Tukisema tunaambiwa mahaba yametuzidi. Tunaambiwa tunyamaze kwa kuwa furaha yetu ni ya muda- bado yuko kwenye honeymoon (fungate).
Wapo wanaosema eti hata Jakaya Kikwete, alipoingia madarakani mwaka 2005 tulimshangilia, lakini baadaye ni sisi hao hao tuliogeuka na kuanza kumlaumu kwa uongozi wake legelegele.
Wanaosema hivyo hawajakosea hata kidogo. Ni kweli wengi wetu, si tu tulimshangilia, bali tulimuunga mkono na hata tukatoa mchango mdogo kuhakikisha anashika nafasi hiyo kubwa kabisa.
Kuwa au kutokuwa na matarajio kwa kiongozi anayetarajiwa au aliye madarakani ni jambo la kawaida. Kuwa na matarajio makubwa zaidi ndiko kunakoweza kuwa si sahihi, lakini kuonesha dhamira ya kumkubali kiongozi, sidhani kama ni jambo la ajabu.
Tuliomuunga mkono Mheshimiwa Kikwete mwaka 2005 tulifanya hivyo tukiamini angeweza kuivusha nchi yetu kutoka pale ilipokuwa na kwenda mbele zaidi. Matarajio yetu hayakuwa kumuona akiwa bingwa wa spidi za ndege au sura za wahudumu wa vyombo hivyo.
Mara kadhaa alituaminisha kuwa tabasamu lake halikumaanisha upole wake. Tena basi, akadiriki kusema” “Wale wanaosema mimi ni mpole, wasubiri tu wataona”. Watanzania hawahitaji kuelezwa kilichotokea kwa miaka 10 ya uongozi wake. Kama alivunja ‘mkataba’ wetu wa kushughulikia yaliyokuwa kero kwa wakati huo, tunawashangaa wanaoshangaa fungate letu kufikia tamati.
Tulipomshangilia Mheshimiwa Kikwete, hatukutarajia awe mlinda wezi na wahujumu uchumi. Sisi wengine tuliamini kwa kutumia fursa zetu katika kazi hizi, tungemsaidia kumwelekeza yalipo matatizo, ili yeye afanye kazi ya kujiridhisha kama ni matatizo kweli; ayashughulikie.
Mheshimiwa Kikwete, akafanya kinyume cha matarajio ya waliomuunga mkono. Akahakikisha hawagusi viongozi wezi na wahujumu uchumi pamoja na wafanyabiashara kadhaa. Akaufanya uongozi wa nchi uonekane mwepesi mno. Hilo limeonekana mwaka jana ambako kila aliyejipima, alijiona anaweza kuwa rais!
Hakuhangaishwa na kelele za waandishi wa habari na wananchi ambao kwa ujasiri mkubwa walijitokeza hadharani kumweleza nani waliokuwa wakiliumiza taifa. Majibu yake yakawa kwamba kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba kulala! Mambo mazito ya kitaifa kwake yakawa yanapewa hadhi kama ya maandishi ya kwenye khanga!
Mungu ni mwema, leo tumempata mtu ambaye wakati akiomba kupitishwa na chama chake, na baadaye akiwa anaomba ridhaa ya kuingia Ikulu, ahadi yake ikawa kuwaletea Watanzania mabadiliko ya kweli.
Ameingia madarakani, anachofanya ni kile alichowaahidi Watanzania ambao kwa wingi wao waliamua kumchagua. Wapo waliomtilia shaka pengine kwa kudhani kwa vile mtangulizi wake hakufanya kilichoendana na ahadi alizotoa wakati wa kampeni, basi huyu naye anaweza kuwa wa aina hiyo.
Siku chache baada ya Rais Magufuli kuingia ofisini, kumekuwapo idadi kubwa ya Watanzania waliomnyima kura ambao wanajutia uamuzi wao. Tunaambiwa hata kule kulikokuwa ngome kuu ya Ukawa, sasa kuna dalili ya kumkubali, na kwa maana hiyo chama chake kinaanza kupata uhai.
