Vipimo ni muhimu sana kwa maendeleo ya afya zetu, kwa watu wa jinsia zote na rika zote. Kupitia vipimo tunaweza kutambua mustakabali wa afya zetu, hivyo kujiweka kwenye nafasi nzuri katika kupambana na maradhi mbalimbali.
Hivi karibuni takwimu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) zilionyesha kuwa idadi ya wanaume watu wazima wanaopatiwa vipimo vya afya ni ndogo kuliko idadi ya jinsia nyingine.
Kama nilivyokuahidi katika toleo lililopita, leo tutaendelea kukumbushana aina ya vipimo ambayo unapaswa kuvipata na kufahamu majibu yake.
Vipimo vya shinikizo la juu la damu
Hatari ya kupata shinikizo la juu la damu huongezeka kadiri umri unavyosogea, lakini pia shinikizo la juu la damu lina uhusiano mkubwa na uzito wa mwili kupitiliza na aina ya maisha, kama vile ulaji wa vyakula vyenye mafuta kwa wingi na kutofanya mazoezi ya viungo mara kwa mara na sababu za kisaikolojia.
Shinikizo la juu la damu humpata mtu bila dalili zozote, na linaweza kuleta madhara makubwa mengine ya kiafya kama vile magonjwa ya moyo, kiharusi na hata kusababisha figo kushindwa kufanya kazi.
Hivyo, ni muhimu kujua vipimo vyako vya shinikizo la damu mara kwa mara na kama vinaashiria kupanda ni vema kupata msaada wa daktari mapema.
Vipimo vya kisukari
Kisukari ni ugonjwa unaowapata watu wa jinsia zote lakini takwimu zinaonyesha kuwa wanaume wapo hatarini zaidi kupata kisukari kuliko wanawake. Ni ugonjwa unaotokana na uwepo wa kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu.
Huenda ikasababishwa na aina fulani ya maisha kama vile ulaji wa aina fulani ya vyakula vinavyosababisha kisukari, kutofanya mazoezi, lakini hata sababu za kifamilia zinazotokana na kurithi.
Japo kisukari pia kinaweza kuwapata watu wa rika zote, lakini inashauriwa pia ni vema kwa wenye umri wa kuanzia miaka 45 kupata vipimo vya kisukari mara kwa mara kwa kuwa kisukari pia kinawapata zaidi watu wenye umri wa utu uzima na kuendelea.
Vipimo vya glakoma
Glakoma huenda likawa ni neno geni miongoni mwa wengi, jina hili linaunganisha makundi ya magonjwa ya macho ambayo husababisha kuharibu neva zilizomo ndani ya macho na hatimaye kusababisha upofu wa kudumu. Glakoma inaweza kutokea bila kuambatana na dalili yoyote hadi pale mgonjwa anapojikuta amekuwa mpofu ghafla.
Ni muhimu kupata vipimo vya macho mara kwa mara kubaini madhara yoyote yanayoashiria kujitokeza kwenye macho. Ni kweli kwamba watu wengi hawana utamaduni wa kupima macho mara kwa mara.
Ugonjwa huo huwa na dalili mbalimbali kwenye macho kama vile matatizo ya kuona, macho kuuma na kuwasha na hata kutoa machozi. Ni vema ikafahamika kuwa glakoma inashambulia jicho bila kuambatana na dalili zozote.
Hivyo, ni vema kufanya vipimo mara kwa mara hata kama unahisi hauna tatizo lolote kwenye macho yako. Vipimo vya glakoma vinashauriwa kufanyika kwa kuzingatia umri na mazingira hatarishi ya kupata ugonjwa huu kwa mtu husika.
Kwa wenye umri wa miaka chini ya 40, wafanye vipimo angalau kila baada ya kipindi cha miaka miwili hadi minne, kwa wenye umri wa miaka 40-54 wanashauriwa kufanya vipimo angalau kila baada ya mwaka 1-3 na kuanzia umri wa miaka 55 na kuendelea wanashauriwa angalau kufanya vipimo angalau mara mbili kwa mwaka mmoja.