Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Geita
Jeshi la Polisi mkoani Geita linamshikilia Elias Bakumye (32), mkazi wa kijiji cha Chikobe, Kata ya Butundwe Wilaya ya Geita mkoani humo kwa tuhuma za kumuua mwanaye mlemavu wa viungo na kumzika porini.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita Kamishina Msaidizi wa Polisi Safia Jongo amesema mtoto huyo alikuwa na umri wa miaka mitano na mwili wake uliokotwa na wasamaria wema Aprili 12, majira ya saa tatu, asubuhi.
Jongo amesema baada ya kupokea taarifa hizo walituma timu ya upelelezi kwenda eneo la tukio ambapo baada ya kufika eneo la tukio walikuta mwili huo.
“Alikaa na mtoto akaona hawezi kuendelea kumhudumia akaamua kumbeba kumpeleka kwa mama yake ambaye alivyofika kule wazazi pamoja na yule mwanamke mtalaka wake wakakataa kumpokea yule mtoto alipofika eneo la porini hapo akakiri kwamba akaona yeye hataweza kumuuguza mtoto huyo akambana pumzi na kumuua na kumfukia” amesema Kamanda Jongo.
Kamanda Jongo amesema mwili ule ulikutwa umeshambuliwa na wanyama na kuonekana kupata michubuko kwenye maeneo tofauti ya ngozi ya mwilini.
Mpaka sasa mtuhumiwa amekamatwa na jeshi hilo la Polisi na taratibu za kisheria zinaendelea na amewataka wakazi wa Geita kutoa taarifa mapema wanapoona viashiria vya ukatili kwenye familia na maeneo wanayoishi.