Bao pekee la kinda Shabani Idd limeipelekea Azam FC ambao ndiyo mabingwa watetetzi wa kombe la Mapinduzi fainali ya michuano hiyo

Mabingwa watetezi wa Kombe la Mapinduzi Azam FC, huneda wakafanikiwa kulibakisha kombe hilo nchini baada ya leo kufanikiwa kuingia fainali kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Singida United katika mchezo wa nusu faianli ya pili uliopigwa uwanja wa Amaan Zanzibar.

Bao hilo pekee la Azam lilifungwa dakika ya 74 na kiungo chipukizi Shabani Idd , aliyeingia muda mfupi kuchukua nafasi ya Yahya Yazid ambaye alionekana kuchoka baada ya kazi kubwa aliyoifanya kwenye mchezo huo.

Singida United pamoja na kutolewa lakini walionyesha ushindani wahali ya juu kiasi cha kumpa presha kocha wa Azam FC Mromani Aristica Cioaba ambaye alitua nchini januari 2017, wakati timu hiyo ikishiriki michuano hiyo ya Mapinduzi na kuishuhudia ikitwaa ubingwa chini ya kocha wa muda Idd Cheche.

Katika mchezo huo Singida waliuanza mchezo kwa kasi na washambuliaji wake Danny Lyanga, Lubinda Mundi na Kambale Salita walionekana kushindwa kuzitumia vyama nafasi walizozipata kwenye mchezo huo huku kipa Razak Abalora akifanya kazi kubwa ya kupangua hatari ambazo zilielekezwa langoni mwake.

Mshambuliaji wa Azam FC Bernald Authur alipoteza nafasi mbili za wazi za kuweza kuifungia timu yake lakini  mabeki wa Singida United Kennedy Juma, Malik Antir na Shafik Batambuze ambaye aliibuka mchezaji bora wa mchezo huo waliweza kutimiza vyema majukumu yao uwanjani.

Hadi filimbi ya mwisho ya mwamuzi Rashid Farhan ni Azam ndiyo walioibula na ushindi na kutinga fainali kwa mara ya pili mfululizo na sasa watapambana na URA katika mchezo wa fainali ambao utapigwa Jumamosi uwanja wa Amaan hapa Zanzibar.