Watu mbalimbali ndani na nje ya nchi wamepokea kwa shangwe kuachiwa huru kwa mwanamuziki maarufu wa muziki wa dansi nchini, Nguza Viking (Babu Seya) na mwanawe, Johnson Nguza (Papii Kocha) baada ya kuwapo gerezani kwa miaka 13 na miezi minne.

Wawili hao walitoka Gereza la Ukonga saa 12 jioni na kulakiwa na umati wa watu wakiwamo marafiki na ndugu zao.

Rais John Magufuli, aliwaachia huru wafungwa hao ikiwa ni sehemu ya wafungwa 8, 157 waliopata msamaha kwa kuachiwa. Wafungwa 1,828 kati ya hao waliachiwa huru kuanzia jana. Wafungwa 6, 329 wamepunguziwa muda wa kukaa gerezani. Idadi ya wafungwa wote walioko katika magereza mbalimbali nchini ni 39,000; huku 666 wakiwa ni wale wenye vifungo vya maisha kama ilivyokuwa kwa Babu Seya na Papii Kocha.

Rais alitumia ibara ya 45 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayotoa mamlaka kwa Rais kutoa msamaha kwa wafungwa.

“Sisi sote ni binadamu, na hata mimi huwa namwomba Mungu anisamehe, ingawa sisi wanadamu ni wagumu kusamehe. Hivyo natangaza msamaha kwa familia ya Nguza Viking maarufu kama Babu Seya na watoke leo, alisema.

Kuhusu wafungwa 61 waliohukumiwa kifo, Rais Magufuli, alitangaza kuwasamehe kutokana na kukaa gerezani kwa miaka mingi.

Alisema baada ya kufanyika uchunguzi, imegundulika wafungwa hao wamejutia makosa yao kwa kiasi kikubwa na wamejirekebisha. Miongoni mwa waliosamehewa ni mzee mwenye umri wa miaka 85.

Nguza Viking ni mmoja wa wanamuziki nyota wa ndasi ambaye alitamba na bendi kadhaa nchini tangu alipoingia nchini kutoka kwao Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), ikiwamo Orchestral Safari Sound (OSS).

Mkuu wa Magereza amweleza Rais Magufuli

Kamishna Jenerali wa Magereza Tanzania, Dk. Juma Malewa, alikwenda Ikulu Ndogo Chamwino, Dodoma kwa ajili ya Rais Magufuli kusaini majina ya wafungwa waliopunguziwa na wengine waliofutiwa vifungo. Katika maelezo yake kwa Rais, alisema: “Ukonga sijui ilizizima au ilikuwa moto kwa sherehe kwa watu nje na ndani ya gereza. Ndani ya gereza afande kulikuwa na msisimko mkubwa sana, kwanza taarifa zile hakuna mtu aliyejua mpaka ulipokuwa umetangaza.

“…Papii Nguza huyu alikuwa kwenye uchezaji mpira, ni mchezaji mpira mzuri sana huyu mtoto wa Babu Seya, alikuwa mpirani akaitwa kutoka kwenye mpira ‘bwana njoo, kuna hili suala’. Hakuamini na baba yake hakuamini.

“Wametoka afande, wamepokelewa vizuri pale nje, watu afande wanajua kumbe mamlaka ipo kwamba na Rais ni mtu mwenye mamlaka makubwa sana.

“Afande umetengeneza historia kubwa sana ambayo ulimwengu huu nadhani itakumbukwa kwa muda mrefu sana au milele. Mimi nimekaa magereza zaidi ya miaka 30 sasa hakuna tukio kama hili ambalo limetokea Tanzania na hata ulimwenguni sikuwahi kusikia tukio kama hili linatokea.

“Lakini  mheshimiwa hii ni heshima ya pekee umetoa kwa wananchi wako, nadhani watakukumbuka na mimi msaidizi wako. Afande mimi nina uhakika wataishi kwa amani kiasi kwamba ndani ya magereza sasa hivi kutakuwa na amani kubwa sana kwamba kumbe ukikaa kwa kurekebishika mamlaka zipo zinazoweza kukuona na kukufanyia kile ambacho mamlaka inapenda kukifanya. Mkuu naomba nikushukuru sana. Asante sana.”

