DAR ES SALAAM

Na Waandishi Wetu

Wachambuzi wa masuala ya uchumi nchini wameunga mkono bajeti iliyosomwa bungeni wiki iliyopita, ila wameeleza maeneo yanayohitaji ufafanuzi ili kuondoa wasiwasi wa wananchi.

Wamezungumzia hoja ya serikali kutaka ipanue wigo wa ukusanyaji kodi. Profesa Honest Ngowi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Kampasi ya Dar es Salaam anaamini zipo dalili njema katika hilo, akitolea mfano wa tozo kadhaa zilizoingizwa kwenye mafuta na miamala ya simu.

“Ingawa bado wigo ni finyu, kuna dalili kwamba tutafika tunakotaka. Kushirikisha sekta binafsi husaidia katika kupanua wigo wa kodi,” anasema Profesa Ngowi.

Anatoa mfano wa ujenzi wa miundombinu kwa njia ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) kama moja ya njia sahihi za kupanua wigo wa kodi.

Profesa Ngowi anasema mapendekezo yaliyomo katika bajeti ya mwaka huu kuhusu uuzwaji wa hati fungani za halmashauri, iwapo mpango huu utakwenda vizuri, utasaidia kupanua wigo wa kodi.

“Lakini mbinu sahihi zaidi ni kujenga mazingira mazuri ya biashara ili uwekezaji uongezeke. Wawekezaji wakiwa wengi, ajira zitaongezeka sambamba na wigo wa ukusanyaji kodi,” anasema Profesa Ngowi.

Akizungumzia suala hilo, Wakili Everest Mnyele anasema kwa kawaida kodi au tozo zinazolipwa ‘indirectly’ huwa hazimuumizi anayetozwa.

“Kodi kwenye miamala ni njia mpya hii. Ni kupanua wigo wa kodi na ni suala sahihi kwa mtazamo wangu.

“Sasa wananchi wanachotaka kukiona ni matokeo ya kodi walizokatwa. Kama Mwigulu anasema Sh bilioni 360 zitakazokusanywa kutokana na miamala ya simu zitajenga hospitali na zahanati; basi mwakani aje kutuambia zahanati ngapi zimejengwa.

“Hilo litawatia moyo walipa kodi na kuondoa malalamiko. Kama Sh 100 zimeongezwa kama tozo kwenye kila lita ya mafuta kwa ajili ya kuwapa fedha TARURA, ni jambo jema na halimuumizi mlipa kodi, kwa kuwa halina ‘pinch’, tofauti na kugongewa mlango ukidaiwa kodi ya kichwa,” anasema wakili huyo ambaye amewahi kuwa Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Tanga.

Anasema iwapo TARURA watatumia fedha hizo kupeleka barabara kila kijiji cha Tanzania, maana yake kazi na shughuli za kibiashara vijijini zitaongezeka na hii miaka michache ijayo itaongeza wigo wa walipa kodi.

Mwenyekiti wa Chama cha ADC, Hamad Rashid Mohamed, anasema serikali ina nafasi kubwa zaidi katika kupanua wigo wa ukusanyaji kodi kama itawekeza baharini.

“Huko kwenye ‘blue economy’ (uchumi wa bluu) kunapaswa kupewa umuhimu wa hali ya juu kuweza kuwa chanzo kikuu cha mapato nchini,” anasema Hamad.

Anashauri serikali kuwapa mafunzo maalumu watoto wa wavuvi wa sasa wanaotamani kuendeleza kazi za baba zao, wapelekwe kwenye vyuo mbalimbali kupata mafunzo ya uvuvi wa kisasa.

“Zanzibar kuna wavuvi kama 50,000 hivi wakati Bara kuna wavuvi 350,000 tu. Lakini uvuvi wao una tija gani?” anahoji.

Anatoa mfano wa mvuvi anayetumia hadi saa 10 baharini akiwa na zana duni za uvuvi, akisema hawezi kushindana na mvuvi wa Mauritius anayetumia saa tatu tu baharini na kurejea pwani akiwa na maelfu ya tani za samaki.

“Kuna vifaa vya kutazama samaki wapo wapi na ni wa aina gani. Wavuvi wetu wawezeshwe. Kwa mfano kilo moja ya jongoo huuzwa kwa dola za Marekani 250; lakini ni jongoo wa aina gani na wanauzwa wapi?” anasema.

Hamad anaamini kuwa iwapo uvuvi hasa wa bahari kuu (deep sea) utapewa kipaumbele, basi wigo wa kodi utaongezeka, lakini anasema ni lazima kwanza wananchi wapewe elimu kuhusu umuhimu wa kodi.

Mwanasiasa huyo mkongwe ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi anapendekeza Chuo cha Uvuvi Mbegani kiboreshwe na kuwa kitivo cha ‘blue economy’ kwa upande wa uvuvi.

