Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, ametangaza kumsamehe Nguza Viking marufu kama ‘Babu Seya’ na mwanae Johnson Nguza ‘Papi Kocha’ waliokuwa wamehukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa la kubaka.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo Mjini Dodoma katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 56 ya Uhuru zilizofanyika katika uwanja wa Jamhuri.
Nguza na wanawe watatu walikamatwa Oktoba 12, mwaka 2003 na kufikishwa Kituo cha Polisi Magomeni, Dar, walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Oktoba 16, mwaka 2003 wakituhumiwa kubaka na kunajisi watoto 10.
Mnamo Februari, 2010, Mahakama iliridhia hukumu ya kifungo cha maisha kwa Babu Seya na Papii Kocha, ikawaachia huru watoto wake, Mbangu na Francis Nguza.
Sambamba na Babu Seya, Rais Magufuli amewasamehe wafungwa 8,157 waliokuwa wakitumikia vifungo vya makosa tofauti tofauti ambapo wafungwa 1,828 wataachiwa leo, na waliobakia 6,329 wataachiwa kwa kufuata utaratibu.
Vile vile Rais amewasamehe jumla ya wafungwa 61 waliokuwa wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa ambapo wafungwa wawili wako gereza la Uyui, 5 Butimba, Rwanda-Mbeya 4, Isanga-Dodoma 15, Maweni-Tanga 11, Kiguluwira 5 na Ukonga wafungwa 19.