Rais Magufuli aeleza

Wakati akipokea karatasi zenye majina ili atie saini kuachiwa huru na kupunguziwa adhabu wafungwa hao kutoka kwa Kamishna Jenerali wa Magereza, Dk. Malewa, Rais Magufuli alisema: “Ukishaona mtu amejirekebisha na mara nyingi hata hawa tuliowaachia nilichambua wale ambao hawakufanya makosa ya kuua ndugu zetu albino, wala sio magaidi, lakini pia si majambazi.

“Wengine wameua kwa bahati mbaya, ndiyo maana niliona nitumie hiki kifungu ambacho ni cha Katiba, ambacho nilipewa na Watanzania kukitumia ingawaje kilikuwa hakijawahi kutumika.

“Nimeona nikitumie, unajua mtu anapohukumiwa kunyongwa na baadaye anaachiwa huru ni kitu kinashtua na kinashangaza kwa sababu kilikuwa hakijatokea katika kipindi chote cha maisha ya hapa.

“Lakini nafikiri nina wajibu wa kufanya hivyo kwa ajili ya faida ya Watanzania. Mimi nikuombe tu, muendelee kusimamia wajibu wenu kwa kuzingatia sheria mtu anayehukumiwa kufungwa afungwe kweli.

“Na nilikwishatoa wito kwako na kwa Magereza kwa ujumla, pasiwepo na mfungwa wa kukaa tu na kupumzika. Muwafanyishe kazi kweli kweli. Kufungwa sio kustarehe. Tuna miradi mingi sasa hivi, tuna mradi wa reli ya standard gauge, tuna majengo na kadhalika. Wapelekeni hawa wakafanye kazi.”

Kushitakiwa

Wanamuziki hao walikamatwa na kisha kufunguliwa kesi ya ubakaji na ulawiti. Walishitakiwa kwa kuwabaka na kuwalawiti watoto 10 wa kike wenye umri kati ya miaka 6 na 8 ambao walikuwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mashujaa, Sinza jijini Dar es Salaam. Walikamatwa Oktoba 12, 2003 na kupelekwa Kituo cha Polisi Magomeni jijini Dar es Salaam.

Waliokamatwa ni Nguza mwenyewe, Papii Kocha, Nguza Mbangu na Francis Nguza ambao ni watoto wake. Babu Seya na wanae walitiwa mbaroni baada ya mmoja wa watoto hao kugunduliwa na bibi yake kuwa alikuwa ameharibiwa sehemu za siri.

Baada ya bibi huyo kumhoji ndipo alipoeleza kuwa amekuwa akifanyiwa vitendo hivyo yeye na wenzake na Babu Seya.

Kupandishwa kizimbani

Oktoba 16, 2003 wapandishwa kizimbani Babu Seya na wanae watatu pamoja na mwalimu wa kike wa Shule ya Msingi Mashujaa. Walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Walisomewa mashitaka 21. Katika mashitaka hayo, 10 yalikuwa ya ubakaji na mashitaka mengine 11 ya kuwanajisi watoto hao.

Kifungo: Juni 25, 2004 walihukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kutiwa mbaroni katika Mahakama ya Kisutu. Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Addy Lyamuya baada ya kuwatia hatiani kwa makosa 20 ya ubakaji na ulawiti.

Pia Hakimu Lyamuya aliwaamuru kuwalipa fidia ya Sh milioni 2 kila mtoto. Mwalimu wa shule hiyo aliachiwa huru.

Kukata rufaa: Januari 27, 2005 wakili wao aliyewatetea katika kesi ya msingi, Hubert Nyange, alikata rufaa Mahakama Kuu. Jaji Thomas Mihayo aliyesikiliza rufaa hiyo alitupilia mbali.