Kwa upande wa Shaibu, anaamini kuwa bado serikali haijafanya ubunifu sahihi katika kupanua wigo wa ukusanyaji kodi.

“Hakuna vyanzo vipya. Anayetazamwa na kukamuliwa ni mwananchi wa hali ya chini. Kodi zote hizo utakuta anayelipa ni mwananchi wa kawaida wala si mfanyabiashara,” anasema Shaibu.

Hoja ya Shaibu inajibiwa na Wakili Mnyele akisema kwa kawaida wafanyabiashara na kampuni huwa ni kama mawakala wa ukusanyaji wa kodi; na ndiyo kazi itakayofanywa na kampuni za simu za mkononi.

“Hata sisi (wakati akiwa meneja wa benki) tunakusanya makato kutoka kwenye miamala ya wateja na kupeleka serikalini. Tunachokuja kulipa kama kampuni ni kodi ya mapato,” anasema.

Deni la taifa

Akizungumzia deni la taifa, Profesa Ngowi anasema kuendelea kukua kwa deni hilo si suala la ajabu, kwa kuwa taifa lina matumizi makubwa kuliko mapato.

Anasema kwa bahati nzuri hadi sasa deni hilo ni himilivu na ndiyo maana Tanzania inakopesheka.

“Issue (suala) kubwa hapa si deni, ila unakopa kwa ajili gani? Kama unakopa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kama vile kujenga miundombinu, basi deni hilo ni afya kwa taifa.

“Lakini iwapo unakopa kwa ajili ya posho za vikao na kununulia maandazi ofisini, hiyo ni mbaya sana,” anasema profesa.

Hata hivyo, anashauri umakini katika kuendelea kukopa na kulipa deni hilo ili taifa lisije kujikuta halikopesheki tena.

Profesa Ngowi amepongeza mpango wa serikali kuzileta nchini taasisi tatu za kimataifa kufanya utafiti na kuipa majibu kama bado Tanzania inakopesheka.

“Wakishakuja na kutufanyia ‘rating’ ndipo tutakapojua mbivu na mbichi na tutapata njia mpya ya kupanua miradi,” anasema.

Katika kuhakikisha deni la taifa linaendelea kuwa stamilivu, Profesa Ngowi anasema ni lazima makusanyo ya ndani yaimarishwe; lazima kuwepo rasilimali za ndani za kutosha.

Anashauri serikali kuwa makini katika kuchukua mikopo ya ndani na nje, akisisitiza kuwa iwapo itakopa ndani zaidi, kuna uwezekano wa kuminya nafasi ya sekta binafsi kukopeshwa na taasisi za fedha za ndani.

“Sasa sekta binafsi ikishindwa kupata sehemu ya kukopa ndani, itayumba na ajira kukosekana hivyo wigo wa kodi kupungua,” anasema.

Ushauri huo wa Profesa Ngowi ameujibu Rais Samia Suluhu Hassan katika hotuba aliyoitoa Juni 13, 2021 jijini Mwanza mwishoni mwa wiki.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini humo, Rais Samia anashauri kuwapo umakini kwa serikali katika mikopo ya ndani.

“Kama serikali itakopa zaidi kwenye benki za ndani kuna hatari ya taasisi hizo kutoikopesha sekta binafsi, kwa kuwa kupitia serikali wana uhakika wa kupata faida kubwa.

“Hii ni hatari, kwani itasababisha kuyumba kwa mitaji katika sekta binafasi,” anasema Samia.

Profesa Ngowi anakitaja chanzo kingine cha kukua kwa deni la taifa kuwa ni kushuka kwa thamani ya shilingi kulinganisha na dola ya Marekani; kwa kuwa deni hulipwa kwa thamani ya dola kwa wakati husika, hivyo zinahitajika pesa nyingi kulipa deni lililokopwa likiwa kidogo hivyo ni hatari shilingi kushuka thamani.

Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2021/22 iliyosomwa bungeni jijini Dodoma wiki iliyopita, imezua mijadala mbalimbali nchini, huku wachambuzi kadhaa wakitarajia serikali kutoa ufafanuzi wa ziada katika masuala kadhaa.

Katika mwaka wa fedha 2021/2022, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, amewasilisha mapendekezo ya mapato na matumizi ya serikali ya Sh trilioni 36.33.

Katika Bajeti hiyo, serikali imepanga kuboresha ukusanyaji wa kodi za majengo kwa kutumia mfumo wa mita za umeme za LUKU (lipia umeme kadiri unavyotumia), suala linalozua mkanganyiko kwa jamii.

Kodi ya majengo

Profesa Ngowi anaamini suala hilo litatolewa ufafanuzi lieleweke kwa wananchi.

“Katika masuala ya kodi sisi (wachumi) tuna kitu tunakiita ‘equity’, ambapo kodi inapaswa kutolewa kutoka kwenye kipato.

