Kabla janga la homa ya corona kulipuka na kuwa balaa tunaloshuhudia, nilianza kuandika makala juu ya athari za awali kabisa za kiuchumi zilizojitokeza. Nikidhani wakati huo, tofauti na sasa, kwamba athari za kiuchumi zingekuwa kubwa kuliko zile za kiafya.
Kinachotokea na kuwa duniani kote kipaumbele ni kuwakinga watu dhidi ya maambukizi. Tunalazimika kuokoa maisha yetu kwanza kabla ya kuanza kulalamikia hali mbaya ya uchumi.
Hata hivyo, kwamba sasa suala la tatizo la kiuchumi si changamoto inayoongoza, si sawa, na kusema kuwa haitajitokeza kuwa changamoto kubwa katika kipindi kijacho. Masuala mengi huhitaji muda upite ili kubaini upana wa athari zitakazojitokeza.
Katika mchakato wake wa kuokoa maisha ya raia wake, China ilisitisha shughuli za kiuchumi na hali hiyo ikasababisha ipunguze uagizaji wa mafuta kutoka nje kwa asilimia 20. China, kwa takwimu za 2018, iliagiza mafuta ya thamani ya Dola bilioni 239.2. Hizo ni Sh 552,623,760,000,000. Kwa kutamkwa kwa Kiswahili ni shilingi trilioni mia tano hamsini na mbili na nukta sita kwa kipawa cha nne.
Kama lugha ya Kiswahili inakosa neno moja na badala yake kulazimika kuunganisha maneno manne kuitaja tarakimu, tukubaliane hiyo hesabu si ya kawaida, ni kubwa. Hatushangai basi kwamba ikipungua kwenye soko inayumbisha uchumi wa dunia.
Matokeo yake kuyumba ni kuwa baadhi ya wazalishaji wakubwa wa mafuta wameanza kuzozana. Katika mkutano wa hivi karibuni wa nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani (OPEC), Saudi Arabia na Iran zilitaka nchi wanachama wa OPEC kupunguza uzalishaji kwa mapipa milioni tano ili kudhibiti kuanguka kwa bei ya mafuta kutokana na kupungua mahitaji.
Urusi ilikataa pendekezo la kupunguza uzalishaji kwa sababu iliona hatua hiyo itasababisha kuhimili anguko la bei ya mafuta, hivyo kuisaidia Marekani kufaidika na uzalishaji na biashara ya mafuta.
Mwaka 2014 Marekani iliingia kwenye soko la mafuta ulimwenguni baada ya kugundulika kuwepo akiba kubwa ya mafuta ya miamba inayojulikana kama ‘shale’. Tofauti na uzalishaji wa mafuta ghafi yanayopatikana kwa wingi Saudi Arabia na Urusi, uzalishaji wa mafuta ya shale unalazimu kuchakatwa kutoka kwenye miamba na ni ghali zaidi kuliko uchimbaji wa mafuta ghafi.
Kupunguza uzalishaji, kama ilivyopendekeza Saudi Arabia, kungezuia bei za mafuta kushuka na hali hiyo kwa mtazamo wa Urusi ingesaidia wazalishaji wa mafuta wa Marekani kuendelea kuhimili misukosuko ya soko na kuendelea kufaidika na mafuta.
Urusi ilivyogoma kupunguza uzalishaji, Saudi Arabia, inayoongoza kwa uzalishaji wa mafuta ghafi, ikaamua kupunguza bei ya mafuta yake ili kuiadhibu Urusi. Adhabu hiyo ikiendelea itaathiri zaidi soko la mafuta ya shale ya Marekani na wazalishaji wadogo wa mafuta ghafi ulimwenguni.
Kwa kawaida, ugomvi wa wazalishaji wa mafuta ungepaswa kumpa ahueni mnunuzi wa mwisho kwa kuwa kushuka kwa bei kunapunguza gharama za uzalishaji kwa bidhaa na huduma mbalimbali. Lakini wachambuzi wanasema kuwa ahueni hiyo ni ya muda mfupi. Kwa mtazamo wa muda mrefu ni bei za juu za mafuta ambazo zinasaidia kukuza na kuimarisha uchumi wa dunia. Kinadharia, uchumi wa dunia ukiimarika, kila mtu ananufaika.
Najaribu kukubali mantiki kwamba nikilipia Sh 4,000 kwa lita moja ya petroli badala ya Sh 500 nitachangia kuimarisha uchumi wa dunia, lakini ninasita kukubali hoja kuwa bei kubwa ina manufaa kwa wote. Ni kweli, kimahesabu ni suala lililo wazi: iwapo sipunguzi mahitaji yangu na kama ninatumia lita 10 kwa siku, bei kubwa nitakayokubali kulipa itahesabika kama ongezeko la kukua kwa uchumi.
Wachumi wanatuambia kuwa manufaa hayaonekani kwenye takwimu za kukua kwa uchumi pekee.
Takwimu za Indonesia zinabainisha kuwa katika kila dola milioni moja zinazowekezwa katika sekta ya mafuta na gesi, uwekezaji huo unasababisha ongezeko la thamani la dola milioni 1.6, linakuza uchumi kwa dola laki saba, na kuongeza ajira ya watu 100.
Lakini baadhi ya tafiti zinakinzana na misimamo hii. Katika utafiti wake wa 2011, Latife Ghalayini, anabainisha kuwa nchi zinazopata manufaa ya kiuchumi kutokana na kupanda kwa bei za mafuta ni nchi za G-7 pekee: Marekani, Italia, Japan, Canada, Ujerumani, Ufaransa, na Uingereza.
Kundi hilo la nchi zenye nguvu kubwa kiuchumi duniani limepanuka sasa na linajulikana kama G-20 likiwa na nchi nyingine za ziada zinazowakilisha asilimia 90 ya uchumi wa dunia, asilimia 80 ya biashara ya dunia, na theluthi mbili ya watu duniani.
Tunaoachwa pembeni ya kundi hilo ni nchi nyingine zaidi ya 200 zenye watu maskini zaidi duniani.
Alichobaini pia Ghalayini kwenye utafiti wake ni kuwa nchi zisizozalisha mafuta hupata pigo kutokana na ongezeko la bei ya mafuta. Cha ajabu pia ni kuwa hata faida inayotokana na kupanda bei ya mafuta kwa nchi zinazozalisha mafuta nayo huelekea zaidi kwenye nchi ambazo zinafaidika na ongezeko la bei.
Pamoja na kuwa ni machache, ni ukubwa wa uchumi unaomilikiwa na mataifa makubwa unaosababisha kukua kwa uchumi wa mataifa hayo kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta, lakini ukweli ni kuwa kuna mataifa mengi huumizwa na ongezeko la bei ya mafuta.
Kijijini tajiri mmoja anayemiliki biashara zote anapopandisha bei za bidhaa na huduma wanakijiji wanaotegemea bidhaa na huduma hizo hawana budi kukubali ongezeko la bei. Takwimu za tajiri zitaonyesha ongezeko la mapato, na Mamlaka ya Mapato Tanzania itakusanya kodi zaidi na kusifiwa na serikali kwa kufikia malengo lakini hakuna atakayekumbuka kuwashukuru wanunuzi waliokubali kupandishiwa bei na kuwasifu kuwa chanzo cha mafanikio hayo.
Vita ya Saudi Arabia na Urusi ni vita vya mafahali. Haitaruhusiwa kuendelea kwa muda mrefu kwa sababu ya athari zake kwa wakubwa. Tusubiri muda ukifika, wadogo tuanze kuumia.