Babu Seya, Papii waendelea na kifungo: Februari 11, 2010 Babu Seya, Papii Kocha waliendelea na adhabu ya gerezani, huku watoto wake wawili wakiachiwa huru. Waliwakilishwa na Wakili Mabere Marando. Walikata rufaa Mahakama ya Rufani wakipinga hukumu ya Mahakama Kuu. Walishindwa katika rufaa yao ya pili.

Mahakama ya Rufani katika hukumu yake ya jopo la majaji watatu; Nathalia Kimaro, Salum Massati na Mbarouk Mbarouk, Februari 11, 2010 ilitupilia mbali rufaa dhidi yao kuwa hoja zao hazikuwa na mashiko na hivyo ikaridhia kuendelea na kifungo hicho cha maisha.

Mahakama hiyo ikawaachia huru Mbangu na Francis baada ya hoja za Wakili Marando kuwa hapakuwa na ushahidi wa kuwatia hatiani.

Wajaribu tena: Desemba 22, 2013 walifungua maombi ya marejeo wakiiomba Mahakama hiyo irejee tena hukumu yake hiyo na hatimaye ione kuwa ilikosea na hivyo iwaachie huru. Hata hivyo, walishindwa.

Katika uamuzi wake uliosomwa na Kaimu Msajili, Zahra Maruma, Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali maombi hayo ikisema kuwa waomba marejeo hao hawakuwa na hoja za msingi.

Wahamishia matumaini yao kwa Rais: Akisindikizwa na askari kuelekea kwenye gari kurejeshwa gerezani, Papii Kocha alisema: “Sasa tunamwachia tu Rais ndiye anayeweza kutoa uamuzi wa mwisho.”

Babu Seya yeye akasema: “Kwa binadamu ni makosa, lakini kwa Mungu hakuna makosa.”

Juni 21, 2014 walimlilia Rais Jakaya Kikwete awasamehe. Walitoa ombi hilo kupitia wimbo wao wakati wakitumbuiza katika maadhimisho ya Siku ya Magereza iliyofanyika Chuo cha Magereza Ukonga, Dar es Salaam na mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe. Babu Seya na Papi Kocha walikuwa na bendi ya wafungwa.

“Waziri Chikawe tunaomba umfikishie Rais Jakaya Kikwete ombi letu, mwambie atusamehe. Hata Petro alimkana Yesu mara tatu, lakini Yesu alimsamehe kwa nini sisi…,” alisikika akiimba Papii Kocha.

Waziri Chikawe alijibu maombi hayo kwa kusema: “Nimesikia maombi yenu, yamefika na nitajitahidi kuyafikisha kwa Rais Kikwete.”

Babu Seya na Papii hawakukata tamaa. Novemba 2015, walipeleka maombi yao katika Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika (AfCHPR) ambako walifungua kesi namba 006/2015, wakidai kuwa haki zao zilivunjwa, hivyo walikuwa wakiiomba waachiwe huru.

Desemba 9, 2017, saa 12 jioni wafungwa hao waliachiwa huru kutoka Gereza la Ukonga, ikiwa ni utekelezaji wa msamaha wa Rais Magufuli, alioutoa wakati akihutubia katika kilele cha Sherehe za miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) mjini Dodoma.

Barua ya Papii Kocha

Mwaka 2013 Papii Kocha alimwandikia Rais Jakaya Kikwete barua ya kuomba kuachiwa. Hapa chini tunaichapisha neno kwa neno bila kuihariri kama ilivyoandikwa na Kocha mwenyewe. Ilisomeka:

 Maombi ya kupewa msaada (msamaha) wa kufutiwa adhabu ya kifungo niliyopewa na mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Oct  2013

Husika na somo hilo hapo juu.
Mimi ni mfungwa katika gereza kuu la Ukonga.

