Ndugu Rais, imani yangu ni nchi yangu kwanza! Tangu mwanzo wa nyakati hadi utimilifu wake mimi si lolote, si chochote, bali sauti ya mtu aliaye kutoka jangwani ikisema: “Watumikieni watu wa Mungu, wananchi wa nchi hii.”
Naililia nchi yangu, nawalilia wananchi wenzangu, namlilia rais wangu, najililia na mimi mwenyewe! Atakapokuja kutokea wa kuwatofautisha watu wa Mungu wa nchi hii na akawafanya wabaguane katika ardhi hii hii tuliyopewa na Mungu katika umoja wetu, huyo tuje tumkatae wote! Alituusia Baba wa Taifa, huyo hatufai! Tumuogope kama ukoma! Naye anamtendea kazi mwovu! Imeandikwa: “Alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”
Ni faraja kubwa kutambua kuwa baba unanipenda. Umenisoma kwa muda mrefu na kutokea mbali nawe umenielewa. Kama ambavyo sina ushabiki wa mpira wa miguu, hivyo ndivyo nilivyo, sina ushabiki wa kisiasa. Sishabikii chama chochote cha siasa wala simshabikii mwanasiasa yeyote. Daima naheshimu busara kubwa na fikra nzito zinazolenga kuistawisha jamii yetu alizonazo yeyote hata kama mtu huyo atakuwa ni mwanasiasa.
Kinachonifariji zaidi baba, ni pale ninapotambua kuwa hukuyaficha mapenzi yako kwa fikra zangu ndani katika kifua chako, bali mara kadhaa ulinionyesha dhahiri na wote wenye mapenzi mema wakajua.
Na kwa sababu hiyo nitakuwa pamoja na wewe kama ilivyokuwa mwanzo, sasa na hata baadaye. Nafunga nadhiri, ikijakutokea nikashindwa kukuambia ukweli, basi ulimi wangu na ugandamane na taya zangu!
Tunasoma kuwa wanafunzi wake walimuuliza, utuambie basi siku ya mwisho itakuwaje? Akawajibu akawaambia: “Msijisumbue kuuliza siku ya mwisho itakuwaje, kwa sababu ishara za siku hiyo zitakuwa wazi. Watazameni ndege wa angani, wanayajuaje majira ya nchi? Kama ndege wanaweza kujua, nyinyi pia hamtashindwa kuzijua ishara za siku za mwisho.”
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro, alitumia takriban saa nzima na dakika kumi kukemea na kutoa kile kilichoonekana na baadhi ya wengine kama kunung’unika kutokana na utendaji kazi wa baadhi ya maofisa wenzake wa Polisi. Aliyoyatamka IGP Sirro yanakumbusha wakati wa Yesu Kristu. Simoni aliitwa Jiwe. Jiwe kuu la pembeni. Akasema na juu ya jiwe hili nitalijenga kanisa langu.
Huyu ndiye IGP wa kwanza ambaye kabla hajawa, akiwa RPC wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na mama aliyekuwa RPC wa Mkoa wa Kinondoni wakati huo, walituhumiwa hadharani mbele ya Waziri Mkuu wetu Kassim Majaliwa kuwa walipokea rushwa kutoka kwa wafanyabiashara wa kilevi kilichojulikana kama shisha. Tuhuma hizi hazijajibiwa hadi leo. Wananchi walishukuru kwa busara kubwa aliyoionyesha waziri Mkuu wetu alipomjibu mtoa tuhuma kwa ukali na kwa usahihi, hivyo kumfunga mdomo pale pale hadharani.
Akawatoa hofu wananchi iliyokuwa imeanza kuwaingia kuhofia kujirudia yale wengine waliyodhania ndiyo yaliyomsababishia mauti ambaye sasa ni marehemu mwanamwema Wilson Kabwe wakati wa ufunguzi wa Daraja la Mwalimu Nyerere, Kigamboni. Mwenyezi Mungu ana njia zake za kuhukumu!