Mijadala mingi inaendelea nchini. Wapo wanaompongeza, na wengine wakimkosoa kwa staili yake ya uongozi. Hata wale waliokuwa wakimsema Mheshimiwa Kikwete, kwa uongozi wake legelege, na ambao walitamani kumpata kiongozi makini asiyekuwa na soni kwa watendaji wabovu, nao wanamshambulia Rais Magufuli.
Wala hili si jambo la kushangaza, na sidhani kama linaweza kumkatisha tamaa pamoja na timu yake ya Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. Jambo la ajabu ni kama watu wote tungekuwa na mtazamo mmoja.
Vyovyote iwavyo, nchi yetu ilimhitaji Rais aina ya Magufuli na Waziri Mkuu aina ya Kassim Majaliwa.
Huko nyuma nimepata kusema mifumo ya nchi yetu- karibu yote ilishakufa, isipokuwa mfumo mmoja tu wa kufanya mambo ovyo! Misingi yote ya uadilifu, uzalendo na utii wa sheria kwa nchi yetu vilishatupwa kabisa.
Mbunge wa Arusha, Godbless Lema, aliwahi kuifananisha Tanzania na ghetto la wahuni. Maisha ya ghetto yule anayewahi ndiye anayetumia kilago. Mkubwa ni yule aliyetangulia. Aliyewahi ndiye mwenye haki! Ghetto hakuna mfumo wa nani afanye nini, au nani amtii nani.
Ndani ya maneno haya ya Lema kuna ukweli unaonekana. Mwenye pesa alipoamua kufanya chochote, alifanya-hakuhofu polisi wala mahakama. Mwenye uhusiano polisi au katika chombo chochote cha ulinzi ama usalama aliweza kufanya alichotaka, na akatazamwa tu.
Maskini walipata shida. Walionewa. Wakikosa huduma za kijamii za matibabu na elimu. Wakubwa walitumia ukwasi wa nchi kusafiri huku na kule duniani kadri walivyojisikia. Walitibiwa nje huku wakiacha maskini wakilala sakafuni bila panadol. Juzi, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali katoa taarifa zikionesha bilioni 28 hivi zikiwa zimetumiwa kwa matibabu kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, mwaka jana. Tujiulize, makabwela wangapi walitibiwa India kwa fedha hizo? Hawapo, na kama wapo, basi ni wachache mno.
Mheshimiwa Kikwete akahakikisha anaendelea kuwalea mawaziri wabovu kabisa licha ya madudu yao kujulikana. Nchi ilishafikia hatua ya kila mtu kujiamulia kitu cha kufanya.
Leo tumempata kiongozi mkuu na wasaidizi wake wanaobadili mambo kuwa mazuri. Tumewapata viongozi walio tayari kuifia nchi kwa kuhakikisha wanasimamia misingi ya haki na maendeleo. Wanafumua mifumo yote ya ukwepaji kodi ambayo watangulizi wao walijifanya hamnazo-wakaruhusu nchi itafunwe kwa kadri ya mtu alivyoweza.
Wananchi wanapomshangilia Rais Magufuli au Waziri Mkuu Majaliwa, hawawashangilii kwa sababu wanatumbua tu viongozi waliofeli, bali wanashangilia kwa kuwa wanauona mwanga wa matumaini kwa hatima ya maisha yao na taifa lao kwa jumla.
Jumamosi iliyopita ilikuwa siku ya usafi kama ilivyo ada. Nilipita mitaa kadhaa nikienda kazini. Watanzania sasa, bila shuruti wanashika fagio, makwanja (mafyekeo) na zana mbalimbali za usafi. Wanashiriki usafi bila shuruti. Wale tulioiona Tanzania ya miaka ile, tunapoona mema ya aina hii-mambo ya kuwaunganisha Watanzania-tunatokwa machozi ya furaha. Tunakumbuka zama tulizoitana ‘ndugu’.
Awamu iliyopita ilishindwa kuwaunganisha Watanzania kwa kutumia mambo ya kawaida kabisa kama hili la usafi. Kama tumewapata viongozi sasa wanaofanikisha mambo yenye tija kama haya, kuna sababu gani ya kuona haya kuwaunga mkono hadharani?