Kwa heshma na taadhima na kwa kutambua utu na huruma yako ya ki-MUNGU ulionayo dhidi ya binadamu wenzako pamoja na mamlaka uliokabidhiwa na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Naanguka na kushika miguu yako mitukufu muheshimiwa rais. Nakuomba msaada (msamaha) kwako muheshimiwa rais, kwa njia hii ya maandishi kusudi niweze kuondolewa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani,niliyohukumiwa na mahakama tajwa hapo juu.
 Mh.Rais mimi nimefungwa nikiwa bado kijana mwenye umri mdogo, na ukweli kutoka moyoni sikufanya kosa hilo. Si mimi, baba yangu Nguza wala ndugu yangu yeyote aliyefanya kitendo kile. Lakini wenye mamlaka wakatuona tuna hatia na kuamua kuteketeza kizazi chetu gerezani.
Natamani kiama ifike ili mwenyezi Mungu aweke wazi ukweli wote uliojificha nyuma ya pazia. Mpaka sasa natambua wazi hatima pamoja na dhamana ya maisha yangu ipo katika mikono yako mitukufu Mh. Rais Naomba huruma yako muheshimiwa rais maana mimi ni mtoto wako ninayehitaji
huruma yako wewe mzazi. Lakini pia sisi ni binadamu wenye nafsi na miili kama wengine. Waliotumia mamlaka yao kutuweka gerezani nao ni binadamu pia, wenye miili na nafsi. Ipo siku nafsi zetu zitapaswa kutoa hesabu ya tuliyoyafanya hapa duniani. wakati huo miili yetu tunayoitumia
kunyanyasa wanyonge itakuwa imeoza mavumbini.
Natumaini kauli yako ya mwisho ndio itakayoleta pumzi ya uhai nafsini mwangu. Nakutakia kazi njema, afya njema na maisha marefu.

Mungu akubariki.
Wako mtiifu
Mfungwa NO: 836’04
JOHNSON NGUZA (PAPII KOCHA)

Wakizungumza na JAMHURI baadhi ya wakazi wa Sinza wamesema ni furaha kubwa kwao kuungana tena na wanamuziki hao.

John Paul ambaye aliyekuwa jirani wa wanamuziki hao Sinza Palestina, amesema ni Mungu pekee mwenye uwezo wa kutenda miujiza kama iliyotokea kwa Mzee Nguza na mwanawe Nguza.

“Nimeishi kwa miaka mingi na familia ya Mzee Nguza kabla ya kukutwa na majanga kwa zaidi ya 25, ndani ya miaka hiyo sikuwahi kusikia mabaya yoyote juu yao,” amsemaPaul na kuongeza:

“Rais ameonyesha ubinadamu na amedhihirisha kuwa yeye ni binadamu mwenye huruma na upendo miongoni mwa wanadamu wanaoishi hapa ulimwenguni ambao siku moja watauonja umauti na kuuacha ulimwengu huu.”

Mkazi mwingine wa Sinza Kumekucha, Hassan Abdallah, amesema Mungu ametenda maajabu yake kupitia Rais Magufuli, na kuwa kinachotakiwa ni kuungana kuwakaribisha uraiani.

“Familia hii majirani zangu kwa zaidi ya miaka ishirini iliyopita mpaka mwaka 2004 walipopatwa na majanga ya kubaka na kulawiti na Mahakama kuwaamuru kwenda kutumikia kifungo cha maisha jela,” amesema Abdallah.

 “Wanadamu tunao maadui wengi, lakini adui namba moja aliyewapeleka wengi katika njia wanayoitegemea na kujuta maishani, adui aliyewaingiza maelfu kaburini kabla ya muda wao, adui aliyewafanya wengi kuonekana wazee kumbe bado vijana ni kukata tama,” amesema Abdallah.

Yusufu Pendeza ambaye ni mkazi wa Sinza kwa Remy amesema familia ya Nguza ameijua kutokana na kupenda kwenda katika uwanja wa timu ya mpira ya Abajalo iliyopo jirani na ilipokuwa ikiishi kabla ya kukumbwa na matatizo.

“Francis Nguza mmoja wa watoto wa familia hiyo alikuwa akipenda sana kucheza mpira na mara nyingi tulikuwa tukikutana naye uwanjani wakati wa jioni mara baada ya kutoka shuleni,” amesema.