Na Magrethy Katengu, JamhuriMedia,
Dar es Salaam

Vicent Peter Masawe a.k.a baba harusi mkazi wa Kigamboni Dar es Salaam anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za wizi wa gari aliloazimwa wakati wa harusi yake huku akijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kisha kukimbilia kwa mganga wa kienyeji kujificha na akitengeneza hisia kwa umma kuwa ametekwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 17, 2024 jijini Dar es Salaam Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi SACP Jumanne Muliro amesema Desemba 15 mwaka huu mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya ufuatiliaji na mahojiano ya kina kati ya Polisi na mtuhumiwa na alikiri kutenda makosa hayo ikiwemo kuchukua pesa kwa udanganyifua kutoka kwa watu mbalimbali Tsh milioni 55 na gari na T642 EGU aina ya Toyota Ractis kwa udanganyifu kutoka kwa Syliveter Beda Masawe.

“Vicent Peter Masawe amefanya wizi huu wa kuaminiwa CDS/IR/2066/2024 baada ya kutengeneza mazingira ya uongo ya kupotea kusemekana na Umma ametekwa baadaye kwenda kujificha Pemba Chakechake mgogoni kwa mganga wa kienyeji aitwaye Hamis Khalid” amesema Kamanda.

Sambamba na hayo amebainisha kuwa mtuhumiwa huyo aliendelea na udanganyifu wake kwa kuchukua fedha kwa watu mbalimbali ikiwemo Ramadhani mkazi wa Magomeni milioni 10 , Ramadhani Bakari Mkazi wa Temeke Milioni 15,Resma Mbuguni milion 5 , Asia Mohamed milion 4, Ngoma Mkazi wa Kibaha milioni 1.5 , Fauz Suleimani milion 8 Mkazi wa Tabata baada ya kumuuzia gari ambalo siyo lake aliloazima siku ya harusi yake mali ya Sylivester Beda Massawe.

Kamanda amesema itakumbukwa kuwa Novemba ,2024 Polisi Kigamboni ilipokea taarifa ya kupotea kwa Vicent Peter Masawe Mfanyabiashara ambaye ilidaiwa hakuonekana toka Novemba 18, mwaka huu baada ya harusi yake na alipotea akitumia gari ya Toyota Ractis no T 642 EGU na ilibainika kuwa mtuhumiwa aliiuza gari hiyo badala ya kuirudisha kwa mwenyewe baada ya harusi yake tarehe 16 Novemba, mwaka huu kwenye ukumbi wa Golden Jubilee.

Aidha uchunguzi wa mashauri unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa katika mamlaka nyingine za kisheria kwa hatua zaidi.