Wale wanaotumia barabara ya Morocco-Mwenge, wanaona nafuu iliyoanza kupatikana. Makali ya foleni yamepunguzwa. Raha hii imeletwa na kiongozi kwa kuamua fedha ambazo zilikuwa zitumbuliwe na genge la walaji wachache, zitumike kupanua barabara! Wapo wanaohoji mamlaka ya Rais kuelekeza matumizi ya fedha kwenye jambo kama hili la barabara! Lingekuwa jambo la maana kuhoji kama fedha hizo angekuwa kazikabidhi kwa familia yake ili iende ughaibuni kununua nguo au kukaguliwa afya! Alimradi fedha hizo zimefanya kazi iliyo machoni kwa wananchi wenyewe, wananchi hawaoni kosa. Rais hakutumia hizo Sh milioni 4 kukarabati makazi yake, bali kuwaondolea wananchi wake kero ya foleni.
Jambo jingine ni safari za watumishi wa umma nje ya nchi. Rais hajazuia safari. Ametaka uwepo utaratibu mzuri ili safari ziwe zile zilizo na tija tu. Tumempata Rais sasa anayeamini maendeleo ya nchi yanaletwa kwa kutumia muda mrefu kufanya kazi ndani ya nchi badala ya kushindia ughaibuni. Udhibiti wa safari siyo tu Tanzania, bali hata katika mataifa makubwa yaliyoendelea yanafanya hivyo. Tulikuwa na Rais anayeiacha nchi yake kwa wiki tatu. Hili siyo jambo la kawaida kwa rais wa nchi, isipokuwa hutokea kama anakuwa katika matibabu.
Wazanaki wanasema “Nyamugya obughini atakhuta aghaye”, yaani mtu kama ni mwanga au mwizi, hata akienda ugenini bado atafanya yale yale aliyozoea kuyafanya. Tumeona wapo hata baada ya kung’atuka, wanasafiri nje ya nchi kana kwamba huku nyumbani hawana wa kunywa nao chai. Kwao, babu au bibi kuketi na wajukuu si jambo la maana.
Miezi mitano sasa kuna dalili ya kuipata Tanzania mpya. Wananchi wameanza kufurahishwa na huduma zinazotolewa katika taasisi kadhaa za umma. Urasimu na majibu ya kejeli kutoka kwa watumishi hao vimeanza kupungua. Haya ni mabadiliko makubwa.
Tunachopaswa kukifanya ni kuendelea kumuunga mkono Rais Magufuli, na watendaji wote wa Serikali wenye nia njema ya kuijenga Tanzania mpya.
Malalamiko yataendelea kuwapo kwa sababu tulishafikia hatua mbaya. Kuufumua mfumo huu ni kazi ngumu itakayochukua muda. Wale walioifaidi nchi hii kwa hila hawawezi kumpenda Rais Magufuli wala Waziri Mkuu Majaliwa. Hao watajitahidi kuuaminisha umma kwamba kinachofanywa na viongozi hawa ni udikteta.
Kwa kuwa idadi ya wanaowapinga ni ndogo, tuna wajibu wa kuhakikisha hawafanikiwi kuwakwaza viongozi wetu waliojitolea maisha yao yote kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania walio wengi. Wajibu wetu tunaopenda kuiona Tanzania mpya ni kuhakikisha tunawaunga mkono na kuwa watetezi wao kila inapobidi.
Bahati nzuri wapo waliokwishang’amua kwamba zama hizi si zile za ‘bora liende’. Hao hawanung’uniki. Wanaolalamika ni wale wanaodhani bado wako katika zama za kufanya lolote na bila kuwajibishwa. Hao wanapaswa kubadilika sasa.
Alishasema, wale waliotumbuliwa ili kupisha uchunguzi, wakibainika hawana dosari, watarejeshwa kazini. Bila shaka hilo litamjengea heshima.
Rais Magufuli, akiwa anaelekea kutimiza nusu mwaka Ikulu, kila nikitafakari mengi aliyofanya kwa maslahi ya makabwela wa nchi yetu, nashindwa kuliona kosa lake.