*Waunda mfumo huru kusikiliza malalamiko ya wananchi, waathirika kujenga ‘Mwadui Mpya’
SHINYANGA
Na Antony Sollo
Kampuni ya Petra Diamond Limited (PDL) inayochimba almasi Mwadui, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, imeanzisha mfumo utakaomaliza migogoro ya muda mrefu na jamii inayoizunguka.
Uanzishwaji wa mfumo huo ni utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa baina yake na Kampuni ya Leigh Day ya Uingereza inayoshughulikia masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Akizungumza wiki iliyopita, mshauri wa Petra Diamond Limited, Bahame Nyanduga, anasema PDL wapo katika mchakato wa kuutambulisha mfumo huo huru.
“Mfumo huu utakatumika kusikiliza malalamiko ya wanajamii kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanyika mgodini,” anasema Nyanduga.
PDL ni mwekezaji katika Kampuni ya Williamson Diamond Limited (WDL) na hawatahusika katika kuusimamia mfumo huru uliobuniwa, bali ukishaanzishwa, utajiendesha wenyewe kwa miaka miwili.
Nyanduga anasema taarifa za uendeshaji zitatolewa na wataalamu huru na kwamba mfumo unatarajiwa kuongeza uwajibikaji na umadhubuti katika utendaji wake.
“Ni muundo shirikishi wa mfumo huru wa malalamiko utakaokuwa na vitengo vitano vitakavyohusika na mchakato mzima wa usimamizi wa malalamiko kutoka kwa wanaodai kufanyiwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu,” anasema.
Muundo unaonyesha kuwapo kwa sekretarieti itakayojumuisha wataalamu wa utawala, fedha, rasilimali watu, utoaji ushauri na usimamiaji wa kuandikisha na kutekeleza uamuzi wa ‘Jopo Huru’ na ‘Jopo la Rufani’.
Kutakuwapo pia uwakilishi kupitia wanasheria kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wanaodai kuvunjiwa haki zao.
Pia kutakuwapo na timu ya uchunguzi (Fact Finding Team) kuchunguza madai yote ili kubainisha ushahidi na vielelezo muhimu, kisha kutoa tathmini kwa ‘Jopo Huru’.
Jopo hilo lenye wataalamu litachambua malalamiko yote kwa vigezo vya sheria za madai na ushahidi husika.
“Uamuzi wa ‘Jopo Huru’ la watalamu unaweza kukatiwa rufani na kusikilizwa na ‘Jopo Huru la Rufani’. Mlalamikaji atakuwa huru asiporidhika na uamuzi wa jopo lolote kupeleka malalamiko yake mahakamani,” anasema Nyanduga.
Na kitengo cha mwisho katika muundo wa mfumo huu ni cha ‘Mfuatiliaji/Msimamizi Huru’.
JAMHURI limeelezwa kuwa uteuzi wa watendaji ndani ya mfumo utazingatia taaluma na usawa wa jinsia baada ya usaili wa wazi kwa watakaoomba nafasi.
“Sifa za Mfuatiliaji au Msimamizi Huru ni uzoefu katika sheria za Tanzania au za kimataifa, hasa sheria za biashara ya kimataifa na haki za binadamu.
“Mtu anayetambulika kuwa ni huru asiyekuwa na upendeleo (kutofungamana na upande wowote). Mfuatiliaji Huru anatakiwa kuwa na sifa ya kusimamia haki,” anasema.
Majukumu yake ni kutathmini kwa ufanisi utendaji wa Mfumo Huru na mwishowe awe tayari kutoa taarifa mara mbili kwa mwaka kila baada ya miezi sita na kutangaza, kusambaza taarifa kwa wadau wote.
Taarifa hizo zinapaswa kuwekwa kwenye tovuti ili zipatikane kwa kila anayependa kujua utendaji na ufanisi wa mfumo huo huru.
Nyanduga anasema kila idara ndani ya mfumo itafanya kazi ikiwa huru bila kuingiliwa na chombo chochote.
“Kitu muhimu tunachoomba hapa ni kwa jamii (wananchi) kutuamini au kuuamini mfumo huu, kwani hautamuonea yeyote. Utafanya majukumu yake kwa haki na kwa kuzingatia sheria za nchi,” anasema mtaalamu huyo na mwanasheria.
JAMHURI limezungumza na Meneja Uhusiano wa WDL, Bernard Mihayo, kuhusu nini kinachoendelea kwa sasa mgodini.
“Ni maridhiano tu. Uongozi wa mgodi umeamua kwa nia thabiti kurejesha uhusiano mwema na jamii, hasa wananchi wa vijiji vinavyozunguka WDL.
“Ni vijiji kama 12 hivi. Tunawaomba wafahamu na kuamini kuwa wao ni wadau muhimu wa mgodi. Waache tabia ya kuvamia maeneo yasiyoruhusiwa kisheria.
“Tumeamua kuja na mfumo mpya wa ushirikishaji jamii katika masuala yote yanayohusu uwekezaji kwenye maeneo yao. Hili, awali lilikuwa na udhaifu, lakini sasa tunatarajia kupeleka miradi mbalimbali kwa jamii. Hakika tunatamani kuiona ‘Mwadui mpya’,” anasema Mihayo.
Mwanasheria wa WDL, Sylvia Mulogo, anasema kampuni hiyo imeanzisha kitengo cha Uhusiano wa Umma ili kuimarisha ujirani mwema na jamii inayouzunguka mgodi.
“Mwaka 2021, PDL na WDL tulishtakiwa na mawakili wanaojihusisha na utetezi wa Haki za Binadamu wa Leigh Day waliopo Uingereza.
“Baada ya mazungumzo, tulifikia makubaliano ya kutenga fedha kwa ajili ya uundaji wa Mfumo Huru wa kusikiliza malalamiko ya waathirika wa ukiukwaji haki za binadamu katika Mgodi wa Mwadui,” anasema.
Sylvia anasema makubaliano yalifikiwa mbele ya Mahakama Kuu ya Uingereza, jijini London na sasa yanatekelezwa ambapo pande mbili zimekubaliana kwa dhati kabisa.
Anasema katika kuhakikisha Mfumo Huru usiokuwa na upendeleo unaundwa, wameshirikisha taasisi na wadau mbalimbali wa haki za binadamu ikiwamo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Anazitaja taasisi hizo kuwa ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jeshi la Polisi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mkoa wa Shinyanga, Wilaya ya Kishapu na viongozi wa kijamii ngazi ya vijiji vinavyozunguka mgodi.
Nyingine ni taasisi za kiraia kama Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), CBOs na viongozi wa dini.
“Ndiyo maana tuna imani mfumo huu utakapoanza utaifanya jamii kuwa huru kuwasilisha na kusikilizwa malalamiko yao bila upendeleo,” anasema.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa taasisi za dini na asasi za kiraia, Mwinjilisti Bernard Mussa, kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Idukilo, anasema ni matarajio yao kuwa uhusiano wa jamii na mgodi utaimarika.
“Lazima tuwashukuru sana kwa kuja na mpango huu na kuweka huru ukusanyaji wa maoni ya wadau kuhusu namna bora ya utendaji wa mfumo huru wa usikilizwaji wa malalamiko.
“Mfumo huru wa usikilizwaji wa malalamiko hayo utaimarisha ujirani mwema baina ya mwekezaji na jamii,” anasema Mwinjilisti Mussa.