Habari za kufukuzwa kazi Jenerali Kale Kayihura katika nafasi ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) na Luteni Jenerali HenryTumukunde kama waziri wa ulinzi zimepokelewa kwa hisia tofauti na wasomaji wa mitandao nchini Uganda.

Wengi wa wachangiaji katika mitandao ya jamii wamemkosoa Rais Museveni katika hatua yake ya kuwafukuza viongozi hao na wengine wamewafurahia na kusema ilikuwa ikitegemewa kuwa hilo litatokea na pengine hatua hiyo imechelewa sana kuchukuliwa.

Wananchi wengine wa Uganda wanasema mabadiliko yalikuwa yanahitajika, hasa ukizingatia kiwango cha uhalifu kilivyokuwa kinaongezeka nchini Uganda, na ukweli wa kuwa majenerali hao walikuwa wameripotiwa kutokuwa na maelewano. Badala ya kukaa pamoja na kutafuta njia za kutatua tatizo lililokuwa linaongezeka la ukosefu wa amani wao walikuwa wako katika mivutano.

Kwa upande wa wale waliokuwa na sikitiko juu ya kufukuzwa majenerali hao wawili kupitia mitandao ya jamii wamesema kuwa pengine walikuwa wanafanya bidii kabisa kwa kadiri wawezavyo kuondoa uhalifu pamoja na kukabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile ukosefu wa fedha na mahitaji mengine ambayo yako nje ya uwezo wao.

Museveni alimuondoa Jenerali Kayihura na kumweka badala yake Martin Okoth Ochola ambaye amekuwa naibu wake.

Kamanda wa jeshi la polisi mstaafu Brig Sabiiti Muzeei ni IGP mpya hivi sasa. Pia Museveni amemfukuza Luteni Jenerali Henry Tumukunde kama Waziri wa Ulinzi na kumweka Jenerali Elly Tumwine.