*Wananchi waomba kodi ya kichwa isirejeshwe

DAR ES SLAAM

Na Mwandishi Wetu

Bajeti Kuu ya Serikali iliyosomwa bungeni jijini Dodoma wiki iliyopita imezua mjadala karibu kila kona ya nchi, ikipongezwa katika maeneo mengi, lakini pia serikali ikiombwa kutoa ufafanuzi hapa na pale huku ikitajwa kutokuwa tofauti na bajeti nyingi zilizopita.

Gumzo kubwa katika bajeti ya mwaka huu; ya kwanza kuandaliwa kikamilifu na Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan, iliyosomwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, ni kodi kwa kila mtu mwenye umri wa miaka 18.

Lakini kwa upande mwingine, Bajeti Kuu ya Serikali 2022/23 inatajwa kuendeleza utamaduni wa miaka mingi wa kusomwa bajeti za kuvutia lakini hakuna utekelezaji stahiki.

Akizungumza na JAMHURI, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) cha jijini Mwanza, Dk. Ntui Ponsian, amesema imekuwa ni kawaida kwa bajeti kuwatia matumaini wananchi.

“Bajeti zetu huwa ni za kisiasa. Ukizisikiliza utadhani kuna kitu kizuri kabisa kinakuja, na kikija itakuwa vema, lakini hakuna kitu. Kwa bajeti ya mwaka huu, kama unanitaka nitoe ‘marks’ (alama), mimi ninaipa ‘wastani’,” anasema Dk. Ponsian.

Mhadhiri huyo anasema katika kuitazama bajeti lazima kutathmini masuala kadhaa muhimu kama uwiano wa ukuaji wa deni la taifa (la serikali) na ukuaji wa uchumi.

Dk. Ponsian anaonyesha shaka kuwa ukuaji wa deni la taifa kwa wastani wa asilimia 14 kwa mwaka kutoka Sh trilioni 60 hadi Sh trilioni 69, hauna uwiano mzuri na ukuaji wa uchumi wa wastani wa asilimia 4.9.

“Sisemi kwamba tusikope, hapana. Ila naona kuna tatizo kwenye matumizi ya fedha. Tukope huku tukijiuliza uwiano ukoje ili tusijekushindwa kulipa,” anasema.

Hofu yake inajikita katika hoja kwamba kwa mujibu wa bajeti, ukuaji wa uchumi wa ndani unakadiriwa kuwa asilimia 8 wakati deni likikua kwa asilimia 14.

Ni Bajeti ya Sh trilioni 20

Pamoja na kuipongeza serikali kwa kupunguza kodi kwa bidhaa zinazozalishwa nchini, Dk. Ponsian anataja mambo mawili ya lazima kufanyika; kulipa mishahara na madeni.

Anasema zaidi ya asilimia 51 ya bajeti ya mwaka huu imeelekezwa katika maeneo hayo mawili na kwamba: “Katika haya hakuna ‘adjustment’. Lazima yatekelezwe. Kwa hiyo ukitoa asilimia 51 ya Sh trilioni 41 za bajeti hii, utabaki na Sh trilioni 20 tu. Sasa maana yake tujipange kwa matumizi ya fedha hizo.”

Dk. Ponsian anashauri kama taifa linapaswa kuwa na vipaumbele vichache vinavyotekelezeka ndani ya mwaka mmoja na serikali ipimwe kwa utekelezaji wake badala ya kuwa na vipaumbele vingi ili kuwatia tamaa wananchi.

Hofu kurejea kodi ya kichwa

Pamoja na ufafanuzi uliotolewa na serikali, bado Watanzania kadhaa wameonyesha hofu juu ya utekelezaji wa ukusanyaji kodi kwa kupitia namba ya TIN.

Mwanahabari mstaafu, Frida Keyssi, ameliambia JAMHURI kuwa bajeti imegusa karibu kila eneo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

“Lakini huu ulipaji kodi kupitia TIN namba, unanitia shaka, hasa kwa vijana. Kwa kusema ukweli miaka 18 huyu ni mtoto tu na wengi ama wapo shuleni au bado wanawategemea wazazi wao. 

“Kumlipisha kodi mtoto huyu si sahihi. Ninaona hii ni sawa na kurejesha tena ‘kodi ya kichwa’ iliyowatesa wanaume wengi miaka ya nyuma,” anasema Frida.

Kodi ya kichwa ni miongoni mwa kero zilizofutwa na serikali miaka ya 1990 baada ya kulalamikiwa na wananchi kuwa ni ya kidhalilishaji.

Frida anasema si kwamba itawaumiza vijana tu, lakini pia itaongeza mzigo kwa walezi wao kwa kuwa hata waliopo kwenye ajira huwa ni zile zisizo rasmi.

Kauli ya Frida inaungwa mkono na mwanaharakati, Leila Sheikh, anayeiomba serikali kutafuta namna nyingine ya kupanua wigo wa ukusanyaji kodi bila kutesa wananchi.

“Kuwa na namba ya TIN si vibaya kwa wenye biashara ndogondogo kulingana na kipato chao, lakini hapa kwetu vijana hawa bado wako shuleni tofauti na kwa wenzetu,” anasema Leila.

Anasema wazazi wengi wa vijana hawa ni ama wakulima au wafanyabiashara wadogo ambao kuwaongezea mzigo si sahihi. 

Akizungumzia suala hilo, wakili wa kujitegemea ambaye pia ni mchumi, Everest Mnyele, anawaomba wananchi kutotishika na kodi hii itakayokusanywa kupitia namba ya TIN.

“Kuwa na TIN si lazima ulipe kodi. Ni utambulisho tu na kwa kweli tumechelewa sana katika hili. Wenzetu wameanza hivi zamani sana. Mfanyakazi lazima awe na namba ya TIN na kodi anayolipa ni PAYE.

“Kwa mwanafunzi naye anapoomba mkopo wa elimu ya juu utaulizwa iwapo ana namba ya TIN. Kwa hiyo hii si kodi ya kichwa,” anasema Mnyele.

Mchumi huyo ambaye ni Meneja (mstaafu) wa Benki ya CRDB, anasema ingawa haina tofauti sana na bajeti za miaka mingine, bado bajeti ya 2022/23 imejitahidi kugusa maeneo nyeti katika kuinua uchumi wa ndani.

Anatoa mfano wa kupunguzwa kwa kodi za bidhaa nyingi zinazozalishwa nchini, akisema kutakuza viwanda vya ndani na hasa vya mafuta ya kula.

“Ni bajeti ya wananchi. Imegusa maisha ya mwananchi wa kawaida kabisa, kwa mfano, kwa kutoa elimu bure hadi kidato cha sita; kutenga Sh bilioni 8 kwa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu. Hiki ni kitu kipya kabisa.

“Lakini hata kuongeza bajeti ya TASAF kunawagusa maskini wengi wa Tanzania,” anasema Mnyele huku pia akipongeza hatua ya kuweka kodi kwenye nywele bandia za akina mama, akisema nyingi zina madhara kwa afya.