Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Tabora

MAHAKAMA ya hakimu mkazi Wilaya ya Nzega mkoani Tabora imemhukumu kifungo cha miaka 30 jera Masanja Shija, mkulima na mkazi wa kijiji cha Shila kata ya Isanzu Mkoa wa Tabora baada ya kupatikana na kosa la kushiriki tendo la ndoa na mtoto wake wa kike mara kwa mara mwenye umri chini ya miaka 18.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Nzega Godfey Rwekite amesema kuwa kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, mahakama imeridhishwa na ushahidi huo wa upande wa mlalamikaji.

Hakimu amesema adhabu hiyo iwe fundisho kwake na kwa watu wengine wenye nia na tabia kama hizo za kufanya vitendo vya ukatili kwa watoto wao wa kike.

Kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka walipo wilayani Nzega wakiongozwa na Jenipher Mandago waliieleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo ni ya jinai namba 90/2021 ambapo Desemba 2,2021 majira ya usiku, mshtakiwa Masanja Shija alikutwa akifanya tendo la ndoa na mtoto wake wa kike mwenye umri chini ya miaka 18.

Mawakili hao wa Serikali waliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine wenye nia ovu na wanaoendekeza vitendo vya kikatili katika Wilaya ya Nzega na nchini kwa jumla.

Kabla ya kutiwa hatiani mshtakiwa alipewa nafasi ya kujitetea ambapo aliiomba mahakama impunguzie adhabu kutokana na kuwa na familia inayomtegemea.