Na Tatu Saad,JAMHURI MEDIA
Matajiri kutoka Chamazi, Azam FC wameanza kujitafakari ili kufanya vizuri katika michezo ya ligi kuu iliyosalia msimu huu wa 2022/23, baada ya kuchemsha kwenye baadhi ya michezo waliyocheza hadi sasa.
Akizungumza kocha msaidizi wa Azam FC,Kally Ongala amesema hatua ambayo timu hiyo imefikia imebidi benchi la ufundi pamoja na wachezaji wajitathmini iki kufanya vizuri katika michezo iliyosaliamsimu huu 2022/23.
Ongala amesema kitendo cha kutokuwa na matokeo mazuri kiliwavuruga wachezaji kisaikolojia lakini wamekaa nao chini na kuwaweka sawa na ana imani watakuwa na matokeo mazuri katika michezo iliyosalia.
Tumejitafakari, tumeongea na wachezaji wetu na kikubwa tumewaambia wanatakiwa kupambana kwa kila ambaye anapata nafasi ya kucheza,” amesema Ongala na kuongeza;
“Wachezaji wanatakiwa kujitafakari lakini na sisi Benchi la Ufundi tufanye hivyo lengo likiwa ni kurudi katika hali yetu ya kawaida katika mechi zilizosalia.”
Azam FC inashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 47 baada ya kucheza michezo 25 huku mwanzoni mwa msimu ilianza vizuri na kuonyesha inaleta ushindani katika Ligi hiyo.