na msawazo katika misamaha hiyo (balanced tax breaks). Misamaha isipungue wala kuzidi sana kiwango stahidi (green line tax index)
Ni vema wabunge waitazame bajeti, majedwali, vielelezo na takwimu waelewe kipimo cha bei (consumer price index) kirekebishwe vipi, ili riba katika mabenki zipungue (lending rate) ambako itakuwa ni msaada kwa wajasiriamali na ajira zitaongezeka. Waieleze Serikali namna ya kukusanya mapato ambayo haitasababisha kushuka kwa uzalishaji.
Vile vile ninatamani wabunge wajiepushe na mitego ya kuwachukia wawekezaji wa nje (hasa kwenye madini na maliasili), kwa kuwakomalia waongezewe kodi. Wabunge wanapaswa kung’amua kuwa wawekezaji wa nje ni zao la uwekezaji wa moja kwa moja (foreign direct investments) ambao ni bawa la kurusha uchumi kwa maana ya ‘aggregate money supply’.
Mbunge asikae kulilia barabara yake ijengwe ikiwa ujenzi wa barabara hiyo unaweza kuzalisha ‘inflation’, kwa mujibu wa kanuni za umiminaji wa fedha (money injection). Ni vema wabunge wakayajua mambo haya ili wasitupotoshe.
Unapoona wabunge ‘wamekomaa’ kuchambua mambo mawili matatu pekee kama ufisadi, misamaha ya kodi au ‘hapa na pale’, basi unatambua kabisa kuwa watu hawa hawajui walitendalo. Kama si hivyo, basi huenda wanakuwa na ajenda nyingine zaidi ya kujadili bajeti.
Wabunge tumewatuma mtusaidie, changamkeni.
0719 127 901, [email protected]