Baada ya viongozi wa Yanga kuzidi kuachia ngazi akiwemo Kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo jana, Clement Sanga kutangaza kujiuzulu wadhifa wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Hussein Nyika, ameitisha kikao na wahabari leo.
Nyika ameitisha kikao hicho kuzungumzia mustakabali mzima wa Yanga juu ya kujaza nafasi za viongozi wake walioachia ngazi namna utakavyokuwa.
Ikumbukwe Yanga imekuwa haina Mwenyekiti kwa muda mrefu tangu kujiuzulu kwa Yusuf Manji akidai anahitaji kupumzika kutokana na kukabiliwa na majukumu mengi binafsi.
Baada ya Manji, wajumbe kadhaa wa Kamati ya Utendaji akiwemo Salum Mkemi na Khalfan Hamis nao wameachia ngazi kutokana na kutokuwa na maelewano mazuri baina yao na uongozi wa juu wa klabu.
Kutokana na kujizulu kwao, uongozi wa Yanga kupitia kwa Nyika utaeleza kiunagaubaga leo hatma ya nafasi zao ikiwemo suala la uchaguzi wa kujaza nafasi ya Mwenyikiti pamoja na ile ya Katibu Mkuu.