Nadhani mjadala wa kutaka Nahimana achunguzwe utakuwa umefika mwisho. Timu zetu zina makipa lakini kuna tatizo kubwa la makocha wa magolikipa. Tumeshuhudia makipa wazuri wakisajiliwa katika timu zetu wakiwa bora lakini baada ya muda viwango vyao vinashuka kadri muda unavyokwenda.
Timu pekee ambazo zina makocha wa makipa serious ni Yanga, Simba na Azam lakini timu nyingine ‘zinaungaunga’ tu na nyingine huwa hazina makocha wa makipa kabisa.
Fikiria kilichotokea pale Azam kwa misimu mitatu mfululizo upande wa makipa tukianzia kwa Mathias Chigonya mpaka sasa. Nini kilimkuta Farouk Shikalo na Metacha Mnata wakiwa Yanga? Fuatilia kilichotokea kwa makipa wote watatu wa Dodoma Jiji msimu uliopita.
Nenda kule Ihefu gonjwa lipo golini mwao, fuatilia kinachotokea langoni kwa Ruvu Shooting kisha malizia na Polisi Tanzania halafu tafakari hiki kilichomtokea kipa wa Geita Gold kwenye mechi ya Simba. Bado mna kesi na Nahimana?