Kwa tuhuma nzito kama zile mbele ya kiongozi mkuu, huku taifa zima na wananchi wakishuhudia, Simoni, hakufungua kinywa chake. Alinyamaza kimya! Watu wa Kongo wana msemo: “Saa ikienea, bubu husema.” Simoni sasa anasema: “Kwa hiyo tuna case study kama Jeshi la Polisi ni tukio la Akwilina na Mwangosi, kitu gani kilitokea. Changamoto kubwa huwa inatokana pale amri inapokuwa dhaifu, haya yanatokea, kwa mfano yale yaliyotokea Kinondoni wote ni mashahidi hatuwezi kulisema, lakini kuna mahala ambako sisi kama Jeshi la Polisi hatukutimiza wajibu wetu.”
Waziri kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, amesema kauli za IGP Simon Sirro zinaonyesha Roho wa Bwana amemshukia Sirro. Kwa sababu Kamanda wa Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alikiri hadharani, lakini kesi wamepewa wengine. Wanawema, kuna tofauti gani kati ya mtu anayesema: “Kwa mfano yale yaliyotokea Kinondoni wote ni mashahidi, hatuwezi kulisema, lakini kuna mahala ambapo sisi kama Jeshi la Polisi hatukutimiza wajibu wetu.” Na mtu mwingine akasema: “Yaliyotokea Kinondoni wote ni mashahidi na ninasema sisi kama Jeshi la Polisi tunapaswa kuwajibika kwa sababu kuna mahala hatukutimiza wajibu wetu?’’
Namna kesi ya viongozi tisa wa Chadema ilivyotengenezwa imeuvuta umakini wote wa dunia ambayo nayo sasa inatushangaa! Ni uzezeta kudhani tumejifunika nguo wakati tumejianika utupu. IGP Simon Sirro anasema kifo cha mwandishi wa habari Daudi Mwangosi kilitokana na udhaifu wa amri. Watanzania wanauliza, ni polisi gani wamewajibishwa kutokana na udhaifu wa amri uliosababisha Akwilina kuuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala? Iko sauti ya kiongozi ilisikika ikisema: “…Ndiyo, kwa maana tuliambiwa wengine wataandamana wakiwa ndani ya daladala.” Ole wake mtu huyu! Hukumu iko juu ya kichwa chake.
Nilipoandika nyongo mkaa na ini nilitumiwa ujumbe kutoka Dodoma ukisema: “Kamanda Simon Sirro namfahamu vizuri. Nilimaliza naye kozi. Ni mtu mcha Mungu’’. Uovu mwingi uliotendeka katika nchi umeufurisha moyo wake mwema na sasa anamrejelea Muumba wake. Wazungu walisema: ‘Time will tell’. Kupitia kwa Simoni, wakati sasa unaanza kusema! Tumeambiwa tusiulize ishara za siku za mwisho kwa sababu ziko wazi. Huyu ni jiwe. Na juu ya jiwe hili utatoka ukombozi kwa wote walioumizwa!
Watanzania wema bado wanatiririsha machozi wakiomboleza kwa mauaji ya kinyama ya binti yao Akwilina! Wanakesha wakilia, “Akwilina! Mungu Baba, Mungu mweke pema Akwilina.” Najaribu kuvaa viatu vya wazazi wake vinanipwaya. Ndugu jamaa na marafiki Tanzania yote tunahuzunika. Ndoto zake zimeyeyuka.
Mungu mwenye haki atahukumu kwa alilotenda. Sisi tunaomba upumzike salama.
Inshallah Mola jalia maumivu yapate kupungua kwa wazazi waliomzaa Akwilina. Alikuwa na ndoto kubwa sana ndiyo maana kwa juhudi akaamua kusoma ili aje aisaidie familia na jamii yake, Tanzania….kila kitu kina mwisho wake, lakini kwanini tuuane? Siasa zina mwisho wake!
Mungu mwenye haki atahukumu kwa alilotenda, tunaomba upumzike salama. Tutaonana tena oh! Akwilina upumzike salama!
Oh! Mwenyezi Mungu, tumekutenda uovu mwingi sisi, tusamehe baba, usikumbuke! Kama sitamwambia baba ukweli huu, basi ulimi wangu na ugandamane na taya zangu!