“Sasa mpangaji anapolipa kodi ya jengo ambalo yeye halimiliki, kidogo kuna mkanganyiko. Hebu tusubiri. Ninaamini hili serikali italifafanua,” anasema mchumi huyo mbobezi.

Katika hilo, Mwigulu anapendekeza kufanyike marekebisho ya sheria ya kodi ya majengo ili kiwango cha kati ya Sh 1,000 hadi Sh 5,000 kikatwe kila mwezi kupitia LUKU, suala ambalo Profesa Ngowi anadhani bado halijakaa sawa sawa.

Hoja hiyo inaungwa mkono na Wakili wa Kujitegemea, Everest Mnyele, akisema: “Halijaeleweka vizuri. Linahitaji ufafanuzi kwa kuwa ni watu wachache sana wanaokaa kwenye nyumba zao.

“Lakini, mtu hununua LUKU mara ngapi kwa mwezi? Wengine tunanunua kila siku. Makato yatafanyikaje?” anahoji Wakili Mnyele, akitaka pia kufahamu uhalali wa mpangaji kumlipia ‘tajiri’ (mwenye nyumba) kodi ya jengo.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, anatofautiana kidogo na wasomi hao, akisema uamuzi wa kukusanya kodi ya majengo kutumia LUKU ni ubunifu.

“Maana yake serikali itapata nafasi ya kukusanya kodi ndogondogo kutoka kwa watu wengi nchini tofauti na ilivyokuwa awali,” anasema Shaibu.

Hoja yake inajikita katika ukweli kwamba umeme kwa sasa umesambaa karibu katika vijiji vyote Tanzania Bara.

Tangu kuanza kwa utekelezaji wa sheria ndogo ya kodi ya majengo Julai 1, 2016, serikali imekuwa ikitafuta namna sahihi ya ukusanyaji wake, kazi hiyo ikihamishwa kutoka taasisi moja hadi nyingine.

Mtazamo wa bajeti kwa ujumla

Wakati Shaibu anaitazama bajeti hii kama iliyoandaliwa kumalizia miradi iliyoanzishwa katika Awamu ya Tano, Profesa Ngowi anasema: “Ni kama ambavyo waandishi wa habari mlivyoiita; ina uma na kupuliza.”

Profesa anasema kuna makundi yamenufaika huku mengine yakiwa yamepata maumivu.

“Kwa ujumla kuna nia ya kulinda viwanda vya ndani inayoonekana wazi. Hii ni nia njema. Kuna kodi zinazotozwa kwa bidhaa kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

“Wamepunguza kodi kwenye kilimo cha maua. Waajiri nao; wenye wafanyakazi hadi 10 hawawalipii kodi ya maendeleo ya ujuzi. Hii ni njema sana kwa waajiri,” anasema profesa.

Hoja ya Profesa Ngowi kuhusu bajeti kwa ujumla inashabihiana na hoja ya Esther Mkemamzi Kroll, akisema bajeti hii inaleta matumaini kwa Watanzania wengi.

“Ni bajeti ya kwanza ya Mama Samia na tayari tunaona mwelekeo mzuri. Sisi kama wazazi tuna furahi kuona mzigo wa faini unapunguzwa kwa vijana wetu wa bodaboda,” anasema Esther.

Anaamini makusanyo ya kodi kupitia simu za mkononi yataongeza fedha serikalini na kwamba kila jengo sasa litalipiwa bila kukwepa kodi.

“Kwa ujumla bajeti hii inavutia wawekezaji. Sisi ambao tunafanya kazi karibu na watu hawa tayari tumeshaanza kupokea simu wakitaka kuja Tanzania,” anasema mama huyu, ofisa wa zamani wa Kampuni ya Dangote aliyeshiriki katika kuhamasisha uwekezaji kwa miaka mingi.

Lakini Shaibu anasema kitendo cha kuendeleza miradi iliyoachwa na awamu iliyopita si sahihi.

“Huu utakuwa ni mzigo kwa wananchi. Bajeti hii ingepaswa kuangalia ni nini kinachotakiwa na wananchi kwa sasa badala ya kung’ang’ania miradi hiyo,” anasema.

Kwa upande wa Hamad, pamoja na kuridhishwa na mapendekezo yaliyomo kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha, anasema lazima sasa kuwe na takwimu sahihi za matumizi ya kodi za wananchi.

“Mlipa kodi akifahamu kuwa kodi yake imetumika kujenga mtaro fulani na mtaro huo ukaonekana, unamfanya aiamini serikali yake na kufurahia kulipa kodi,” anasema Hamad.

Kauli hii inaungwa mkono na Mnyele, akisema wananchi wanataka bajeti yenye tija.

“Mwigulu atambue kwamba Watanzania tunafuatilia. Mwakani tutataka majibu,” anasema.

Bunge limeanza mjadala wa bajeti wiki hii….