Tanzania imeendelea kuimarisha uhusiano wa kidugu na kibiashara na mataifa jirani baada ya wiki iliyopita Rais Samia Suluhu Hassan kufanya ziara ya siku mbili nchini Burundi.
Nchi hiyo ni moja ya majirani wanaopakana na Tanzania upande wa magharibi, ikiitegemea sana nchi yetu kiuchumi kwa kupitishia bidhaa zake katika Bandari ya Dar es Salaam.
Kuwa na uhusiano mzuri na taifa hili dogo ni muhimu kwa uchumi wa pande zote mbili lakini zaidi hasa kwa wakazi wa mikoa ya mpakani, yaani Kigoma na Kagera wanaojishughulisha na biashara.
Kwa sasa Burundi imetulia kisiasa baada ya miaka kadhaa ya misukosuko na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayochochewa na chuki za kihistoria katika siasa na makabila.
Umuhimu wa Burundi kwa uchumi wa Tanzania ni sawa na umuhimu wa taifa jingine kubwa lililopo magharibi ya nchi yetu; Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Amani inayoendelea kwa sasa mashariki mwa DRC inatoa fursa nzuri kwa wafanyabiashara wa Tanzania kunufaika kiuchumi, kwani taifa hilo lina fursa nyingi za kibiashara.
DRC na Tanzania zimetenganishwa na Ziwa Tanganyika lililojaa fursa nyingi ambazo hazijatumiwa ipasavyo ama kwa serikali kutohamasisha wananchi kuzitumia, au kwa kutofahamika kwa wengi.
Mpaka wa mataifa haya ni miongoni mwa mipaka mitatu mirefu zaidi nchini, pamoja na mpaka wa Kenya uliopo kaskazini na ule wa Msumbiji uliopo kusini mwa Tanzania.
Takwimu zinaonyesha wazi pia kwamba DRC ndilo taifa linalopitisha mizigo mingi zaidi katika Bandari ya Dar es Salaam, ikimaanisha kwamba wafanyabiashara wengi wa huko wanaufahamu umuhimu wa bandari hiyo.
Kwa bahati mbaya, mikoa inayopakana na DRC haionekani kunufaika kiuchumi na uwepo wa taifa hilo lenye rasilimali nyingi zaidi barani Afrika.
Karibu biashara zote zinazofanyika Ziwa Tanganyika ni haramu na ndiyo maana tunashauri serikali kuingilia kati na kuzirasimisha biashara hizo kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Hakuna ziara ya kiongozi mkubwa wa kitaifa iliyowahi kufanywa eneo la mashariki ya DCR katika majimbo ya Katanga na Tanganyika na kuhamasisha uhusiano wa kibiashara mpakani pamoja na ujirani mwema.
Tunaamini kwamba wakati umefika sasa kwa Serikali ya Awamu ya Sita kuchochea maendeleo ya mikoa iliyo pembezoni na namna mojawapo ya kufanya hivyo ni kufungua biashara rasmi maeneo hayo.
Tuna uhakika kwamba biashara kati ya DRC na Tanzania inaweza kuwa kubwa na yenye manufaa zaidi kwa taifa kuliko biashara zinazofanyika kati ya nchi yetu na majirani wengine, kutokana na ukweli kwamba wingi wa watu mashariki ya DRC kunalifanya eneo hilo kuwa soko kubwa na zuri zaidi la bidhaa za Tanzania.